Arumeru: Tupime wagombea siyo wapiga debe


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

TWENDE Arumeru Mashariki ambako kampeni za uchaguzi mdogo zinaendelea. Washindani wakuu ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA).

Viongozi wa CCM wanadai katika mikutano yao kuwa CHADEMA inawadanganya wananchi kuwa itatatua matatizo yao.

Kwa upande mwingine CHADEMA inadai kuwa CCM inawahadaa kuwa itatatua matatizo, wakati imeshindwa kufanya hivyo kwa miaka yote.

Pamoja na vijembe vya wapiga debe, mameneja wa kampeini na makada wengine, hatimaye uwezo wa mgombea ndicho kigezo cha msingi. Sasa tujadili.

Matamshi mengi ya wanasiasa katika kampeni hizi yanaacha maswali mengi, ikiwa kweli wanasiasa hawa wanamaanisha kile wanachokisema.

Mathalani, inawezekanaje Waziri Stephen Wassira asimame jukwaani kumnadi mgombea wa CCM, Sioyi Sumari kuwa anafaa kuwa mbunge wa Arumeru Mashariki?

Katika kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichojadili wagombea, Wassira alisimama kidete kupinga Sioyi kuteuliwa kwa madai kuwa alihonga wapiga kura.

Ni Wassira aliyemkumbusha mwenyekiti wa kikao, Jakaya Kikwete kuwa katika hotuba yake mkoani Mwanza wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya chama chake, alikemea tabia ya wagombea kutumia fedha kununua wapiga kura.

Je, inawezekana vipi, leo Wassira asimame na kusema Sioyi anafaa kuwa mbunge?

Au tukichukulia matamshi ya rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa matatizo ya ardhi ya eneo la Arumeru yatatatuliwa hivi karibuni na kwamba atamwambia mwenyekiti wa CCM ili amalize tatizo hilo. Hili nalo linaashiria ulaghai mwingine wa hali ya juu.

Ardhi ya Wameru iliuzwa kwa wawekezaji chini ya utawala wa Mkapa. Na tangu hapo serikali inajua nini kinaendelea katika eneo la Meru. Haiingii akilini kuwa serikali ilisubiri Jeremiah Sumari afe ndipo iwaambie Wameru kuwa itashughulikia suala la ardhi yao.

Inatia shaka mtu wa heshima kama Mkapa kudanganya umma kwa ajili tu ya kumpatia kura mgombea wa CCM.

Ingekuwa nafuu kama hata angewaambia Wameru kuwa ardhi ile sasa ni mali ya wawekezaji, na serikali itaingia katika mazungumzo nao ili wakubali kuachia sehemu ya ardhi kwa matumizi ya wakazi wa Meru.

Mkapa aliendelea kudanganya umma na hata kujiingiza katika siasa za kuchafuana pale alipodai Vincent Nyerere si mwana familia ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Hili halikunishangaza, kwa sababu niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Mkapa akihutubu bila karatasi, huwa anafyatuka na kuropoka mambo ya hatari.

Aliwahi kufyatuka na kuwatukana viongozi wa dini, wanahabari na hata Watanzania kwa jumla.

Hivi sasa wale wajumbe wa Kamati Kuu waliopinga pendekezo la kumuomba kuzindua kampeni wanashangilia kwa sababu walichoonya kimetokea.

Kampeni za ubunge wa Arumeru Mashariki zimegeuka kuwa mgogoro kati ya serikali na familia ya Baba wa Taifa. Lile onyo, la wanaoona mbali, kuwa Baba wa Taifa awe baba wa wote na kamwe asihusishwe na itikadi za vyama, sasa limeeleweka.

Kama Mkapa anapenda kubaki na heshima kidogo kabla ya kutoweka duniani, afikirie mara mbili kujihusisha na siasa za vyama. Ni bora angeitwa mchawi, fisadi kama anavyoitwa, kuliko kuitwa na “muongo na muuaji wa Nyerere.”

Uongo mwingine wa , lakini unafichwa kwa ustadi mkubwa, ni juu ya uwezo wa kiuongozi alionao mgombea Sioyi Sumari.

Mpaka sasa, Sioyi hajaonyesha uwezo wake kama kweli anaweza kumudu mikiki ya siasa za ushindani. Hali hii imesababisha hata wale wanaomnadi kuanza kumpamba kwa sifa zenye walakini.

Kwa mfano, Wassira amedai Sioyi ni mpole na mstaarabu. Livingstone Lusinde akadai Sioyi apewe ubunge ili kumfuta machozi ya kufiwa na mzazi wake, na kwamba hii itasaidia kumpa mshahara wa kutunza familia.

Wapiga kampeni wanapofikia kutumia vigezo hivi kumnadi mgombea; ujue wamekosa sifa nyingine za maana.

Sioyi hajajipambanua kama mtetezi wa haki za wananchi wake; kama mtu makini anayeweza hata kutofautiana na chama chake pale kitakapoonekana kutaka kupotosha mambo.

Aidha, Sioyi hajaonyesha kama anaguswa na matatizo ya wananchi anaotaka kwenda bungeni kuwatetea.

Hali hii inazalisha tatizo jingine: Uongo wa hatari. Inapotokea katika kampeini, mgombea akafunikwa na wanaomnadi, inajengeka fikra kuwa jimbo hilo litaongozwa na watu wengine, siyo yule anayetaka kuchaguliwa.

Lakini hawa watu – mathalani, Nchemba Mwigulu na Stephen Wassira, wana majimbo yao. Hata haya wanayosema jimboni Arumeru hawawezi kamwe kuyasema kwao.

Hatimaye, wananchi wa Meru watahitaji kubaki na mbunge wao; wakae naye na kupanga mikakati ya kujiletea maendeleo. Sioyi hataweza kuwaambia wananchi wake kuwa wasubiri amuite Mchemba au Wassira wamsaidie.

Jambo hili pia linamgusa Edward Lowassa ambaye anahusishwa, kwa karibu, na mipango ya Sioyi kugombea nafasi iliyoachwa wazi na baba yake.

Sioyi ni mkwe wa Lowassa na kuna uvumi usiokanushwa kuwa mtandao wa Lowassa ndio uliwezesha Sioyi kupitishwa katika hatua zote.

Wakati naandika makala hii nimeambiwa kuwa, Edward Lowassa ameamua kwenda jimboni Arumeru Mashariki na kuzungukia kata zote 17 kuhakikisha mkwe wake anashinda.

Yasemekana Lowassa anadai kuwa mgombea Sioyi anahujumiwa na wapinzani wake wa ndani ya chama na kwamba wanaomhujumu wanafanya hivyo kwa chuki binafsi waliyonayo kwake kama Lowassa.

Kama hii ni kweli, basi kuna mushkeli katika siasa za ndani ya CCM; lakini zaidi sana ni uthibitisho wa udhaifu wa mgombea Sioyi.

Kumtetea Sioyi kwa sababu tu anachukiwa na makada wa ndani ya CCM, hakumfanyi kuwa mgombea bora wa Arumeru.

Vilevile kumkataa Sioyi kwa sababu tu anaungwa mkono na Lowassa, hakumfanyi awe bora au dhaifu; bali ni kudhihirisha udhaifu wa chama kilichomteua kuwa mgombea licha ya upinzani mkali uliokuwa wazi.

Hatimaye, huu ni mgogoro wa CCM ambayo sasa inasimama mbele ya wananchi wa Meru na kuahidi kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili. Huu ni uongo wa mchana kweupe.

Kosa kubwa wanaloweza kufanya wananchi wa Meru, ni kuchagua Sioyi kwa kuangalia ni nani anamuunga mkono au anampinga.

Kumchagua kwa sababu anaungwa mkono na Lowassa; au kwa sababu ananadiwa na Mwigulu; au basi tu kwa kuwa ameombewa kura za huruma na Wassira; ni kutenda kosa kubwa.

Hawa watu hawatabaki Meru kutataua kero zao. Wapigakura wanapaswa kuangalia kama Sioyi amekomaa kifikra na ana uwezo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

Ni kosa kumchagua Sioyi kwa sababu tu alinadiwa na Mkapa au kwa kuwa anatoka katika chama tawala. Hakuna chama tawala milele; na kimsingi mbunge ni zaidi ya chama anachotoka. Uwezo wa mgombea uwe kigezo cha kwanza katika kuchagulika kwake.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)