Baada ya Gongolamboto, wapi?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto

MAZINGIRA ya milipuko ya mabomu, Jumatano iliyopita, katika kambi ya Jeshi la Wananchi (JW), Gongolamboto, jijini Dar es Salaam, hayajaandikwa kwa kuwa hayajachunguzwa. Bado ni papasapapasa.

Kuandika habari hizi kunahitaji juhudi binafsi na ujasiri wa kitaaluma. Makala hii ni kwa wanaoandika na wanaopenda habari za uchunguzi.

Haitoshi kuuliza kwa nini kumekuwa na milipuko ya mabomu katika kambi ya jeshi wakati watawala walikwishaahidi haitatokea tena baada ya ile ya Mbagala miaka miwili iliyopita.

Haitoshi kuuliza serikali inachukua hatua gani hivi sasa kuzika wafu, kutibu walioumia, kuhifadhi wasio na makazi, kulisha wasio na chakula na kufidia wanaostahili. Haitoshi.

Mwandishi atalazimika kusikiliza kila chanzo chenye taarifa, ndani na nje ya jeshi na katika hili hakuna visingizio kuwa anaandika “siri za vyombo vya ulinzi.”

Siri za jeshi ni mbinu zao za vita, basi.

Kutoandika kwa kina kutafanya mambo mengi yafichike, hata yale ambayo yangesaidia taifa, serikali, jeshi na raia mmojammoja.

Hivyo, kwa wanaojali, maswali yatakuwa mengi. Yafuatayo yaweza kutoa mwanga juu ya kilicholeta maafa Gongolamboto.

Tuanzie hapa. Mabomu yamelipuka katika kambi ya jeshi. Je, mabomu ni nini? Kila kinacholipuka ni bomu? Kuna aina ngapi za mabomu katika maghala ya Tanzania? Ni mabomu ya aina gani yaliyolipuka Gongolamboto?

Kwa nini mabomu ya aina hii yamelipuka na mengine hayakulipuka? Yaliyolipuka yana umri gani? Umri wa “kuishi salama” wa aina ya mabomu yaliyolipuka ni miaka mingapi? Umri wa mabomu mengine yaliyoko nchini ni miaka mingapi?

Kwa faida ya wasomaji magazeti, wasikilizaji redio na watazamaji televisheni, mwandishi aweza kupata aina za mabomu duniani, picha zake na kueleza tabia zake; akikamilisha kwa uchambuzi na maelezo juu ya tabia ya mabomu ya Gongolamboto – yaliyolipuka na ambayo yanatishia kulipuka.

Mwandishi aweza pia kutafiti nguvu ya kila aina ya mabomu; uzito wake, uwezo wake wa kwenda mbali; kishindo chake, uwezo wake wa kufanya uharibifu na madhara yatokanayo na vumbi na moshi pale mabomu ya aina hizo yanapotua au yanapolipuka.

Kwa hatua hii, bado mwandishi yuko salama. Anajihusisha na elimu juu ya mabomu.

Kwa mfano, kuna usemi kwamba ukiona mwanga au kusikia mpasuko wa radi, ujue uko salama; hujapigwa – hujafa.

Hali ikoje kwa upande wa milipuko ya mabomu? Lini mwananchi yuko salama? Achukue hatua zipi wakati wa “mvua” ya mabomu?

Kawaida mabomu hupashwa joto na kulipuliwa na anayetaka kuyalipua. Nani alipasha joto au aliwasha mabomu haya ya Gongolamboto? Je, yaweza kupata joto yenyewe kwa yenyewe? Kwa kugusana? Vipi? Wakati gani?

Kama mgusano waweza kuleta msuguano na hatimaye joto na milipuko je, hakuna njia za kuzuia misuguano?

Hakuna njia za kuzuia milipuko kwa kufyonza nguvu za joto zilizojitokeza kwa njia ya msuguano?

Hivi ni kweli wataalam wa silaha na hasa mabomu jeshini hawajui mitego, mithili ya ile ya radi ambayo hutumika kufyonza nguvu za mvutano katika maghala ya mabomu?

kuu ni hili: Mitego hiyo ipo katika kila kambi ya kijeshi yanakohifadhiwa mabomu?

Kama mitego hiyo ipo, mbona haitumiki? Imechoka? Haibadilishiki? Utaalam huo umepitwa na wakati? Teknolojia mpya inasemaje kuhusu ulinzi wa silaha nyeti kama mabomu?

Wapiganaji wanasemaje juu ya mabomu na jinsi ya kuyahifadhi? Waliishaomba fedha za kununulia vikinga milipuko wakanyimwa?

Kama walinyimwa walichukua hatua gani? Kama walipewa, viko wapi sasa?

Kuna madai kuwa baadhi ya mabomu yamezeeka.

Si yakizeeka yanakufa? Mbona bado yana kiherehere? Hivi hayawezi kuteguliwa na kutupwa? Hivi bado yanahitajika yote kama yalivyo?

Kwa maswali yote haya, waandishi wachunguzi watafute nani wa kuyajibu – ndani ya jeshi, serikali, wataalam binafsi nje ya taasisi za kijeshi, mashirika na makampuni yatengenezayo silaha, kwenye intaneti na kokote ambako wanaweza kupata taarifa.

Ni elimu tu. Bali sasa tugeukie Gongolamboto. Hivi nani, ndani ya kambi alikuwa anafanya nini, hadi mabomu yakalipuka? Nani alitekenya mabomu hadi yakaanza kulipuka?

Nani alikuwa anajua kuwa mabomu yatalipuka? Alijuaje? Alichukua hatua gani? Alifahamisha utawala? Kama hakuufahamisha, kwa nini?

Hivi milipuko ilianza alasiri ya Jumatano kama ambavyo baadhi ya wananchi wanadai au ni pale kuelekea saa mbili usiku ilipotoka kwa kishindo kikubwa?

Kuna kila sababu ya kusikiliza kila mmoja anayeweza kutoa taarifa, hata maoni, ili viweze kufuatiliwa kwa kina na kupata majibu sahihi.

Kwa mfano, ni kweli kuwa mabomu mengi yaliyoko Gongolamboto yamechoka na yanastahili kulipuliwa kitaalamu?

Je, ni kweli kuwa kuna mabomu makubwa zaidi ya yaliyolipuka ambayo inadaiwa yakilipuka yaweza kuteketeza jiji zima la Dar es Salaam? Yanaitwaje? Ni ya kutoka wapi? Yanatumika lini? Bado yanahitajika?

Hivi ni kweli kwamba hata jeshi au serikali ikitaka kutegua mabomu ya aina hiyo sharti iajiri wataalam kutoka nchi za nje kwa kuwa nchini hakuna wenye uwezo wa kutegua mabomu hayo makubwa, mazito na hatari zaidi?

Sikiliza wasemavyo baadhi ya wananchi na chunguza: Kwamba baadhi ya nyumba za raia karibu na kambi zilikuwa zimefungwa muda mrefu kabla ya milipuko.

Je, kuna aliyewapelekea taarifa kuwa wasiwepo wakati wa milipuko? Hakuna taarifa za baadhi ya askari kufariki. Je, wapiganaji hawakuwa kambini? Walikuwa wapi?

Mzazi mmoja amedaiwa kunukuliwa akisema mtoto wake aliambiwa kuwa “kesho wasiende shule, kuna hatari.”

Kuna ukweli gani katika kauli hii? Wazazi wa watoto wa wanasemaje? Watoto wenyewe wanasema nini? Kama kweli hawakwenda shule, mkuu wa shule anasema nini?

Rafiki yangu kaniandikia sms: “Kama dawa ya kuua mbu, hata ile ya kikohozi, imeandikwa ‘weka mbali na watoto,’ vipi mabomu yabebayo mauti yawekwe kwapani mwa wananchi?” Waandishi wanapaswa kutafuta.

Jeshi la polisi Dar es Salaam liliendelea kutangaza kuwa “ajali imetokea Gongolamboto,” bila kusema kilichotokea.

Mkuu wa polisi nchini anasema nini juu ya hili? Polisi walikuwa wanajaribu kuficha nini wakati maelfu ya wananchi wakikimbia ndimi za moto?

Rais Jakaya Kikwete anawaambia wananchi wasisikilize kile alichoita “redio mbao” zinazotangaza kuwa mabomu yatalipuka tena.

Je, ana uhakika “amelipua” yote aliyotaka kulipua? Hizo “redio vyuma” au “redio plastiki” zinazosema ukweli ziko wapi na zinasema nini?

Rais aulizwe. Ajibu. Vivyo hivyo waziri muhusika; mkuu wa majeshi na wasaidizi wake. Katika zoezi hili la kutafuta ukweli, askari wa ngazi zote wasikilizwe.

Iwapo waandishi hawatapa majibu kwa maswali haya, watakuwa wameshindwa kazi yao. Viongozi wa serikali na jeshi wakificha ukweli, watakuwa wasaliti wa ukweli, haki na umma.

Hapo suala la milipuko ya mabomu litabaki kuwa simulizi za kishirikina katikati ya teknolojia ya kisasa. Isiwe hivyo.

<p> 0713 614 872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: