Askofu KKKT katika tuhuma nzito


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version
Maaskofu KKKT

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, limetumbukia katika mgogoro mzito na wa aina yake ambao, iwapo busara haitatumika utaweza kuliacha kanisa limekatika vipande viwili, imefahamika.

Habari hizo ambazo zimetapakaa na hata kuifikia ikulu ya Rais Jakaya Kikwete, vyombo vya habari, polisi na idara ya usalama wa taifa, zinamtuhumu mkuu wa kanisa hilo, Askofu Owdenberg Mdegella kwa ufisadi.

Bali alipoulizwa na MwanaHALISI juzi Jumatatu juu ya tuhuma hizo, Askofu Mdegella alisema, “Hayo madai ni maji machafu.

“Ndugu mwandishi usikubali kuandika maji machafu ya chooni kwenye gazeti lako. Hao wanaosambaza habari hizi ni wahuni…Kama wana madai ya kweli si wajitokeze kwenye halmashauri?”

Alisema, “Hakuna kingine kinachofanya wanichafue zaidi ya kulilia madaraka. Watu wanataka cheo. Mimi nasema hawawezi kuning’oa hapa.”

Madai dhidi ya askofu yameorodheshwa katika andishi lenye maneno 2008 lililopelekwa kwa maaskofu wote wa KKKT, ikulu, taasisi (mbalimbali) na vyombo vya habari. Lilisambazwa kwa njia ya baruapepe.

Askofu Mdegella anatuhumiwa makosa ya jumlajumla tu yakiwemo ufuska, ufisadi wa mali za kanisa na ushirikina.

Tayari baraza la maaskofu wa KKKT, limeunda tume inayoongozwa na Askofu Dk. Hance Mwakabana wa Dayosisi ya Kusini-Kati (Makete) kuchunguza tuhuma zinazolichafua kanisa hilo na Askofu Mdegella mwenyewe.

Wajumbe wengine wa tume hiyo, ni Askofu Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini (Moshi) na Askofu Elisa Buberwa wa Dayosisi ya Kaskazini - Magharibi (Bukoba).

Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Askofu Mdegela, ni kufisidi fedha za dayosisi yake na zile za chuo kikuu cha Tumaini, Iringa; kushinikiza kulipwa mishahara miwili – ule wa dayosisi na mwingine wa chuo kikuu; pamoja na malipo ya safari za binafsi ndani na nje ya nchi.

Tuhuma nyingine ni kwamba askofu anataka ofisi yake ilipe mikopo yake binafsi katika baadhi ya mabenki nchini; igharimie matumizi ya familia yake zikiwamo karo za watoto wake na jamaa zake wengine.

Askofu anatuhumiwa pia kushinikiza vyombo vingine vya kanisa hilo ambamo yeye ni mjumbe wa bodi au mwenyekiti, kama vile shirika la wakimbizi la kanisa hilo (TCRS), kugharamia masuala yake binafsi.

Hata hivyo, tume ya maaskofu iliyoundwa ilipofika Iringa wiki iliyopita, inadaiwa ilifukuzwa na Askofu Mdegella huku akiwatishia kuwa wakiendelea kumchunguza yatawapata makubwa ambayo hawatakaa wayasahau.

Huku akijiapiza, pamoja na baadhi ya wachungaji, Askofu Mdegella anaripotiwa kuwaambia wachungaji hao, “Niko tayari kuiondoa dayosisi yangu katika KKKT ili isiwe inaingiliwa na KKKT ambayo haina kiongozi mwenye uwezo wa kuninyoshea kidole.”

Habari zinasema mzozo wa matumizi mabaya ya madaraka anaotuhumiwa Askofu Mdegella tayari umetinga kwa marafiki wakubwa wa dayosisi hiyo walio Ulaya na Marekani na wameweka msimamo wa kutaka kufahamu jinsi fedha wanazotoa zinavyotumika.

“Hata wafadhili wetu wameanza kulalamikia matumizi mabaya ya fedha za miradi ya dayosisi. Kanisa limevumilia mambo haya kwa muda mrefu, sasa ndiyo maana unaona kuna hatari ya kutokea mpasuko,” ameeleza mmoja wa viongozi wa kanisa hilo.

“Pamoja na tabia hizi za Askofu Mdegella kuwa za muda mrefu, kanisa limeendelea kuzinyamazia na kila mmoja anaona zimevuka mipaka,” ameeleza mtoa taarifa.

Aidha, Mdegella amekana kumbaka mwanafunzi wa chuo kikuu cha Tumaini Iringa, ambaye ametajwa kuwa mtoto wa askofu mmoja wa kanisa hilo.

Aliliambia gazeti hili, “Hivi kwa nafasi yangu hapa chuoni (mwenyekiti wa bodi) na nafasi yangu ya kiroho, wewe unaamini mimi naweza kufanya hilo?”

“Hayo ni madai niliyofananisha na maji ya chooni. Achana nayo,” alisema Mdegella kwa sauti ya utulivu.

Mdegella anatuhumiwa pia kushindwa kutunza nidhamu ya watumishi wa dayosisi hiyo na hata wachungaji kutokana na tabia inayodaiwa kuwa sugu ya kuendekeza matendo “kinyume cha maadili ya kanisa,” ameeleza mtoa taarifa. 

Alipoelezwa tayari malalamiko hayo yamefika ndani ya kanisa lake na ndiyo msingi wa kuundwa kwa tume kumchunguza, Askofu Mdegella, kwa sauti ya hasira alijibu, “Nakwambia… hakuna wa kuning’oa.”

Askofu Mdegella aliyeendelea kukana tuhuma, na madai mengine kuwa hayapo, alikiri kuwafukuza ofisini kwake wajumbe wa tume iliyoundwa kumchunguza.

Alipoulizwa kwa nini asiruhusu tume kuchunguza ili ukweli kubainika, Askofu Mdegella alisisitiza, “Nimekwambia huo ni uwongo unaofanana na maji machafu ya chooni.”

Alisema, “Mimi ni askofu wa maisha. Kwanza ninastaafu 2015 na baada ya hapo nitabaki hapa; lakini naomba uwape salamu kwamba nitawafanyizia.”

Alipoombwa kufafanua maana ya “kufanyizia,” Askofu Mdegella alisema, “Wewe ngoja tu. Unajua kuna uchaguzi mwaka huu na watu wanahangaika tu…”

Alilitishia kushitaki gazeti hili iwapo litaandika habari hizo. Alisema, “Nitawashitaki. Nitakodi mawakili kutoka hata Marekani kuja kusimamia kesi hii. Haya mambo hayana ukweli na hata hiyo tume ilipokuja hapa niliwaondoa maana hakuna maji machafu ya chooni hapa.”

Gazeti hili lilimwita mkuu wa kanisa hilo, Askofu Mkuu Dk. Alex Malasusa. Simu yake ilipokelewa na aliyejitamnbulisha kuwa ni karani wake.

Karani alipoulizwa alipo askofu ili atoe ufafanuzi wa sakata la Askofu Mdegella, alijibu kwa ufupi tu, “Askofu hawezi kuzungumzia mambo hayo kwenye simu.”

Alimtaka mwandishi kufika ofisini kwake, jengo la Luther House, gorofa ya pili. “Njoo na barua na uweke ahadi ya kuzungumzia jambo hilo. Huu ndio utaratibu wa kanisa,”  alisema na kisha kukata simu.

Wakati hayo yakitokea, askofu mmoja wa kanisa hilo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, amedai kuwa tuhuma zinazomkabili Mdegella ni za kweli na kanisa “litazichunguza kwa njia yeyote ile.”

“Nakwambia ndugu yangu, katika dayosisi ile, wachungaji wengi na watumishi wanaishi maisha ya ovyo mno huku wakiwa na vimada na wengine kuzaa nje ya ndoa,” ameeleza askofu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Inadaiwa hivi sasa Askofu Mdegella amewekewa kitanda katika chumba maalum karibu na ofisi yake kwa “kupumzikia pale anapochoka.”

Miongoni mwa tuhuma dhidi ya Mdegella ni kuwepo akina mama wengi wenye mahusiano naye ambao wamekuwa wakidai matunzo. Inadaiwa baadhi ya akina mama hao wameonana na wakuu wa kanisa la KKKT na kuwasilisha malalamiko yao.

Tuhuma nyingine inayomwandama Mdegella ni kulipwa mishahara miwili; yaani wa Dayosisi na Chuo Kikuu.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)