Askofu KKKT atishia kumega kanisa


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Askofu Mkuu  wa Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), liko hatarini kupasuka vipande viwili endapo viongozi wake wakuu watashindwa kushughulikia mgogoro kati yake na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela, MwanaHALISI limegundua.

Tayari Askofu Mdegela ametoa waraka unaoashiria kuwa yuko mbioni kuiondoa dayosisi yake ndani ya KKKT kwa kile anachodai, “kufuatwafuatwa” na mkuu wa kanisa hilo Askofu Dk. Alex Malasusa.

Aidha, kuthibitisha kuwa Askofu Mdegela amepania kuiondoa dayosisi yake ndani ya KKKT, katika kipindi cha siku nne amefanya mambo mawili makubwa:

Kwanza,  tarehe 8 Juni 2011 aliitumia Halmashauri Kuu ya dayosisi yake kutoa tamko la kumtetea na kisha kumtuhumu mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Malasusa kwa kusema alichoita “majungu” na kwamba kanisa hilo “halihitaji tume kufanyia kazi majungu.”

Pili, tarehe 12 Juni 2011, Askofu Mdegela aliwaeleza waumini wake mjini Iringa, kwamba “yote aliyofanyiwa yatabebwa na wahusika wenyewe.”

Alisema, “…katika muda huu wa mwezi wa tano, bila shaka wengine kwa sababu mpo hapa mjini mmesikia kwamba walikuja maaskofu watatu kunichunguza. Walifanya kazi hiyo siku moja, siku ya pili niliwafukuza kwa mujibu wa katiba na taratibu za kanisa. Sitoi maelezo ya kwa nini niliwafukuza; maelezo ni kwamba walikwenda kinyume cha taratibu.”

Alisema, “Mimi mchungaji, Daktari, Owdenburg Moses Mdegela, siyo daktari wa mifugo wala wa watu: Ni daktari wa falsafa, ni askofu wa KKKT dayosisi ya Iringa kwa mujibu na utaratibu na katiba yake kama nilivyochaguliwa tarehe 8/10/1986 nikaanza kazi rasmi tarehe 01/01/1987.

“Nikawekwa wakfu baada ya chakula cha Meza ya Bwana hapa kanisani tarehe 27/09/1987, pale kwenye uwanja wa Samora; bado ni Askofu wa dayosisi ya Iringa bila tashwishi wala kizuizi cha mamlaka halali iliyonichagua na kuniruhusu niwekwe wakfu yaani – mkutano mkuu wa dayosisi ya Iringa,” alitamba.

Alisema, “…wale walioandika kwenye magazeti na kwenye barua pepe; na wote waliofanya chochote walichofanya, walifanya mambo yao, hawakufanya mambo ya dayosisi ya Iringa… hivyo gharama za mambo waliyoyafanya zinawahusu wao na watazibeba wao; matusi waliyotukana yanawahusu wao na watayabeba wao.”

Tamko la Halmashauri Kuu ya Iringa linamtaka Askofu Malasusa kuwataja wachungaji watano wa dayosisi hiyo wanaodaiwa kuwa ndiyo waliowasilisha malalamiko kwake dhidi ya Askofu Mdegela, vinginevyo wachungaji wa dayosisi hiyo watalazimika kuamini kuwa taarifa zote zilizotolewa ni uchochezi unaolenga kuwasababishia wachungaji hao kutowaamini viongozi wao wa juu.

“Haya mambo yakomeshwe mara moja. Tunataka mamlaka ya dayosisi ya Iringa yaheshimiwe na gharama zilizotumika katika kuunda tume ya uchunguzi zirejeshwe ili fedha hizo zitumike kwa kazi ya kueneza injili na malengo ya kazi za umoja za kanisa,” inasema sehemu ya taarifa inayodaiwa kutolewa na Halmashauri Kuu ya KKKT, dayosisi ya Iringa.

Askofu Mdegela anatuhumiwa ubadhilifu wa fedha za kanisa, kupoteza maadili na kashfa za ngono.

Gazeti hili lilipoongea na Askofu Mdegela mapema mwezi uliopita, alidai habari hizo ni “maji machafu ya chooni.”

Tangu MwanaHALISI lichapishe tuhuma hizo mwezi mmoja uliopita, Askofu Mdegela amekuwa akitoa matamko ya maandishi mbalimbali.

Katika moja ya barua pepe inayosadikiwa kuandikwa naye, Askofu Mdegela anadaiwa kumjulisha askofu mwingine wa KKKT (jina tunalo), mbinu mbalimbali anazopanga kutumia ili kujinusuru na tuhuma dhidi yake. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuiondoa dayosisi yake katika KKKT.

Lakini Askofu Mdegela amekana kuandika barua pepe hiyo, badala yake anasema anuani hiyo imeingiliwa na wabaya wake na kuitumia kuandika ujumbe unaotajwa kupelekwa kwa askofu huyo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umeonyesha bado Askofu Mdegela anatumia anuani hiyo hata baada ya kudai imeingiliwa na maadui wake.

Katibu Muhtasi wa askofu aliyetumiwa barua pepe hiyo na Askofu Mdegela, amekiri kuwa ilitoka kwa Askofu Mdegela na kuwa alipiga simu kuhakikisha kama imefika na kusisitiza kuwa skofu wake aipate.

Taarifa, katika barua pepe, zinawataja wanawake wawili waliodai kuwa wazazi wenzake (umewaona? umewahoji? Wako wapi?) na Askofu Mdegela ambao wamelalamika kuwa amewatelekeza muda mrefu bila kupeleka matumizi ya watoto wake.

Walipohojiwa iwapo wanajua kuwa ni hatari kumsingizia “mtumishi wa Mungu,” walidai ushahidi uko wazi, na kudai kuwa sehemu ya ushahidi ni mke wa askofu ambaye amekuwa akiwabembeleza kuwa wamkabidhi watoto awalee mwenyewe kuliko kutegemea askofu aendelee kuwapatia fedha.

Katika moja ya matamko na hotuba zake wiki iliyopita, Askofu Mdegela anamlaani mwandishi wa habari wa gazeti hili, Alfred Lucas pamoja na Mhariri Mtendaji, Saed Kubenea kwa kile alichodai wamemsingizia mambo mengi. Hakutaja aliyosingiziwa.

Kuhusu hatima ya uchunguzi ulioagizwa na kanisa juu mwenendo wake, Askofu Mdegela alidai ugomvi uliopo ni sawa na ule wa kati ya mke na mume.

Alidai kwa mila na desturi za Kiafrika, ugomvi wa mama na baba huwezi kuupeleka kwa watoto.

Taarifa kutoka ndani ya kanisa hilo zinasema, Askofu Mdeghela aligeuka mbogo pale baadhi ya waumini walipomuliza baada ya ibada yeye ni nani katika mgogoro huu – baba au mama?

Haraka alijibu, “Mimi baba, ndiyo maana nimewafukuza wakatili.”

Kanisa la KKKT lina dayosisi 20 nchi nzima na endapo Askofu Mdegela atafanikiwa kuizuia KKKT isishughulikie mgogoro wa Iringa, kuna hatari kuwa waumini wa dayosisi hiyo wakabaki kama mateka katika mikono ya kiongozi mmoja.

Katika moja ya hotuba zake hivi karibuni, Askofu Mdegela amenukuliwa akieleza jinsi asivyowaamini hata wasaidizi wake wa karibu, hali inayoashiria kuwapo kwa mnyukano mkubwa ndani ya dayosisi yake.

0
No votes yet