Bahi wasema ‘chalemaa, wauchee’ watafiti wa uranium


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

SERIKALI inaweza kukaa kimya au, kama kawaida yake, inaweza kufumbia macho kero. Lakini ukweli ni kwamba kuna mvutano mkubwa katika maeneo ya utafiti wa uranium wilayani Bahi.

Wananchi wamewaambia wazi watafiti, “Chalemaa, sichikusaka, wauchee” – Hatupendi, hatuwataki, waondoke!

Kitu pekee kinachojaribu kutuliza hasira za wakazi, hasa wa vijiji vya Ilindi na Mindola, ni taarifa kwamba kazi ya utafiti wa madini ya uranium huchukua muda wa hadi miaka 10 kabla ya kuchimbwa.

Taarifa hiyo iko kwenye maandishi yaliyosambazwa na kampuni ya Tanzoz Tanzania Limited inayoendelea na kazi ya utafiti wa madini hayo katika wilaya ya Bahi. Maandishi hayo, kwenye karatasi maalum, yamebandikwa kwenye ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji.

Yanaonyesha pia maandalizi ya kazi za utafiti, maeneo husika, mitambo ya kuchimbia na muda wa utafiti. Hata hivyo, wananchi wamekosa uvumilivu hasa pale wanapoona watafiti wa kampuni hiyo wakiingia kwenye mashamba yao, tena bila taarifa, na kuchimba mashimo ya kina kipatacho futi 12 hadi 14 na baadaye kuyaacha bila kuyafukia.

“Wenye mashamba walikuja juu. Wakahoji kwa nini hawakushirikishwa wala kuarifiwa kwamba mashamba yao yatachimbwa mashimo makubwa na ya kina kirefu kama yale,” anaeleza mwenyekiti wa Kijiji cha Ilindi, Emmanuel Matonya Masumbi.

“Ulikuwa ugomvi mkubwa. Wenye mashamba walichachamaa wakitaka walipwe fidia kwa mashamba yao kuharibiwa; lakini baada ya mjadala mrefu ikakubaliwa wenye mashamba walipwe kiasi fulani. Baadhi walilipwa Sh. 5,000 na wengine Sh. 10,000 kadri ya mapatano,” ameeleza Matonya.

Hiyo haikuwa suluhu ya kudumu. Uliibuka mtafaruku mwingine baada ya wananchi kuona watafiti wakibeba udongo waliochimba. Kwa vile hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya juu aliyefika kuwapa elimu, wananchi walidhani walichokuwa wanabeba watafiti (wanajiolojia) wale yalikuwa madini yenyewe.

“Wananchi walijua huko ndiko kuchimba kwenyewe. Hivyo baragumu likapigwa kukusanya watu. Magogo yakapangwa njiani kuzuia magari ya watafiti kupita. Wakaamuriwa washushe udongo,” Matonya anaeleza.

“Ilikuwa patashika nguo kuchanika,” anasimulia na kwamba ililazimu yeye, diwani na ofisa mtendaji washughulikie mgogoro huo. Baada ya mjadala mrefu walikubaliana kuruhusu watafiti kuondoka lakini bila udongo. Kingine kilichofikiwa siku hiyo ni kukubaliana kuitisha mkutano wa serikali ya kijiji wiki iliyofuata na kuwaalika watafiti kuhudhuria.

Katika mkutano huo viongozi walipendekeza watafiti wanufaishe vijiji kwa kujenga kliniki, kununua madawati ya shule ya sekondari ya Ilindi na kuchimba visima virefu vya maji.

Kwa upande wao, watafiti walisema watawasomesha vijana kutoka familia zisizojiweza. Baada ya mkutano huo, ilikubaliwa uitishwe mkutano mkuu wa kijiji. Ilielezwa na Matonya na Ofisa Mtendaji wa Ilindi, Mbedegalo Majani kwamba katika mkutano mkuu wa kijiji, uliohudhuriwa pia na watafiti (wazungu wawili na wazalendo watatu), mzungu mmoja “alichafua hali ya hewa” pale alipoeleza, pamoja na mambo mengine, kwamba madini ya uranium yana madhara pindi yakianza kuchimbwa.

Wananchi wa Ilindi hawakusubiri mzungu huyo atoe maelezo ya kina kuhusu wakati gani madini ya uranium huwa hatari na wakati gani si hatari. Waliposikia tu kuwa madini hayo ni hatari, walibadilika na kupaza sauti kwa kusema, “Chalemaa, kwanza sichikusaka kabisa, wauchee!” – hatupendi, kwanza hatutaki kabisa, waondoke!

Mkutano ulivurugika bila kufikia makubaliano. Hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu, vitongoji saba kati ya 10 vya kijiji cha Ilindi, vimethibitika kuwa na mashapo ya madini hayo na utafiti unaohusisha uchimbaji mashimo makubwa na ya vina virefu, unaendelea kuathiri mashamba ya uwele, ufuta, karanga na mahindi.

Maeneo mengine yanayoathirika kutokana na utafiti wa aina hiyo ni uvuvi katika bwawa la Ilindi na eneo la kutengenezea chumvi. Eneo hilo ambalo liko umbali wa kilomita 30 kutoka mjini Bahi lina wakazi zaidi ya 12,000.

Licha ya mkutano huo kukatizwa na vurugu, serikali ya kijiji bado ilivuta subira; ikashauri iandaliwe semina ili watafiti hao wapate muda wa kujieleza kwa kina. Lakini kabla ya kufanyika semina hiyo, watafiti walirudi Ilindi kimyakimya kuendelea na shughuli zao.

“Hapo zilizuka vurugu nyingine hadi akaja kamanda wa polisi wa wilaya (OCD) katika gari aina ya Defender lililojaa askari. Mara ya pili alikuja OCS,” anasimulia Matonya. Alichokifanya OCD ni kuwashinikiza raia wawaruhusu watafiti waendelee na kazi zao lakini alipokuja OCS alisikiliza tu malalamiko ya wananchi na kuondoka akiwa “ameshiba maneno.”

“Kwa jumla asilimia ipatayo 95 ya wananchi wa vijiji hivi vya Ilindi na Mindola, wanasema ‘chalemaa sichikusaka’ na asilimia tano ndio wanakubali kwa masharti kwamba watekelezewe mambo kadhaa niliyokueleza,” anasema.

Kinachochangia vurugu hizo na kutamka “chalemaa sichikusaka” ni ukimya wa serikali ya wilaya, mkoa, serikali kuu na hata mbunge kushindwa kufika kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo. Kuna ukosefu wa elimu sahihi juu ya faida na madhara ya madini ya uranium, anakiri Harun Chibita mkazi wa kitongoji cha Mlimani, Ilindi.

Peter Mtundu wa kitongoji cha Mwenge A anasema kuna sababu tatu za kupinga shughuli za utafiti eneo hilo. Kwanza, watafiti wameingia kinyemela. Pili, faida zake hazitawasaidia wananchi. Tatu, watapoteza maeneo yao ya asili wakihamishwa kupisha uchimbaji na hawajui watakwenda wapi.

Kwa mujibu wa Matonya, serikali inajua mvutano kati ya wananchi na makampuni ya utafiti; kwani kila kampuni inapokurupushwa huenda moja kwa moja wilayani kulalamika na ushahidi OCD na OCS kufika Ilindi.

Tarehe 15 Agosti 2009, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima alitembelea eneo hilo na katika msafara huo alikuwepo Mbunge, William Kusilla na mkuu wa Wilaya, Betty Mkwassa.

Msafara huo ulizomewa na wananchi baada ya waziri kushindwa kuweka bayana majaaliwa ya wakazi hao ambao wamezaliwa, wamekulia, wamesoma, wameoa/ wameolewa na wanazeekea Ilindi/Mindola.

Hapa ndipo serikali ilipasa kutoka usingizini na kuchukua hatua za makusudi za kuielimisha jamii kwa njia ya semina au mikutano ya hadhara juu ya kinachoendelea na madhara ya uranium pale itakapokuwa inachimbwa na kuchenjuliwa.

Serikali haijafanya hivyo. Ama imedharau, imeshindwa, imeogopa au inakataa kutoa elimu hiyo. Wananchi wanajiuliza: Kwa nini? Hawajapata jibu.

0
No votes yet