Bajeti mpya au chakula cha mafisadi?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

NANI anakataa leo anapoambiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) haijasalimika na ufisadi? Hawezi kutokea. Sasa kila kitu hadharani.

Ushahidi umetoka. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Zanzibar ya mwaka 2008/09 inaeleza yote.

Hii ni ripoti ya wataalamu wa hesabu, ukaguzi na tathmini ambao baada ya kujumuika kukagua namna fedha za serikali – hakika ni fedha za watu wa Unguja na Pemba – zinavyotumika, wametujuza walichogundua.

Ni nini kama si ufisadi wizara sita za SMZ kukutwa zimetumia vibaya karibu nusu bilioni (Sh. 500 milioni) kwa mwaka wa fedha 2008/09? Lakini ripoti ya mwaka uliotangulia, 2007/08 ilikuwa hivyohivyo – ufisadi.

Kumbe tunao kupe wanatunyonya. Tunao manunda wala watu. Kumbe tuna watumishi waovu wanaofaa hasa kuitwa MAFISADI. Hawa ni watumishi wasiojali maisha ya watu bali kwanza wanajali maisha yao na familia zao. Mafisadi wakubwa.

Inakuaje miaka 47 sasa baada ya wananchi kupata unaoitwa “utawala walioutaka” kupitia mapinduzi ya 12 Januari 1964, serikali haiwezi kujua thamani ya kumpa mtu/kampuni fedha kwa mkataba?

Haijui umuhimu wa kutoa fedha na kudai risiti (stakabadhi)? Sasa itasisitizaje yenyewe kuwa mwananchi anayenunua bidhaa muhimu adai risiti? Unafiki! Usaliti!

Haiwezi kujua kweli. Mbona hata wizara ya fedha, tanuri kuu la hifadhi ya fedha za serikali kwa niaba ya wananchi, inatuhumiwa kufuja fedha hizi?

Labda watu hawajui. Wizara ya fedha ndipo ulipo mfuko wa serikali. Walipo wataalamu wa mipango ya uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii. Ni wao wanapanga serikali itumie kiasi gani na itaraji tija gani. Ni wao.

Wizara hii ndiyo ina wataalamu wa aina zote zinazohusu hesabu, mipango, takwimu na tija. Wanaye mhasibu mkuu wa serikali ambaye tangu mwaka 2003(?) anaitwa Omar Hassan “King.”

Wanaye mtakwimu mkuu wa serikali, wanaye kamishna mkuu wa tume ya mipango na wanao wataalamu wa kukusanya mapato chini ya kiitwacho Bodi ya Mapato (ZRB).

Jamani, matumaini ya umma ni kuwa wote hawa ni watu waliobobea kitaaluma. Wasaidizi wao na watumishi wa idara au taasisi zao lazima ni wajuzi wenye viwango kielimu.

Kumbe wenyewe – niseme wakuu wake – wanalea ufisadi; kama siyo kwa kuidhinisha maovu basi kwa kunyamazia wale wanaoyatenda. Kumbe wanadanganya wasaidizi au kushirikiana na baadhi yao ili kutafuna fedha za umma. Hawa ni mchwa.

Kufikia sasa serikali inashindwa kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za wananchi. Huko ni kushindwa iwapo hakuna angalau kesi tatu za kushitaki maofisa wa serikali kwa tuhuma za kufisidi uchumi wa nchi.

Hebu tudurusu ugunduzi wa CAG wa Zanzibar. Ripoti yake inasema: kuna malipo ya Sh. 413.6 milioni yaliyolipwa kwa kazi zisizo mikataba; yeneywe wizara ya fedha nauchumi imetumia Sh. 350 milioni bila ya kuwepo mikataba ya kazi na malipo hayo.

Ripoti inatuhumu pia iliyokuwa wizara ya nchi ofisi ya rais (Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ); Ofisi ya Waziri Kiongozi; wizara ya Biashara, Utalii na Uwekezaji. Yapo mashirika kadhaa yaliyotumia vibaya fedha za umma: Bima (ZIC), Utalii (ZTC), Hoteli ya Bwawani ambayo inaelezwa kuwa ilitia hasara ya Sh. 53 milioni kwa kuwahudumia wateja bila ya kulipwa. Eti wote walikuwa na vibali vya kusamehewa malipo. Eti vibali hivi vilitolewa na viongozi wakuu wa serikali.

Niliposema sasa hakuna atakayethubutu kubisha ufisadi unavyomaliza serikali nilikuwa na maana hasa kuwa maovu haya yalikuwa yakikanushwa.

Niliwahi kuyaeleza zamani haya kwamba SMZ inanuka kwa ufisadi wanaojidhani wana haki zaidi katika nchi wakalalamika na kunituhumu ninatumika. Eti mimi nitumike kuihujumu serikali ya CCM; ili nipate nini?

Sikuvunjika moyo. Nilishambulia serikali ile iliyoongozwa na Dk. Salmin Amour Juma 1990-2000 na iliyofuata chini ya Amani Abeid Karume. Kila moja ilijenga na kulea ufisadi.

Na ilipofika mwaka 2006 baada ya kumsikia rais akijitia hamnazo alipoulizwa kuhusu ufisadi katika serikali yake, nilirudia kusema ufisadi ni tatizo kubwa serikalini.

Zilikuwepo dalili zake kutokana na vitendo vya mtumishi mmoja mmoja. Bali pia hata serikali yenyewe ilishathibitisha ufisadi kupitia mpango wa kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa.

Kipindi kile niliandika mfululizo wa makala nikidadisi kama yale niliyoyabainisha hayakuwa matendo yaliyothibitisha ufisadi. Wakabaki kulalamika chinichini dhidi yangu.

Wakati ule ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) ilikuwa siri kubwa. Wakati wa CAG Keis Khamis (Mwenyezi Mungu amrehemu), ripoti hizi hatukuzipata.

Bila ya shaka ile ilichukuliwa na wakuu wa serikali kama maficho ya uovu wanaoufanya. Wakadhani wataendelea kuficha mambo yanayowatilia mapato makubwa ya haramu.

Nawapinge leo! Hawawezi maana mfumo umekubali. Kila kitu kinawekwa hadharani. Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali inachapishwa kila mwaka.

Ingawa bado haijawa utaratibu kuzigawa kwa vyombo vya habari wala kuzichapisha kwenye mitandao ya kiserikali, angalau zinatolewa.

Baraza la Wawakilishi lililopita, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010, liliwahi kupokea ripoti hii ingawa mjadala wake haukuwa mpana. Kambi ya upinzani ilitaka waliohusika washitakiwe na kufilisiwa. Walionekana fitna.

Leo, arobaini ya mafisadi inatimia. Haipo tena nafasi ya kujificha. Nafasi ya mafisadi ndani ya serikali kuficha matendo yao, wallahi haipo.

Maofisa wa serikali wanaopanga na kutekeleza mipango michafu ya kuibia umma, wanachoweza kufanya ni kuchelewesha tu hatua za kudhibitiwa, hawawezi kuzifuta kabisa. Hawana njia.

Ni bahati nzuri waliokuwa upinzani sasa ni sehemu ya serikali. Iwapo watashiriki kujenga na kulea ufisadi wakati utaamua. Kwa sasa matarajio ya watu ni kwamba ufisadi utakomeshwa.

Serikali ya umoja wa kitaifa inayoshirikisha mawaziri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) ndiyo inayoongoza.

Balozi Seif Ali Iddi ndiye kiongozi mkuu wa serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Je anamtuma Waziri wa Fedha, Uchumi na Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, kusoma bajeti itakayonufaisha watu au ufisadi na mafisadi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: