Bado nasubiri ‘maridhiano ya kweli’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SHIDA wanazopata wananchi wengi wakati huu awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura Zanzibar ukiendelea, zinaelezea tatizo la msingi liliopo katika uongozi wa nchi.

Kwamba wapo watu – tena ndani ya serikali na taasisi zake – wanaamini hakuna mfumo wa vyama vingi nchini. Kwao CCM tu ndio chama na chama kimoja tu.

Hata pale penye sheria hawataki kuzifuata. Kanuni na taratibu kwao hazina maana. Wanafanya kazi kwa mazoea. Wanatenda waonavyo siyo wanavyotakiwa kutenda.

Mimi ni mpiga kura jimbo la Fuoni, mkoa wa Mjini Magharibi, ambaye awamu ya kwanza ilipoanza sikupata nafasi ya kujiandikisha. Nikajipanga mapema ili nitumie haki yangu ya kikatiba awamu ya pili ilipofika.

Nikaenda kituoni Kijitoupele kujiandikisha. Nje, nikakutana na Sheha wa shehia yetu, Haji Pandu Ameir anatangatanga.

Msaidizi wake mmoja ndiye aliyeshika wanachoita “daftari la wakazi” akiwa ndani ya kituo. Ndiye anayekagua wanaoingia na kuhitaji huduma ya kuandikishwa.

Lakini kule nje siyo kwamba Sheha anatangatanga bila lengo. Nilibaini utaratibu wa kupenyeza watoto katika foleni ili waandikishwe.

Mbele ya askari polisi anapita msichana ambaye kwa vigezo vyote vya macho alionesha hajatimia umri wa miaka 18. Anapita kwa mtendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na anaandikishwa baada ya kuidhinishwa na Sheha wa eneo husika.

Sikufahamu mahojiano yalivyokuwa kituoni kwani msichana huyu aliingia upande wa kituo cha Shehia ya Pangawe, tofauti na yetu. Ila nilithibitisha kuwa ameandikishwa kwa kuona ameshika kikaratasi maalum wanachopewa walioandikishwa ili kuja kuonesha siku ya kupatiwa shahada zao.

Ndani ya kituo chetu, akaingia mama ambaye kwa vigezo vingi vya macho niliamini ni mtu mzima. Alikuwa ana kitambulisho cha Mzanzibari bali hana shahada ya kupigia kura aliyoitumia uchaguzi wa 2005.

Alipoulizwa iko wapi akajibu “sina maana nilikataliwa kupiga kura.” Alipohojiwa zaidi, alisema urasimu uliowekwa na sheha kwa ushirikiano na watendaji wa ZEC ndio uliomkwamisha.

Akaulizwa “umeolewa.” Akajibu ndio na “nina watoto wakubwa.” Akaulizwa cheti cha ndoa. Akajibu “kiko Pemba kwa baba.” Ikatoka kauli kwamba akifuate.

Mama akagoma kwa kusema “hakuna sheria ya kudaiwa cheti cha ndoa hapa na nyie hamjatangazia wananchi kuwa tukija kuandikisha tuchukue vyeti vya ndoa.”

Mtendaji wa Tume akatazamana na sheha. Sekunde tano, kumi, dakika moja; mama anasubiri. Mtendaji wa tume akasema, “Sheha huyu vipi sasa.”

Sheha akajibu, “naona haki yake.” Hiyo ilikuwa ni “ruhusa” ya kuandikishwa. Nikajiuliza hivi sheha ndiye anathibitisha mtu kuandikishwa na siyo vielelezo alivyonavyo?

Yule mama alikuwa na kitambulisho ambacho kisheria ndio sharti kuulizwa. Ni kweli watu wengi hawakupiga kura 2005 kwa kuzuiwa na mfumo wa kisiasa uliotandikwa. Kwani lazima ya kuchukua shahada imetoka wapi?

Kupewa haki yake, ilikuwa ni bahati tu kwani inazoeleka sasa Zanzibar unapokuja uchaguzi, mwananchi kupewa haki yake ni zawadi siyo sheria.

Katika kituo cha Chuo cha Kiislam Mazizini, jimbo la Dimani, mtu na mkewe waliondoka kituoni bila ya kuandikishwa kwa sababu walidaiwa cheti cha ndoa.

Alitangulia mke kuingia kituoni. Ana kitambulisho cha Mzanzibari, ana shahada ya kupiga kura 2005. Alidaiwa cheti cha ndoa na kushindwa kwake kujieleza vizuri, kulisababisha atolewe nje bila ya kuandikishwa.

Akiwa mlangoni kutoka, alifika mumewe. Akamuuliza, “Umeshaandikisha.” Akajibu, “nimekataliwa kwa kuwa sina cheti cha ndoa.”

Mume akaona ni uhuni bali hakutaka ubishi. Akageuka nyuma, akawasha vespa yake akampakia mkewe, wakaondoka. Hawa bila ya shaka wamekosa kuandikishwa. Ni uhuni tu si sheria iliyowakosesha haki yao.

Baadhi ya watu wanasimulia kuwa pale kulikuwa na maelekezo kutoka kwa “wamiliki” wa jimbo ya kujitahidi kupungaza idadi ya wapiga kura wanaojulikana hawatapigia chama tawala.

Kituo cha Skuli ya Maandalizi, jimbo la Magomeni, nako kumejaa malalamiko. Sheha wa Magomeni, Hassan Ali, ofisa mstaafu wa Polisi ambaye niliambiwa wala haishi Magomeni bali Fuoni, anatuhumiwa kuzuia watu wenye sifa kuandikishwa.

Anasumbua watu waliofika kujiandikisha. Anauliza maswali lukuki. Mengine ya kuudhi. Katika awamu ya pili ya uandikishaji watu waliofika vituoni ni wale tu wenye kitambulisho cha Mzanzibari. Wapo waliokuwa na shahada ya 2005, wengine hawakuwa nayo. Sababu zinatofautiana.

Mtu mmoja alinipigia simu na kunieleza kwamba alikuta watu kama 150 hawakuandikishwa kwa sababu hawana shahada ya kupigia kura ya uchaguzi uliyopita.

Ni rahisi tu kusema wenyewe hawakupiga kura kwa sababu walikataliwa kuingia kituoni siku ya upigaji kura. Wangepata wapi shahada?

Masheha na watendaji wa Tume si kwamba hawajui kuwa watu wengi walikosa kupiga kura, wanatekeleza matakwa ya watawala.

Wakati wanazuia watu wenye haki na vielelezo, wanaruhusu makundi ya watoto kuingia ndani na kuandikishwa. Ndio kusema uchaguzi ujao Zanzibar utakuwa na idadi nzuri ya watoto. Hata wasipopiga kura, inawezekana shahada zao wakapewa wageni kupiga kura.

Halafu unajiuliza, “Hivi katika hali kama hii ya mtandao wa CCM kuendelea kuvuruga taratibu, hiki kinachoitwa maridhiano ya viongozi wakuu yana maana gani?

Wakili mmoja anasema haamini kama kuna maridhiano ya kweli maana yanayofanyika kwenye vituo vya uandikishaji – mengine akiwa ameyashuhudia – ni kinyume na morali ya maridhiano hayo.

Malalamiko ya wananchi kunyimwa haki ya kuandikishwa ili kuja kupiga kura, yanaendelea. Bado wapo wasiokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari kutokana na madai urasimu katika Idara ya Usajili na Kitambulisho.

Lakini wakuu wa idara wanajitetea kwa kusema wamekuwa wakijitahidi kushughulikia ipasavyo malalamiko ya wananchi, bali ni kwa mujibu wa sheria.

Tume ya Uchaguzi inasema uandikishaji unaendelea vizuri. Lakini taarifa zitokazo vituoni kwa mujibu wa vikundi huru vya watazamaji, zinaonyesha hali ni tofauti. Kuna matatizo mengi yasiyokuwa ya kisheria yanayoendelea.

Ukweli sishangai kuendelea kuwepo malalamiko ya watu kunyimwa haki yao ya kuandikishwa, wala ubabe wa masheha ambao ni viongozi wa chini mno kimfumo. Ni kwa sababu mtandao wa kuvuruga uchaguzi haujatokomezwa.

Chini ya mtandao huu, hakuna kitu kama kufuata sheria na kanuni ili kuhakikisha kila mwenye haki anaandikishwa.

Kikubwa ni kwamba naendelea kushuhudia kiapo alichotoa Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame. Huyu alipata kusema, “Tume ya Uchaguzi kamwe haitafikia kuandikisha watu wapatao 500,000 ambao wao wamewapatia vitambulisho.”

Tatizo ni kwamba kulingana na sheria, mtu anayetaka kuandikishwa kuwa mpiga kura ili aingie kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar, ni lazima awe na kitambulisho. Na hiki ndicho watu wengi wanaendelea kulalamikia kuwa kinatumika kuwanyima haki yao ya kikatiba.

Ukiniuliza sasa itakuaje? Nitajibu tu, katika mwelekeo wa maridhiano ya kisiasa kati ya Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, “bado nasubiri kuona maridhiano ya kweli ya kisiasa.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: