Anusurika kifo mara saba baharini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

MIONGONI mwa watu wanaosisimka mwili kila wanaposikia taarifa za ajali za majini ni Yusuf Zuberi, mkazi wa kijiji cha Kizingani, wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.

Zuberi ni mvuvi. Alizaliwa mwaka 1945. Anasema aliposikia Watanzania wengi wamekufa majini katika ajali ya meli ya m.v. Spice Islander I, alijawa na kumbukumbu za ajali.

“Nimenusurika kufa majini mara saba, wee acha tu!” anasema Zuberi ambaye anakiri hakuwahi kwenda shule.

Mtoto wa tatu katika familia ya watoto 10, mvuvi huyu anasema mara ya kwanza kunusurika kufa ilikuwa Mei 25 mwaka 1965.

Mtumbwi wake ulipasuka kwa chini baada ya kugonga mwamba na kuingiza maji ambayo alishindwa kuyatoa na kusababisha chombo chake kuzama.

“Nilikaa majini kwa saa tano mpaka boti ilikuja kunifuata baada ya kuniona kwa kupitia mnara wa kuongozea meli wa Ulenge,” anakumbuka.

Anasema tukio la pili lilikuwa Desemba mwaka 1969 ambapo mtumbwi wake ulizama na kusababisha akae majini kwa zaidi ya saa saba.

“Hapa niliokolewa na wavuvi wenzangu,” anasema.

Zuberi anakumubuka pia kilichotokea tarehe 20 Aprili 1982. Upepo ulikuwa mkali; bahari ikachafuka; mara hii alikuwa na ngarawa. Akawa anapigwa na upepo na mawimbi huku na kule.

Anasimulia jinsi alivyozamishwa na maji na kusota kwa saa tisa kabla ya wavuvi waliokuwa wakipita kumuona na kumuokoa.

Akielezea tukio la nne, ambalo anasema “lilitaka kuchukua maisha yangu,” Zuberi anasema alikaa majini kwa zaidi ya saa 20. Vilevile aliokolewa na wavuvi wenzake. Hii ilikuwa Januari 1992. Anasema hilo ndilo tishio kubwa kuliko yote maishani mwake.

Matukio ya kipigwa na upepo na mawimbi; mtumbwi kujaa maji na kuzama yalimkumba Zuberi pia mwaka 1999, 2001 na tarehe 3 Januari mwaka huu.

Akikumbuka ya mwaka huu alisema, “Ngalawa yangu ilizamishwa. Nikakaa majini kwa saa tatu. Nilipata msaada kutoka mashua ya abiria  iliyokuwa ikitokea Pemba kwenda Tanga.”

“Angalia yote niliyokueleza. Hakuna popote ambako serikali imetoa msaada. Kumbuka yanayonipata mimi ndiyo yanawapata wavuvi wengine wengi. Wao (serikali) hufuata kodi tu,” analalamika.

Zuberi alianza kuvua akiwa na umri wa miaka 15. Alifundishwa na mjomba wake aitwaye Rashidi Mzaka (85) ambaye anaishi Sahare mkoani Tanga.

0
No votes yet