Anthony Komu: Aitwa kuwa mbunge Moshi Vijijini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
ANTHONY Bahati Komu

ANTHONY Bahati Komu, mkurugenzi wa fedha na utawala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amejitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni Moshi Vijijini.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI mwishoni mwa wiki mjini Moshi, Komu ambaye ni mwanasiasa aliyetokea katika harakati za kupigania wanyonge, anasema ameamua kutangaza mapema azma yake ya kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya kushawishiwa na baadhi ya wananchi na marafiki zake.

Anasema, “Nimekuwa nikiulizwa karibu kila mahali katika Jimbo la Moshi Vijijini, iwapo nitagombea tena ubunge mwaka 2010. Swali hili limekuwa likiulizwa kwa namna mbalimbali, kama ombi, kama lawama, kama onyo au tahadhari ya kutowaacha wananchi hawa kwenye mataa.”

Akiwa kiongozi, Komu anasema ameona ni muhimu ajibu kiu ya wananchi kwa kutoa “majibu kwa kila swali ninaloulizwa” na kwamba huo ndio msingi wa uongozi.

Anasema, “Maswali yote haya katika tafakari yangu na baadhi ya wananchi yanaonyesha kuwa kuna walakini katika uwakilishi tulionao bungeni.”

Jimbo la Moshi Vijijini hivi sasa linawakilishwa na Dk. Cyrill Chami, naibu waziri wa biashara, viwanda na masoko ambaye Komu anamtuhumu kushindwa kutetea wananchi na badala yake amejiweka katika kwapa la watawala.

Anasema, “Mbunge wetu anawajibika kwa utawala badala ya wananchi. Tabia hiyo na hulka hiyo ya mbunge ndiyo imetusababishia kuwa nyuma kimaendeleo.”

Komu ambaye amejijengea historia ya kuwa miongoni mwa vijana wachache waliojiunga na mageuzi hata kabla ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa, anasema katika jimbo hilo kuna mambo mengi ambayo hayajafanyiwa kazi na hayawezi kufanyiwa kazi chini ya uongozi wa Chami na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema Moshi Vijijini kuna matatizo ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na hakuna matumaini ya kuyapatia chini ya uwakilishi wa sasa.

“Kila anayewatakia mema wananchi wale ni shahidi, kwamba hali ya uchumi wa jimbo letu inaporomoka kila kukicha, vyanzo vya mapato vimekufa, zao la kahawa linateketea, miundo mbinu kwa ajili ya umwagiliaji inaendelea kutoweka; jambo lililosababisha hata mazao kwa ajili ya chakula kupungua kwa kiasi kikubwa,” anasisitiza.

Anasema, “Si hivyo tu, kuna tatizo jingine kubwa na la msingi. Uwezo wa wananchi wa Moshi Vijijini kusomesha watoto wao, unapungua kila mwaka. Nikiwa mwananchi wa Moshi Vijijini, lazima nishiriki katika kupatikana majibu sahihi ya matatizo yaliyopo.”

Akiongea kwa kujiamini, Komu anasema “Hatuhitaji miujiza kuondokana na matatizo yanayotukabili jimboni kwetu, tunahitaji uongozi na uwakilishi wenye nia ya dhati ya kumwendeleza mwananchi wa kawaida.”

Anatoa mfano wa mashamba yao na kuuliza, “ni kwanini vihamba yetu visipimwe tukapata hati, hadhi na uwezo wa kupata mikopo ya benki ya kufanyia biashara? Kwa nini viongozi wetu wasisimamie hili na tukarudi katika enzi zetu za ustawi?” anahoji.

Anasema, CCM imeshindwa kutoa majibu sahihi kwa matatizo hayo. Badala yake viongozi wengi wa chama hicho wamejitumbukiza katika utafutaji mali kwa njia ya mikondo michafu, kama vile Richmond, ukwapuaji katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) na ununuzi wa rada.

Anasema, “Kuibuka kwa kashfa hizi za wizi wa fedha za umma, kwa njia ya mikataba na kiholela, hasa katika kipindi hiki ambacho viongozi wa CCM  wamekiri kwamba rushwa ni donda ndugu ndani ya serikali, kunathibitisha kuwa chama hiki kimeshindwa kutimiza wajibu wake.

“CCM imeshindwa kusimamia rasilimali za taifa; imeshindwa kulinda na kutetea dhamana walizopewa,” anaeleza Komu kwa sauti ya utulivu na kujiamini.

Komu ambaye alijiunga na vyama vya mageuzi, wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwanzoni mwa miaka ya tisini, historia yake imejikita zaidi katika mapambano ya wanyonge dhidi ya mabwenyenye.

Komu anasema hawezi kurudi nyuma na kwamba hana sababu ya kufanya hivyo, kwani anataka kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa faida ya wananchi wengi.

Anasema anajua ilivyo ghali kuwa katika upinzani wa kiasiasa katika nchi kama hii. Lakini pamoja na gharama hiyo, ataendelea kupigania kile anachokiamini, tena bila kurudi nyuma.

Akizungumzia madai ya baadhi ya viongozi wa CCM kuwa CHADEMA kimekuwa kikitumia vibaya fedha za wahisani, Komu anasema madai hayo hayana msingi na yamelenga kukipaka matope chama chake.

“CHADEMA ndicho chama pekee kilichoweka hadharani hesabu zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Hizo ni fedha tulizozipata kutoka chama cha Conservative cha Uingereza. Maelezo ya fedha hizo yalitolewa wazi kwenye ripoti ya hesabu zetu. Pikipiki tulizo nazo nchini ni nyingi sana kuliko zinazosemwa na CCM,” anafafanua.

Lakini jambo la msingi, anasema Komu, ni wananchi kufahamu kwamba CCM kuna matatizo makubwa yanayohitaji majibu kuliko hata katika CHADEMA. “Wao, CCM wanaeneza porojo mitaani ili kukichafua chama chetu,” anaeleza.

Anasema, “CCM inapata ruzuku ya Sh. 2.34 bilioni kwa mwezi wakati CHADEMA inapewa Sh. 61milioni. Hesabu hizo za CCM ziko wapi? Za kwao wanazifanyia nini? Viongozi wa CCM waseme haya.

“CCM ina mapato mengine yanayotokana na viwanja vya michezo kama vile Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Uwanja wa Maji Maji Songea na vingine vingi. Imechukua majengo mengi ya umma. Mapato yote hayo, hesabu zake ziko wapi? Haya ndiyo majibu ambayo wananchi wanayataka siyo kuichafua CHADEMA,” anaeleza Komu kwa utulivu.

Anasema imekuwa ni tabia ya baadhi ya viongozi wa chama hicho kuchukua hoja dhaifu na kuzifanyia poropaganda ili kujenga sumu kwa wananchi kuwa CHADEMA kuna matatizo. “Jambo hili si kweli na si sahihi hata kidogo,” anaeleza.

“Kwa zaidi ya miaka 40 sasa, taifa hili limekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na vitendo haramu vya kutumia fedha kuingia madarakani vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa hasa kutoka CCM. Haya ndiyo mambo ya msingi ya kujadili kama taifa, siyo kukimbilia hoja dhaifu,” anasisitiza.

Akizungumzia hoja ya vyama kushirikiana katika uchaguzi ujao, hoja ambayo imekuwa ikipigiwa chapuo zaidi na mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Komu anasema ushirikiano wa vyama ni kitu kizuri kama kuna uadilifu ndani yake.

“Kama mnazungukana, mnasalitiana kama ilivyokuwa katika uchaguzi mdogo katika jimbo la Tarime, sioni sababu ya vyama kuungana na kushirikiana,” anaeleza Komu.

Anasema CHADEMA hakina matatizo na vyama adilifu. “Tumezungumza sana. Sasa tunatafakari. Siyo mambo ya kuendelea nayo. Approach (mwelekeo) wetu ni very reconciliatory (ni wa maafikiano). Nchi ni yetu tuiendeshe pamoja. Tofauti zetu ni ndogo kuliko matatizo yanayoikabili.”

Hata hivyo, Komu anaonya kuwa wanasiasa waliojiweka katika kwapa la CCM na mgombea wao, Rais Jakaya Kikwete hawana nafasi katika kujadili suala hilo.

Komu ameona na ana watoto watatu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: