Baba yetu anajali misiba


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

WANAUME wote wenye matatizo na ndoa zao huwa hawakai nyumbani. Mabwana hawa huwa mabingwa wa kutafuta njia mbadala ya kuahirisha kero au matatizo ya nyumbani.

Baadhi huwa chapombe wakidhani wakiamka asubuhi matatizo yatakuwa yameisha. Halafu wengine huamua kujificha nyumba ndogo.

Omba usikutane na mwanaume mwenye matatizo na ndoa (utawala) yake. Baba yetu anashinda misibani bila kujali inamhusu au la mradi tu asikae nasi muda mrefu.

Wanamwita Mzee wa Misiba, eti anatamani watu wafe ili apate pa kushinda. Anatia huruma na unaweza udhani siye aliyekuwa anakosa usingizi usiku kucha kwa kumuwaza huyo aliyekuja kuwa mkewe.

Akina baba wenye vijisenti, hasa kama ni mabosi kazini, kama baba yetu, wao huwa safarini kila mara; mikoani au nje wakibadili ndege kuhudhuria mikutano hata isiyo na tija.

Siku wanapolazimika kufika nyumbani (nchini) huwa ni kubadili nguo tu. Hakuna mazungumzo ya upendo na familia.

Tazama, baba yetu aliporudi kutoka safari ndefu ya kule wanakocheza samba, tukafurahi sana. Lakini tulipotaka kumweleza ugomvi wetu na marafiki zake, akasafiri eti kaenda msibani.

Baba anapofika mahali akajali zaidi safari kuliko familia, mke hujuta kuolewa, na watoto hujuta kuzaliwa na baba asiyewathamini. Ukweli sote tunajuta; majuto makubwa kabisa.

Kaka yetu anataka kunyang’anywa cheo Mjengoni, baba hajali; na ndugu zetu wanafilisi duka (nchi) baba hajali. Tufanyeje?

Siku watoto wakiona mama yao anapigwa na baba msafiri hujitosa kuamua. Watoto wanaojua mama yao anaonewa hasa kutokana na anavyohangaika kuwalea humsaidia mama yao kumpiga baba, lakini wasiojali huona mke ni wa kupigwa tu.

Huu ndiyo mwanzo wa baba na mama kutoa huduma kwa watoto kwa upendeleo. Jiulize wewe unapendwa na mama au baba? Je, baba yako anakusikiliza na kukujali?

Ukinijibu baba yako anakujali, halali misibani na hasafiri unataka kujiridhisha tu.

Yule mjomba mkubwa aliyesomea fedha na kule kazini ni maarufu kwa jina la utani la Sieyijii (CAG), amesema baba anawapenda mno mafisadi hata kama wanamtia hasara.

Ametoa siri kwamba duka (nchi) linafilisiwa; wamelipa zaidi ya Sh.8,076,574,791 kununua vitu bila nyaraka sahihi na bila kuwa na maelezo ya kuthibitisha uhalali wake.

Pia amesema bidhaa za thamani ya Sh.31,027,797,820 zilinunuliwa na kulipiwa lakini hazipo. Jumla ya Sh. 142,715,828 walilipwa vibarua (watumishi) hewa.

Amesema, japokuwa tunalala njaa na hatuna kitu deni limeongezeka hadi Sh. 14,441,617,939,770 kutoka Sh. 10,503,806,011,885 mwaka  2009/2010.

Sieyijii amesema mwaka 2005 zilinunuliwa mita ambazo ziliidhinishwa na Wakala wa Vipimo (badala ya kuzamisha fimbo – stick dipping)  kwa ajili ya kuhakiki mafuta yanapopakuliwa melini kabla hayajaingia kwenye matangi ya wafanya biashara.

Lakini tarehe 2 Februari, 2011 wakala yule yule wa vipimo akaandika barua akiagiza kuacha mara moja utumiaji wa mita hizo.

Sababu eti mita hizo zilikuwa zikitoa vipimo visivyo sahihi ikilinganishwa na ujazo halisi unaopatikana kwa njia ya kutumia fimbo kabla na baada ya kupakua mafuta.

Pia eti mita hizo zilitengenezwa mahsusi kwa ajili ya kupima mafuta wakati wa kupakia melini, hivyo basi, kuzitumia wakati wakupakua kunasababisha matatizo mengi yanayotokana na ufanisi mdogo wa mita hizo na kuongeza msongamano wa meli bandarini.

Wajinga ndio tuliwao. Ni vema baba asisafiri kukimbia matatizo, arejeshe mapenzi kwa familia na nyumba, mafisadi hao wanamdhoofisha.

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: