Babu wa Loliondo na ‘Kuomintang 2015’


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KWA sasa, habari kubwa kuliko zote hapa nchini iko Loliondo. Mtu ambaye wengi hawakupata kusikia jina lake likitajwa hata mara moja, Ambilikile Mwasapile (76), sasa amegeuka lulu na habari nzito miongoni mwa Watanzania.

Mzee Mwasapile ambaye anafahamika zaidi kwa jina la “Babu wa Loliondo” anatibia watu wenye magonjwa mbalimbali sugu; kwamba yamekuwa magumu kutibika katika hospitali na hata kwa tiba asili.

Wapo wanaosema kuwa wamepona kutokana na dawa za babu huyo ambaye ni mchungaji mstaafu. Baadhi yao ni viongozi wa serikali na dini ambao wana ushawishi mkubwa kwa jamii. Sijasoma wala kusikia popote kuhusu mtu aliyewahi kutumia dawa ya mzee huyo na kuwa hajapona tatizo lake.

Hata hivyo, sisemi kwamba hiyo maana yake ni kuwa wanaotumia dawa hiyo wote wamepona. Na nikiri mapema kuwa nafahamu dawa hiyo ya “Babu” Ambilikile ni ya kiimani zaidi na ndiyo maana sikuunga mkono wakati serikali ilipotaka kuifanyia dawa hiyo vipimo vya kisayansi ili ionekane kama inafaa.

Katika yote hayo niliyoyasema, nadhani serikali ina wajibu wa kufanya jambo ambalo haijalifanya hadi sasa. Inatakiwa kupeleka baadhi ya wagonjwa waliopo katika hospitali zake kwa mchungaji Mwasapile ili wapewe dawa hiyo na yenyewe ifuatilie kuona kama wanapona kweli baada ya kutumia dawa hiyo.

Itakachofanya ni sawa na majaribio mengine yoyote ambayo wataalamu wake wanafanya. Unachagua wagonjwa wa viwango tofauti na unawapeleka kwa mchungaji. Unachagua wagonjwa mahututi sana, mahututi kiasi na wale walio katika hatua za awali za ugonjwa ambao babu anadai kuyaponya.

Baada tu ya kupewa dawa, serikali iwarejeshe wagonjwa hao hospitali na kuanza kuwafanyia uangalizi maalumu. Kabla ya kuwarejesha, itabidi wamuulize mzee huyo inachukua muda gani kwa mgonjwa kupona baada ya kutumia dawa hiyo.

Ikijulikana ni muda gani dawa hiyo inafanya kazi – kama ni siku saba kama inavyoelezwa na wanaoshuhudia hayo kijijini Samunge kwa “Babu” Mwasapile – serikali itatakiwa kuwatunza wagonjwa hao katika muda wote huo katika hali itakayowazuia wasifanye chochote ambacho masharti ya babu huyo yamekataza.

Baadaye, itawapima upya kubaini iwapo dawa hiyo ya babu inaponya au la. Utafiti wa kisayansi kuhusu kilichomo ndani ya dawa hiyo na madhara au athari zake unaweza kufanyika wakati wowote. Lakini la kwanza ni kubaini iwapo kweli dawa hiyo inaponya.

Ninavyofahamu, maradhi ni miongoni mwa maadui wakuu wa taifa letu. Kama kuna mtu inaonekana ana uwezo wa kulisaidia taifa katika kutokomeza adui maradhi, ni muhimu akapewa msaada na si kuwekewa urasimu.

Kama serikali itaamua kufanya utafiti huu, inaweza kubaini iwapo dawa yenyewe haifanyi kazi. Na kama dawa ina sumu au madhara yoyote, serikali itakuwa na wajibu wa kumzuia Mzee Ambilikile kuendelea na utoaji wa dawa yake hata kama watakuwapo watakaopinga amri hiyo.

Ikibainika kuwa dawa hiyo inaponya, taifa zima litafaidika. Kama serikali itahakikisha kuwa Watanzania wote walioathirika na ukimwi, kisukari au shinikizo la damu wanapata dawa hiyo, Tanzania ndiyo itakayokuwa mshindi kwa namna yoyote ile.

Magonjwa hayo matatu yanaigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha. Magonjwa hayo matatu yamelipunguzia taifa sehemu kubwa ya nguvukazi yake. Ninafahamu wapiganaji, madaktari, walimu, waashi na waandishi wa habari waliofariki kutokana na magonjwa hayo wakati taifa likiwa linahitaji mchango wao.

Ninafahamu kuwa watoto wengi wameachwa yatima au wanakaribia kuachwa yatima kwa sababu ya magonjwa hayo niliyoyataja. Kama dawa ya mzee Ambilikile inaponya kweli, na serikali ikathibitisha, mzigo wa kulea yatima utapungua katika familia nyingi nchini petu.

Nina uhakika pia kuwa nchi yetu itapata mapato makubwa kwa sababu magonjwa haya yameathiri watu wengi duniani. Kama dawa hiyo inaponya kweli, na serikali ndiyo yenye kazi ya kuthibitisha hili, watu watatoka kote duniani kuja kuinunua.

Lakini faida zote hizo zitapatikana kama serikali itafanya jambo la kwanza – ambalo ni kupeleka wagonjwa na kuwafuatilia. Na serikali haina cha kupoteza kwani kama itathibitika kuwa dawa hiyo haiponyeshi lolote, itawatangazia wananchi kwamba “dawa ya Babu Ambilikile haiponyi ugonjwa wowote.”

Huo ndio wajibu wa serikali kwenye suala hilo kwa wakati huu. Ile kuwatumia Dk. Haji Mponda, waziri wa afya, na William Lukuvi, waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) kuchanganya watu, ni mzaha mtupu.

Upande mwingine wa maisha
Hali ya Tanzania kiuchumi kwa sasa si nzuri. Ndiyo maana wanasiasa wanaoonekana kuvutia wengi katika siku za karibuni ni wale wanaozungumzia jinsi hali ya maisha ya Watanzania wengi ilivyo ngumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kwa kasi kubwa huku uwezo wao wa kuhimili ukizidi kudhoofika.

Habari mbaya ni kuwa inaonekana si Tanzania peke yake inayokabiliwa na hali hiyo. Uchumi wa nchi nyingi barani Afrika, Ulaya, Asia na Marekani umeingia katika matatizo kutokana na sababu mbalimbali. Hali inaonekana si nzuri ingawa kuna nafuu ya hapa na pale kutegemea na mazingira ya nchi na nchi.

Kudhoofika kwa uchumi wa kidunia kulikokuja miaka miwili iliyopita ndio chimbuko la tatizo la msingi.

Kwa kuzingatia hilo, nchini Taiwan jambo la ajabu limetokea hivi karibuni. Mgombea urais kupitia chama tajiri kuliko vyote duniani –Kuomintang (KMT) cha Taiwan, Ma Ying-jeou, aliamua kugawa fedha kwa watu waliokuwa wakihudhuria mikutano yake ya hadhara.

Kuomintang, chama kilichoanzishwa Oktoba 10 mwaka 1919, kinakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia kiasi cha kati ya dola milioni mbili na dola milioni 10 (kati ya Sh. trilioni tatu na trilioni 15). Utajiri huo unatokana zaidi na mali zisizohamishika kama vile viwanja, viwanda, makampuni ya uwekezaji, mabenki na biashara nyingine.

Kwa hiyo, badala ya kuwapeleka kina Ze Comedy na Bongo Fleva kwenye mikutano, Ma na Kuomintang aliamua kugawa bahasha kwa wananchi wote wenye hali ngumu ya maisha waliofika kwenye mikutano yake. Na ingawa mshindani wake, Frank Hsieh wa chama cha DPPP na Meya wa Mji wa Taiwan, Taipei, ndiye aliyekuwa kipenzi cha wengi, chama hicho tajiri kilishinda kwa tofauti ya asilimia 17 ya kura!

Hali hiyo ya Taiwan, haraka imenirudisha nyumbani. Kama hali hii ngumu ya kiuchumi nchini itaendelea hadi mwaka 2015 utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine, nani atazuia ushindi wa kile chama au mgombea atakayetumia staili ya KMT?

Kama polisi na walinda sheria wengine wanakwenda kwa Babu Ambilikile kupata kikombe kwanza kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao, nani atawazuia kupanga foleni ili kuchukua fungu lao kabla ya kutazama kama wanavunja au hawavunji sheria?

Hali ni mbaya jamani.

<p> 0718 81 48 75</p>
0
No votes yet