Bajeti hii inahitaji umakini mkubwa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 June 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MKUTANO wa 20 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza jana mjini Dodoma unatarajiwa kuwa wa wiki tano tu badala ya miezi mitatu.

Mabadiliko hayo ya ratiba yamefanywa ili kubakiza muda wa kutosha kushughulikia mambo mengi ya kitaifa na hasa uchaguzi mkuu wa viongozi.

Bunge hilo linatarajiwa kuvunjwa Julai 16 na baadaye Julai 19, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaanza mchakato wa kura za maoni ili kupata wagombea wa udiwani, ubunge na urais. Vyama vingine vya siasa tayari vimeanza mchakato huo.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Uongozi imepanga mkutano wa Bunge la Bajeti uwe wa wiki tano na kwamba, kila siku wizara mbili zitakuwa zinawasilisha makadirio ya matumizi.

Hii ina maana wabunge watakuwa na muda mfupi wa kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya serikali na kutoa mapendekezo.

Pamoja na muda mfupi uliopangwa kwa ajili ya vikao vya Bunge hili la mwisho katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya awamu ya nne, tunapenda kuwashauri wabunge wawe makini.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukiwashuhudia wabunge wakikwepa vikao muhimu, wakishindwa kuchanganua majimbo yao yametengewa kiasi gani cha fedha katika bajeti na miradi ipi ya maendeleo imepewa kipaumbele.

Tumeshuhudia pia baadhi ya wabunge wakijigeuza mawaziri, kwamba badala ya kuwasilisha hoja ili serikali iifanyie kazi, hujibu maswali ya wapinzani wenye hoja zenye lengo la kuwatetea masikini nchini.

Aidha, tumeshuhudia wabunge wengine wakijali zaidi na kupigia debe vyama badala ya kero na matatizo ya wapiga kura wao.

Halafu wapo wanaopiga usingizi wakisubiri waamshwe kupiga kura kupitisha bajeti. Matokeo ya wabunge wa aina hii ni kuacha mjadala wote wa makadirio ya mapato na matumizi kujadiliwa na watu wachache.

Lakini, mwisho wa miaka mitano ya ubunge wao ukiwa umewadia, baadhi watakuwa bungeni kimwili huku fikra zao zikiwa majimboni.

Kwa kuwa bajeti hii itabeba mambo mengi, huku muda wa kuijadili ukipunguzwa, tunawasihi wajipange vema na wawe makini kutoa michango yenye tija kwa Bajeti itakayowasilishwa kesho kwa maslahi ya taifa.

0
No votes yet