Bajeti kiinimacho


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Waziri mpya wa fedha, Dk. William Mgimwa

BAJETI ya serikali inayotangazwa kesho bungeni mjini Dodoma, imeelezwa kuwa ni “kiinimacho kingine.”

Wasomi, wanasiasa wakiwemo wabunge na baadhi ya wananchi mashuhuri wamesema, zitatajwa tarakimu tu kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini haitakuwa bajeti ya kutekelezeka.

Wengi wamesema wingi wa fedha zilizotangazwa kwa bajeti ya 2012/2013 – Sh. 15 trilioni; na miradi itakayoorodheshwa, siyo hoja.

Hoja kuu wamesema, ni iwapo kiasi hicho kitampa mwananchi nafuu ya maisha na kumwongezea matarajio ya mabadiliko.

Bali kila mmoja aliyeulizwa na MwanaHALISI, alisema kama serikali haikuweza kushawishi wafadhili kutoa kiwango cha fedha walichoahidi mwaka jana, itafanyaje kupata ahadi kwa mwaka huu?

Na kama serikali ilishindwa kukusanya mapato ya kutosha na kuelekeza mafungu katika maeneo yaliyoidhinishwa na bunge, itakabili vipi tatizo hilo mwaka huu?

Kwa mujibu wa tarakimu ziliopo, serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuliko mapato yake.

Aidha, imekuwa ikilalamika kuwa baadhi ya wafadhili hawakutoa ahadi zao na kwamba imelazimika kukopa fedha kutoka mabenki ya biashara ili kuziba mapengo katika mipango yake ya maendeleo.

Waziri mpya wa fedha, Dk. William Mgimwa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita kuwa, wafadhili wamekubali kuendelea kuisadia bajeti ya Tanzania.

Alisema wametoa masharti kuwa ili wasaidie, sharti ionekane kuwa serikali iko makini katika kukusanya kodi na inaimarisha “misingi ya utawala bora.”

Hadi tarehe 31 Mei, serikali ilikuwa bado inawasiliana na Shirika la Fedha Duniani (IMF) juu ya masuala ya kodi.

MwanaHALISI ina taarifa za mjadala mkali na hatimaye maafikiano kati ya pande hizo mbili.

Mashauriano ya mwisho yalikuwa juu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambapo IMF ilikuwa inasema inaunga mkono “uanzishwaji kiwango kipya cha asilimia 10 (10%)…” kwa kundi maalum la watakaopata unafuu.

Hata hivyo, kiwango hicho cha 10% kitakuwa cha muda hadi hapo sheria mpya kuhusu VAT itakapoanza kutekelezwa.

“Tunatarajia kuona kiwango kimoja tu cha VAT na kuondolewa kwa viwango mbalimbali vya upendeleo pale sheria mpya itakapokuwa imeanza kutumika,” imeeleza taarifa rasmi ya IMF kwa wizara ya fedha.

IMF, kwa mujibu wa mawasiliano hayo, inaibana serikali kutoa maelezo jinsi ilivyofikia hesabu ya VAT kuhusu asasi za kijamii.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali, asasi zilitakiwa kulipa asilimia 18 ya VAT kama ilivyokuwa mwaka jana; na kuingiza pato la Sh. 50.6 bilioni.

Sasa IMF inataka kujua serikali itapataje nyongeza ya mapato ya Sh. 22.6 bilioni wakati itakuwa imepunguza kiwango cha VAT kutoka 18 hadi 10%.

Shirika hilo linaibana serikali pia kuhakikisha inalipatia ripoti za kila robo mwaka (miezi mitatu) juu ya matarajio ya ukusanyaji kodi katika Mamlaka ya Mapato (TRA).

IMF ilikuwa inatarajia kutoka serikalini, maelezo ya matarajio ya matumizi kwa kila robo mwaka juu ya kipaumbela katika huduma za jamii – priority social spending.

Maeneo mengine ambayo serikali ilikuwa bado inajadiliana na IMF siku 22 zilizopita, yalikuwa juu ya kodi ya PAYE, ufafanuzi juu ya kodi ya ngozi na gharama za uwanja wa ndege.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anasema ana shaka iwapo serikali itafanikiwa kutekeleza bajeti.

Profesa Lipumba ambaye ni mchumi, anasema kama kwa miongo mingi serikali imeshindwa kutatua tatizo la umeme nchini, haoni ni vipi itatekeleza hilo katika bajeti ya sasa.

“Bila umeme hakuna maendeleo. Sijaona mipango ya kupata umeme wa uhakika; isipokuwa miradi ya kifisadi ya uzalishaji umeme kwa mitambo ya kukodi,” ameeleza.

Amesema utawala mbaya wa CCM umechangia, kwa kiasi kikubwa, kuzorotesha kasi ya ukuaji wa demokrasia, jambo ambalo amesema linakwamisha maendeleo ya nchi.

Anasema katika hali kama hiyo, ni vigumu kuweka matumaini maana bila ya umoja ndani ya chama kilichoko madarakani na serikali yake, huwezi kutarajia ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya serikali.

Waziri kivuli wa fedha, Zitto Kabwe anajadili suala hili kwa kusema kambi ya upinzani inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), itaibana “kisawasawa” serikali kwenye maeneo muhimu yanayochochea ukuaji wa uchumi na upunguzaji umasikini wa wananchi.

Katika taarifa aliyotoa kwa waandishi wa habari na kwenye mtandao wake wa facebook, Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), anasema bajeti lazima ilenge kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa; mzigo wa kodi kwa watumishi wa serikali na kuongeza mapato ya ndani.

“Bajeti yetu, kambi ya upinzani inaelekeza kufuta au kupunguza kodi za bidhaa za chakula ili kushusha kiwango cha mfumuko wa bei kilichofikia asilimia 26,” anasema.

Anasema misamaha ya kodi imekuwa ikitolewa ovyo kiasi cha kuinyima serikali mapato ya Sh. 1.03 trilioni kwa mwaka uliopita huku manufaa yakibaki kwa waliosamehewa kodi kuliko kwa taifa.

Ulegevu katika kukusanya mapato, amesema umeifanya serikali kushindwa kupata fedha za kutosha kutekeleza bajeti ya Sh. 13 trilioni iliyoidhinishwa na bunge kwa mwaka 2011/12.

Amesema serikali imeishia kuendelea kukopa kwenye benki za biashara na hivyo kupandisha deni la taifa hadi Sh. 22 trilioni kutoka Sh. 13 trilioni mwaka 2010/11.

“Tunahitaji kujua fedha zilizokopwa zimetumikaje. Kukopa si tatizo bali tumetumiaje mikopo ndipo penye tatizo… lazima tuhakiki deni hili maana linazidisha mzigo kwa wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Zitto, msisitizo wa kambi ya upinzani utakuwa katika kutumia vema raslimali watu ili kuongeza upatikanaji wa umeme vijijini na kuimarisha huduma za reli ya kati pamoja na njia za reli za Tanga, Moshi na Arusha.

Eneo jingine la kipaumbele kwa serikali kivuli ni utozaji kodi kwa ajili ya kukuza stadi; ambapo fedha nyingi zitapelekwa kwenye vyuo vya ufundi na bodi ya mikopo ya elimu ya juu.

Mbunge wa Kasulu mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), anasema serikali inaleta bajeti “kiinimacho” huku ikiwa na deni kutokana na kushindwa kutekeleza bajeti ya mwaka uliopita.

Machali anasema bajeti iliyopita ya 2011/12 imetekelezwa kwa kiwango cha chini ya asilimia 40, angalau kwa sekta kuu zinazosimamiwa na kamati ya miundombinu – uchukuzi, mawasiliano, sayansi na teknolojia.

“Tumekutana na viongozi wa wizara hizi mbili na kuthibitishiwa kuwa hazikupata fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Uchukuzi imepata asilimia 40 ya bajeti wakati wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia imepata asilimia 30 tu. Namna hii utajenga vipi uchumi? Utasaidiaje shughuli za ubunifu na ugunduzi kiteknolojia?” anahoji.

Amesema serikali ya CCM inaugua ugonjwa wa kutozingatia imepanga nini na itekeleze nini na vipi.

“Utakuta fedha zilizoidhinishwa kwa mradi fulani, zinapelekwa kwenye mradi tofauti. Mimi sina matumaini na bajeti mpya. Hawawezi kutekeleza kitu maana wamefika mwisho wao wa kufikiri,” amesema.

John Shibuda (Maswa Magharibi, CHADEMA) anasema bajeti ijayo ni “bajeti isiyo kitu chochote. Ni bajeti isiyosema wala kujibu shida za wananchi.”

Shibuda anasema kwa Tanzania, bajeti yoyote isiyolenga kushughulikia kwa dhati upatikanaji wa soko la uhakika la mazao ya wakulima, haina maana kwa nchi.

“Kwangu mimi bajeti ya Sh. 15 trilioni haina maana yoyote kama haijibu shida ya soko la pamba, kahawa, korosho na mazao mengine ambayo yanategemewa na zaidi ya asilimia 70 ya wananchi,” anasema.

Shibuda anasema tabia ya serikali ya CCM ya kutosikiliza watu, imeiponza na kilichobaki sasa ni “kuishindilia hukohuko ilikoelekea.”

Dk. Honest Ngowi, mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu Mzumbe anasema, bajeti iliyopita haijatekelezwa vizuri kwa sababu fedha zilizotarajiwa kutolewa na serikali hazikutolewa.

“Ukiangalia mchanganuo, utaona kwamba Sh. 10 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati maendeleo yametengewa Sh. 5 trilioni. Hapa uwezekano wa kupata maendeleo ni mdogo,” anasema.

“Halmashauri nyingi hazikupata fedha zilizopangiwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. Maana yake ni kwamba bajeti haikutekelezwa.”

Dk. Ngowi anasema imefika wakati sasa serikali kuunda mpango wa muda mfupi utakaoweza kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi kutokana na mfumuko wa bei unaoendelea hivi sasa hapa nchini.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Kitila Mkumbo, anasema “…bajeti iliyopita haikutekelezwa kwa kiwango stahiki.”

Dk. Mkumbo ambaye ni mtaalamu wa uchumi anasema, “Hakuna mabadiliko ya maisha ya watu na taasisi; na hali hii inakatisha tamaa.”

Hoja hizo zinaungwa mkono na Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany anayesema, “…hii ni bajeti hewa. Ni kiinimacho; kwa sababu hakuna jipya litakalotekelezwa.”

“Serikali imefikia pabaya kuwaza kila kitu kutekelezewa na wahisani,” anasema na kuongeza kwamba tatizo la wahisani ni kwamba wana hiari ya ama kusaidia au kuacha.

Anasema kwamba kwa kawaida fedha za wahisani ndizo huingizwa kwenye miradi ya maendeleo; kwa hiyo wanaposema mwelekeo wa bajeti mpya ni Sh. 15 trilioni maana yake ni kulipa madeni au kuziba mapengo ya asilimia 70 iliyobaki mwaka jana.

Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) anasema, “Mje bungeni. Siwezi kuzungumza na mwandishi mmojammoja. Maoni yetu yatasomwa bungeni.”

Bajeti ya serikali mwaka wa fedha 2011/12 ilikuwa Sh. 13 trilioni wakati katika bajeti itakayosomwa kesho, serikali imesema itatumia Sh. 15 trilioni.

Mwaka hadi mwaka, bajeti ya serikali imeongeza bei ya bia, sigara na soda. Haitarajiwi kuwa tofauti mwaka huu.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)