Bahari Beach ni mali ya Gaddafi?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Hoteli ya Bahari Beach

WAKATI mataifa ya Magharibi yakitafuta kumning’iniza kitanzini kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, kiongozi huyo ametajwa kuwa na hoteli nchini Tanzania.

Hii ni hoteli ya Bahari Beach ambayo sasa inafahamika kwa jina la LAICO Bahari Beach Hotel.

Hoteli ipo katika eneo la Kunduchi Mtongani, kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi, yapata kilometa 14 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam, hoteli hiyo ilinunuliwa na Gaddafi kupitia kampuni ya LAICO, yapata miaka minane sasa. Hoteli hii ilikuwa ikimilikiwa na serikali.

LAICO ni kifupi cha Libya Africa Investment Company, kampuni iliyoanzishwa na serikali ya Gaddafi kwa lengo la kukuza biashara baina ya mataifa ya Afrika na nchi hiyo tajiri kwa mafuta.

Tayari Umoja wa Mataifa (UN) umetaja LAICO kuwa miongoni mwa mali za Gaddafi zinazopaswa kuzuiliwa kwa madai kuwa, yeye na maswahiba zake ndio wananufaika na uwekezaji unaofanywa na kampuni hiyo.

Aidha, serikali imekana kufahamu kuwa kuna mali za Libya au Gaddafi nchini. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, ameliambia MwanaHALISI kuwa hafahamu iwapo kiongozi huyo ana mali zozote nchini.

“Mimi sifahamu kama Gaddafi ana mali zozote hapa nchini. Siwezi kusema hana kwa vile sina uhakika na ndiyo maana siwezi pia kusema zipo.

“Na hata kama atakuwa nazo (mali), basi uwekezaji utakuwa si mkubwa sana kama ilivyo katika baadhi ya nchi ambazo zimetangaza kuzuia mali zake,” alisema Mahadhi.

Hoteli ya Bahari Beach iliwekwa katika kundi la mali za umma ambazo zilitakiwa kubinafsishwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) katika miaka ya 1990.

Wakati serikali ya Tanzania ikiwa bubu kuhusiana na mali za Gaddafi zilizopo nchini, Uganda tayari imetangaza mali za kiongozi huyo ambaye mataifa makubwa, kwa kutumia UN, yamedhamiria kumwondoa madarakani kupitia wapinzani wake wa ndani.

LAICO imewekeza katika sekta ya hoteli, mabenki na mawasiliano nchini Uganda na serikali ya Yoweri Museveni inakadiria mali za LAICO kuwa na thamani ya dola milioni 345 (Sh.517 bilioni).

Azimio Na. 1973 la UN lililotolewa Februari mwaka huu, lilizitaka nchi wanachama wa umoja huo “…kuwa makini na kufanya biashara na makampuni au taasisi za Libya” kwa vile hilo linaweza kuzifanya nchi hizo zionekane zinamsaidia Gaddafi kukandamiza wananchi wake.

Kwenye tovuti ya LAICO, kuna taarifa kwamba kampuni hiyo inamiliki hoteli katika nchi 11 barani Afrika.

Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Tunisia, Gambia, Mali, Burkina Faso, Gabon, Congo naGuinea.

Kwa ujumla, LAICO inajidai katika tovuti yake kuwa ina vitegauchumi katika nchi 25 za bara la Afrika; katika maeneo ya utalii, mawasiliano, uchimbaji madini na hoteli.

Akizungumzia vitega uchumi vya Libya vilivyopo nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel ole Naiko, amesema ofisi yake haina taarifa yoyote kuhusu Gaddafi kununua mali nchini bali ana taarifa kuhusu mali za Libya.

Amesema kwa mujibu wa rekodi zilizopo katika ofisi yake, kuna makampuni matatu ya Libya yaliyosajiliwa kufanya kazi zake hapa nchini.

Ameyataja makampuni hayo kuwa ni LAICO, Pearl Investmant Limited na Tan Fruit Processing.

“Sina taarifa zozote kuhusu mali za Gaddafi hapa nchini. Ninachojua ni kwamba kuna makampuni ya Libya ambayo yanafanya shughuli zake hapa nchini,” amesema.

Bahari Beach hotel ilikuwa miongoni mwa hoteli kubwa zilizojengwa na serikali ya awamu ya kwanza.

0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)