Awamu nne, vioja vinne


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version

NILISOMA hivi karibuni habari kuwa mfanyabiashara maarufu nchini Yusuf Manji ameifungulia mashitaka kampuni ya Kagoda kwa kushindwa kumlipa deni lake. Inaelekea mkubwa fulani wa Kagoda alikwenda kukopa kwa Manji.

Wiki mbili baadaye nikasoma kwamba eti Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewaomba wananchi wenye ushahidi kuhusu ufisadi wa kampuni ya Kagoda wampelekee ili aweze kukamilisha upelelezi na hatimaye kuwafungulia mashtaka walioiba fedha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia akaunti ya EPA!

Nikakumbuka pia vituko vingine vinavyofanyika katika enzi hizi za kujivua na kuvuana magamba katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo waziri aliyetuhumiwa kumiliki vijisenti kutokana na rushwa ya rada badala ya kuwajibishwa, akafanywa mkuu wa idara ya maadili ya chama cghake!

Mambo haya na mengine yanayofanyika nchini sasa, yamenifanya kuangalia historia ya utendaji serikalini katika awamu zote za utawala wa nchi tangu enzi za Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa hadi ya Jakaya Kikwete. Katika uchunguzi wangu nimegundua vioja vinne.

Awamu ya kwanza ya Nyerere(1961 – 1985):

Hii ni awamu iliyojitahidi kufanya kila linalowezekana kwa manufaa ya nchi licha ya matatizo ya ugeni wao kiutawala baada ya kupata uhuru.

Walifanya makosa mengi kama vile kufuta vyama vya ushirika na halmashauri za wilaya, miji na jiji. Hata hivyo, walipogundua makosa yao waliomba radhi na kuzirejesha.

Hii ilikuwa awamu ya wajenzi wa taifa. Walijenga viwanda kama vile Kiwanda cha Kilimo Mbeya (ZZK); kiwanda cha mbolea Tanga, kiwanda cha vifaa vya kilimo Ubungo (UFI);viwanda vya nguo – Kiltex, Sunguratex, Mwatex, Mbeyatex, Tabotex; viwanda vya mabati, mablanketi, chuma, matairi, viatu (Bora) na vingi vinginevyo.

Waliunda mashirika ya umma kama shirika la usagishaji la taifa (NMC), shirika la nguo nchini (Natex), shirika la kuku (Napoco), Shirika la Elimu Kibaha, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Ndege (ATC), Shirika la Madini (Stamico), Shirika la Meli (Tacoshili) na Shirika la Uvuvi (Tafico).

Walianzisha pia makampuni ya taifa kama vile kampuni ya ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO).

Mwalimu Nyerere alipoondoka madarakani, watawala waliomfuata wamejitahidi sana kuuza na kugawa hovyo mashirika, makampuni na viwanda alivyojenga hadi leo wanaendelea kuuza na kugawa.

Rais Mwinyi aliuza sana na hadi anaondoka kulikuwa na viwanda, mashirika na makampuni yaliyosalia. Akaingia Mkapa ambaye alifanya rafu—hakuuza kwa staha kama mtangulizi, hata hivyo hakuyamaliza.

Halafu akaingia madarakani Rais Kikwete ambaye alimalizia kuuza mashirika, makampuni na viwanda vilivyojengwa enzi ya awamu ya kwanza. Ameuza hata mashamba ya umma ya Mbarali na Kapunga yaliyoko wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Awamu ya pili ya Mzee Ruksa(1985 – 1995):

Hii ni awamu ambayo mambo yote yalikuwa holela na kila kitu ruksa. Huu ndio wakati tuliposhuhudia kwa mara ya kwanza mgawanyiko baina ya Waislamu na Wakristo.

Mabucha ya nguruwe Manzese yakavunjwa na mihadhara ikatamalaki nchi nzima. Kwa mara ya kwanza watu tukalazimishwa kusema sisi ni dini gani!

Sisi “wapagani” tukakaa kimya na mpaka sasa wenye dini wanadhani hatupo. Na wale wanaokubali tupo hawatuamini, tunaambiwa sisi ni “Wagalatia,” na kwamba tulifaidi wakati wa Nyerere.

Uholela haukuishia katika kuzagaa mihadhara pekee bali pia kwenye biashara ambapo hakukuwa na udhibiti tena. Wenye fedha kwa mara ya kwanza wakaanza kuneemeka na kuabudiwa.

Huu ndio wakati walipoanza kufahamika watemi wa fedha wanaotambulika kama mafisadi sasa.

Ikafikia wakati wenye majina wakagawana hata mahindi ikulu. Ndipo kukazuka mtindo wa kutoa fedha nyingi za mchango au kununua zawadi kwenye minada bila hofu ya kuulizwa kama watoaji wamelipa kodi.

Muasia mmoja alinunua kidani kwa Sh. 2milioni katika mnada wa hadhara kuchangia shughuli nisiyoikumbuka.

“Tatoa milioni bili hiyo dani shemeji avae”! Shemeji kwake yeye ni mke wa rais ambaye alikuwapo kwenye hadhara ile!

Awamu ya tatu ya Mkapa (1995 – 2005):

Mkapa aliingia akiitwa ‘Mr Clean’ lakini alitoka akiwa amechafuka. Hii ni awamu walioingia madarakani na Mkapa; mmoja mmoja au kwa umoja wao walichukia kitu kinachoitwa mali ya umma.

Hii ndiyo awamu iliyoshangaza ulimwengu kwa kufanya mambo kana kwamba mwisho wa dunia ulikaribia. Hii ndiyo awamu iliyokuwa na viongozi wasiojua maana ya maneno kama kuwajibika, uzalendo, maslahi ya taifa na rasilimali za taifa.

Waliona bora na muhimu chochote chenye thamani kimilikiwe na mgeni au wageni kwa maana ya watu wasiokuwa weusi na wasiozungumza Kiswahili!

Bei waliyokuwa wanauzia ilikuwa ndogo kuliko hata bei ya soko ya kiwanja kilipo kiwanda. Kwa hiyo, awamu ya tatu ya ‘njomba Nkapa’ iligawa hovyo mabenki, viwanda na mashirika ya umma.

Mkapa pia aligawa mashamba ya umma na akagawa pia ranchi za taifa. Awamu hii iligawa kila kilichoweza kuuzika au kutolewa bure kwa wageni. Vioja vingi vinavyompeleka puta Kikwete vilianzishwa na njomba.

Hii ndiyo awamu ambapo waziri wa ujenzi alipewa fursa kugawa na kujigawia nyumba za serikali huku akitangaza kuwa anawauzia watumishi wa serikali.

Wenye kujua mambo wanasema kuwa waliopewa ni pamoja na wakubwa wenye magamba katika CCM.

Huu ndio ulikuwa wakati wa kashfa maarufu za EPA na Kagoda yake, Meremeta, ndege ya serikali, kashfa ya rada na hata kashfa ya kampuni maarufu ya Deep Green na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao Mkapa alijipa. Hii ilikuwa awamu ya uhujumu uchumi.

Awamu ya nne ya Kikwete(2005 – 2015):

Hii ni awamu ya wasanii – wanaahidi hili, wanafanya kile na wanaleta lingine kabisa. Kwa mara ya kwanza tukasikia neno “kuchakuchua” na habari za wizi wa kura zikaibuka bila kificho.

Hii ni awamu ambayo Tanzania kama taifa imepoteza dira na inaonekana dhahiri shahiri kuwa hakuna kiongozi wa kitaifa kwa sasa anayeaminika hata chembe.

Hii ndiyo awamu iliyoshindwa kutumia madaraka iliyonayo kikatiba. Leo wezi wanatajwa, lakini kesho tunaambiwa hawakamatiki kwa vile hakuna ushahidi.

Siku mbili baadaye tunaambiwa chama tawala kinajivua magamba na kuwatimua mafisadi! Tunajiuliza mafisadi ndani ya CCM na serikalini wametoka wapi wakati jana tu tuliambiwa hakuna ushahidi wa mafisadi na wezi na wabadhirifu serikalini bali ni kuchafuliana majina?

Hii ni awamu ya inteligensia ya polisi yenye uwezo wa kubashiri yatakayotokea kesho, lakini haiwezi kujua wamiliki wa Kagoda, Deep Green na Meremeta. Awamu hii ni ya wasanii; wanafanya mambo na kuamua kisanii.

0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)