Askofu huyu katumwa na nani?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version

ASKOFU wa Kanisa Katoliki anategemewa azungumze mambo ya maadili na imani. Anatarajiwa afundishe mafundisho ya kanisa, yasiyoegemea upande wowote wa kisiasa kwa kuwa yeye ana waumini wa vyama mbalimbali katika kanisa lake analoliongoza.

Katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliomalizika hivi karibuni hali imekuwa tofauti.

Uchaguzi umepita, walioshinda wanafurahia mitaani, walioanguka wanasikitika; yote hayo ni maamuzi ya wananchi na yanapaswa kuheshimiwa.

Katikati ya shangwe, wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki walitumiwa ujumbe kupitia mbunge wao, Tundu Lisu. Ujumbe huo ulitoka kwa mkuu wa mkoa wa Singida na mkuu wa wilaya, unaomtaka mbunge huyo mteule aache kufurahia ushindi kwa nguvu, na kupeperusha bendera huku akipita na vipaza sauti.

Sababu? Eti kwa kufanya hivyo anawaumiza wale walioshindwa. Huku ni kupotosha maana ya mashindano.

Hakuna shida. Tatizo ni kwamba waliotuma ujumbe huo ni viongozi wa serikali, yaani mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya – Singida.

Mbaya zaidi aliyetumwa kuwasilisha ujumbe huo ni kiongozi wa Kanisa Katoliki mkoani humo, yaani askofu. Tunashindwa kuelewa.

Ilikuwaje mkuu wa mkoa, na mkuu wa wilaya wamtume askofu huyo kumwambia mbunge wetu maneno hayo? Hakukuwepo na watu wengine wa kutumwa katika ofisi ya viongozi hao wa serikali ila atumwe kiongozi huyo wa kiroho?

Na kwanini kiongozi huyo wa dini alijishusha sana kiasi cha kutumwa kazi kama hii isiyo na tija kwa kanisa? Na alikubali kuifanya kwa maslahi ya nani? Kwa ajili ya nini?

Askofu ananukuliwa akimwambia Lissu kwamba “kwa kuwa umepata ulichokuwa unatafuta usiwahamasishe wananchi waache kuchangishwa.” Loo!

Mojawapo ya sera zilizomwongezea umaarufu Lissu katika kampeni zake ni kuzuia michango yote haramu, ukiwemo wa sekondari. Hoja ya Lissu ni kwamba mchango huo ni haramu kwa kuwa haukupitishwa kisheria na bunge.

Lisu amekuwa akihoji kuwa pesa nyingi zinazotengwa na serikali hazifiki kwa wananchi kujenga shule, hivyo anataka serikali iwajibike kujenga shule hizo kwa pesa za kodi badala ya kuwatoza wananchi michango ambayo imekuwa ikiwanufaisha wachache.

Lissu amekuwa mkali pia kwa vizuizi vinavyowekwa barabarani kukusanya ushuru wa mazao, kwani upo kinyume. Sheria ya serikali za mitaa liyofuta ushuru wa mazao ilitolewa kupitia tangazo la serikali Na 231, la tarehe 3/5/2002, wakati huo Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi akiwa waziri mwenye dhamana.

Sasa Bunge hadi sasa halijatunga sheria nyingine tofauti na hiyo, hivyo kuonekana kuwa serikali imewaibia Watanzania michango na au ushuru haramu kwa miaka minane.

Hayo ndio madai ya mbunge huyu machachari. Lakini askofu huyu ameenda kumshauri aache kuzungumzia ajenda hizi. Inakuwaje askofu anapokuwa anapenda wananchi wake kutozwa ushuru isivyo halali? Askofu anatumia gari yake inayolipiwa mafuta kwa sadaka za wakristo toka Singida mjini hadi Dung’unyi kwa Tundu Lissu kueleza mawazo mepesi haya.

Njia nzima Roho Mtakatifu hakumshukia askofu huyo amshauri tofauti? Wananchi wa Singida wamekuwa wakisikitishwa na baadhi ya dhuluma zinazoonekana kufanywa na viongozi hao waliomtuma.

Wananchi wamedhulumiwa mashamba katika mradi wa umeme unaotarajiwa kuanza, wananchi wameendelea kunung’unikia kuuzwa kwa majengo ya Chama cha Ushirika mkoani (SIRECU), wananchi wameendelea kushuhudia mikataba tata ya kifisadi katika jengo la utamaduni lililopo mjini Singida.

Wananchi wamekuwa wakitozwa ushuru usio halali mjini Singida, hutozwa fedha kwa ajili ya usafi wakati mji wa Singida ni mchafu. Hayo yote yanahitaji mtetezi.

Askofu anapoamua kumwonya mtetezi wa haki ili kutumikia mafisadi hawa, analenga nini? Anafaidika vipi na uongozi unaolalamikiwa na wananchi? Yeye kama askofu aliumia vipi na kwa nini aliumia na ushindi wa Lissu, hadi aone walioshindwa wanahuzunika?

Je, anakubalina na rushwa iliyotumika kuwanunulia wananchi vitenge, kanga, magodoro fulana na kofia alizokuwa anatoa yule aliyeshindwa? Anamhurumia aliyeshindwa kwa kuwa alitoa fedha nyingi kupita kiasi kuhonga wananchi? Anatufundisha nini sisi waumini wake kwa siku zijazo?

Je, kuwahurumia watoa rushwa walioshindwa huku akiwawaonya walioshinda kihalali waache kushangilia ushindi wao ni msimamo wa kanisa au wake binafsi?

Maaskofu wangapi walifanya kitu kama hicho kwenye majimbo yao? Askofu huyu atatumiwa na mkuu wa mkoa kwa mambo mangapi? Na atatumiwa vile kwa muda gani? Na alipotumwa hakugundua kuwa mkuu wa mkoa anao watu wengi wa kutuma kwa mambo mepesi kama hayo ili amshauri vinginevyo kuliko kujitolea kwenda?

Ziara yake kwenda kuonana na Lissu ililipiwa kiasi gani toka kwa mkuu wa mkoa? Kwa nini hakupewa gari na ofisi ya mkuu wa mkoa akaamua kutumia gari yake inayolipiwa na waamini wa kanisa hilo? Ni kitendo cha aibu, ambacho kama bado kipo kwenye akili za waumini, basi ni cha kuvumilia.

Lakini mkuu wa mkoa wa Singida na askofu huyu wamedhalilisha kanisa kwa kutumia gari ya askofu kufanyia siasa ambazo hazina lengo la kumkomboa maskini wa Kitanzania.

Si vema askofu kuwabeba viongozi wa aina hii, ni aibu katika jamii. Tunamwomba Mungu awajalie busara wasirudie mchezo mchafu kama huu. Na kwa aibu hii ingefaa askofu na mkuu wa mkoa wa Singida na mkuu wa wilaya waombe radhi wakristo kwa Singida kwa kutumia gari la wakristo kwa shughuli zenye manufaa ya kifisadi, yasiyo na tija hata kidogo kwa maendeleo ya Kanisa.

Hofu ya viongozi wa serikali kwa ushindi wa Lissu imekuwa kubwa tangu wakati wa kampeni, ndio maana akiwa Singida, Jakaya Kikwete alinukuliwa akisema; “Heri Dk. Slaa awe rais, kuliko Tundu Lissu kuwa mbunge.”

Pamoja na hayo yote tunawaomba viongozi wa serikali na viongozi wa dini msipingane na sauti za wananchi. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: