Au Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
SMZ, dawa ya deni kulipa tu

MOJA ya hatua muhimu ambazo rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alizichukua baada ya kuingia madaraka, ni kule kutunga sheria inayosimamia ununuzi wa huduma au bidhaa.

Ilikuwa hatua muhimu kwa sababu, kwa muda mrefu eneo hilo lilikuwa likitumiwa kunufaisha baadhi ya maofisa wa serikali na washirika wao walioko nje ya serikali.

Sheria ile ya mwaka 2003, ikiwa ni moja ya sheria za kwanza kutungwa na serikali ya rais Karume, ilijenga msingi mzuri na mpya wa utaratibu wa kisheria unaoiwezesha serikali kupata huduma na bidhaa kutoka nje.

Rais alichukua hatua hiyo kwa kukerwa na mfumo mbaya uliokuwepo ambao kwa sehemu kubwa uliwapa maofisa wa serikali ulaji kwa kutumia mgongo wa serikali.

Aliona hasara na gharama ambazo serikali ilikuwa inaingizwa kila inapopata huduma au bidhaa kutokana na uzoefu wa kutosha alioupata kwani alishakuwa ofisa mwandamizi wa muda mrefu akianzia na ukurugenzi katika wizara.

Baada ya kuingia ikulu, alijionea vituko zaidi kutokana na taarifa za wasaidizi wake. Aliona mabadiliko madogo. Kubwa ni serikali kuendelea kugharamika.

Lipo tatizo – labda kutokana na utamaduni ulioota mizizi miongoni mwa maofisa wengi wa serikali wa kutojali mali ya umma, ikiwa ni pamoja fedha za serikali ambazo ni fedha za wananchi – uzembe na ubabe kutawala shughuli za umma.

Kwa kutaka kuziba nyufa katika sheria hiyo, kwa bahati mbaya sana, rais amekuja na sheria mbaya. Inaelekeza dharau juu ya utawala bora; unaofuata sheria na kanuni zilizo wazi kulingana na wakati tulionao.  

Sasa, kupitia baraza lake la mawaziri, Rais Karume amekuja na sheria mpya – na wala siyo ya kurekebisha matumizi mabaya ya sheria aliyoasisi tangu wakati akihubutubia wananchi kwenye kampeni za uchaguzi. 

Serikali inataka kuzuia mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa mali zake pale kampuni au mtu binafsi anaposhinda kesi dhidi ya serikali na kuamuliwa kupitia hukumu kuwa alipwe fidia au deni kwa kuwa aliiuzia bidhaa au huduma serikali. 

Tayari sheria hiyo imepitishwa na Baraza la Wawakilishi, kinachosubiriwa ni rais kuitia saini ili kuanza kutumika. 

Nini serikali inataka katika sheria mpya? Inataka kuwajibisha maofisa wote wa serikali na wanasheria watakaosababisha hasara au gharama kwa serikali inaposhitakiwa mahakamani na kudaiwa deni au fidia.

Serikali inasema msingi wa kutunga sheria hiyo ni kulinda mali za serikali dhidi ya uwezekano wa kukamatwa na kupigwa mnada ikitokea imeshindwa kesi ya madai mahakamani na kutakiwa kulipa deni.

Kwamba kwa maofisa wa serikali, wakiwemo wanasheria wa serikali na mawakili wa kujitegemea, watakaobainika kufanya uzembe katika kuitetea serikali na ikatokea kushindwa kesi, basi waadhibiwe wao kulipa fidia au deni linalodaiwa serikali.

Maana yake pia mahakama haitaweza kukazia hukumu iliyoitoa dhidi ya serikali, ambayo itakuwa inaelekeza kutolewa amri ya mahakama ya kukamata mali za serikali ili kumlipa mdai aliyeshinda kesi.

Na ofisa huyo akishawajibika kwa hasara au gharama aliyoisababishia serikali kutokana na kile kinachoitwa uzembe wa kutowajibika ipasavyo wakati akisimamia kesi, ataifidia serikali kwa hasara au gharama hiyo.

Sheria hiyo pia inaelekeza katika kumwajibisha ofisa wa idara maalum ya serikali, kulazimika kulipa gharama kwa madhara aliyosababisha katika utendaji wake wa kazi za serikali, iwapo utendaji wake huo ulimuumiza mtu mwingine ambaye ameishitaki serikali na kushinda kesi.

Hapa kusudio hasa ni kuzuia uwezekano wa serikali kushitakiwa na kudaiwa fidia kutokana na madhara aliyosababishiwa mtumishi wake kutokana na utendaji mbaya wa ofisa wa idara fulani ya serikali. Madhara hayo yaweza kuwa ni pamoja na kifo.  

Nasema sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imetangaza rasmi upinzani dhidi ya dhana ya utawala bora na utawala unaofuata sheria na kanuni.

Imetunga sheria ambayo utekelezaji wake ukifanywa sawasawa, itakuwa na maana kwamba mahakama haitakuwa tena chombo kinachotegemewa katika utoaji wa haki kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kuitazama sheria hiyo, harakaharaka mtu makini unapata taswira kwamba serikali iko juu ya sheria na haijali kamwe mantiki ya mgawanyo wa madaraka. Kwa ufupi, haijali mihimili mingine miwili ya dola: mahakama na baraza la wawakilishi.

Najua serikali ina nia njema ya kuzuia matumizi mabaya ya madaraka kwa maofisa wake, lakini njia iliyoamua kuitumia ni mbaya isiyostahili kwa wakati huu.

Ni kama vile kusema kwamba sasa serikali inataka kunyonga mtu anayeidai asiishitaki mahakamani. Kwamba iwapo serikali imepewa huduma au imenunua bidhaa kwa njia ya mkataba wa kupata bidhaa ndipo ilipe, na ikatokea imeshindwa kulipa kimkataba, basi mtoa huduma adai kwa kuzungukazunguka tu ofisi na siyo kushitaki mahakamani.  

Hii haiwezekani wakati huu. Nassor Ahmed Mazrui, mjumbe mpya wa baraza la wawakilishi aliyeteuliwa na rais, anasema:

Sasa wafanyabiashara wa ndani na nje wataogopa kuikopesha serikali. Hata hakimu akishatoa hukumu hataweza kuisimamia itekelezwe kwa vile waziri amepewa mamlaka makubwa (na sheria hiyo) ya kuipinga au kuibadilisha hukumu.

Sahihi. Haitakuwa kitendo kizuri na kinachokwenda na mantiki ya utawala wa sheria na uzingatiaji wa dhana nzuri ya ujenzi wa uchumi wa nchi unaojali ushirika kati ya sekta ya umma na binafsi. 

Badala ya serikali kutunga sheria ya kuzuia mahakama kufanya kazi yake kuu, ya utoaji wa haki, ilichotakiwa ni kudhibiti maofisa wake kwa kujenga nidhamu ya utumishi iliyotukuka.

Kuja na sheria inayozuia mtoa huduma au bidhaa kwa serikali kulipwa haki yake baada ya serikali kugoma bila ya uhalali wa kisheria, ni kinyume na msingi mkuu wa haki za binadamu.

Dawa ya deni ni kulipa. Kama serikali imepokea huduma lazima ilipe; na ilipe kwa mujibu wa makubaliano. Kukataa kulipa ni wizi na Karume ni muumini mzuri wa dini anajua kwamba kuiba ni dhambi.

mwisho

Ushetani ni kwamba unataka kufanya biashara lakini wewe hutaki kugharamia. Ukishitakiwa unatisha mahakama kutumika kukubana ulipe. Huu ni ushetani.

  Machungu ambayo serikali inayapata sasa ya kudaiwa mabilioni ya shilingi na watu binafsi au na watumishi wake kutokana na kuumizwa na serikali, ni matokeo ya kiburi cha viongozi.

Kwa mfano, wengi wao wanadharau amri za mahakama; wanakataa kuishauri vizuri serikali inapopatwa na tatizo la kisheria; wanaingiza siasa katika masuala ya uongozi; wanatoa amri za kihuni dhidi ya watumishi wengine na wananchi walio nje ya utumishi wa umma. Kutenda ovyo kote huko, bado serikali haiwadhibiti maofisa wake waovu.

Hakuna namna. Dawa ya deni ni kulipa tu.

0
No votes yet