Bajeti nyingine hatarini kukwama


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Meya wa jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi

KUNA kila dalili za kukwama kwa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, kama ilivyotokea kwa Nishati na Madini, imefahamika.

Hatua hiyo inatokana na serikali kuipangia fedha kidogo wizara hiyo katika sekta ya reli huku kukiwa na kashfa ya uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) katika “mazingira ya kifisadi.”

Habari zinasema kuhusu shirika la UDA limeuzwa kwa bei ya kutupwa ilihali kuna matatizo makubwa ya usafiri wa abiria katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine kama Mwanza na Mbeya.

Taarifa zilizopo ni kwamba UDA, imebinafsishwa kwa Kampuni ya Simon Group Limited kwa bei ya kutupwa ya Sh. 285 milioni badala ya kile kilichoitwa thamani halisi ya Sh. 1.4 bilioni.

Pia kuna habari kwamba ofisi ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inasema kuwa jiji la Dar es Salaam limeshindwa kutambua thamani ya sasa ya hisa 3,631,046 zinazomilikiwa katika UDA ambazo zilinunuliwa mwezi Oktoba 2000 kwa Sh. 363,104,600.

Taarifa zinasema kwamba Simon imenunua hisa asilimia 52 ya shirika hilo hivyo kuwa na sauti ya maamuzi. Hadi sasa imelipa asilimia 12 tu na tayari imekabidhiwa kampuni.

Taarifa zinasema kwamba serikali haijahusika katika mchakato huo ambao Meya wa jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi aliitisha kikao na wenyehisa tarehe 6 Juni mwaka huu na kupitisha azimio la kuimilikisha kampuni ya Simon hisa hizo.

“Masaburi hakutumwa na ye yote wala kikao chochote. Manispaa hazikuhusishwa na wabunge hawakufahamishwa,” kilisema chanzo chetu cha habari na kuongeza: “Baadaye akaitisha kikao cha kamati ya uongozi tarehe 10 Julai mwaka huu ambacho kilibariki uuzaji.”

Kisheria ilikuwa jiji liwe na asilimia 51 na serikali kuu (hazina) asilimia 49, lakini kwa mujibu wa makubaliano ya kumilikishana, Simon itamiliki kwa asilimia 52 na 48 zinabaki kwa jiji na hazina.

“Hali ya uchumi inaonyesha kuwa mwaka 2010 UDA ilikuwa na mabasi 22 tu ikilinganishwa na mabasi 17 mwaka 2009. Kwa wastani mabasi 12 yalikuwa barabarani kila siku kwa mwaka 2010 kulinganisha na mabasi 10 mwaka 2009,” amesema mbunge mmoja ambaye alidokeza kwamba mwaka 2009, thamani ya shirika hilo ilikuwa Sh. 12 bilioni.

Habari zinasema kwamba wabunge wanataka kujua zoezi zima la ubinafsishaji wa shirika hilo kwani wana hofu kwamba huenda kukawa na mazingira ya rushwa “ambayo hatuwezi kuyafumbia macho,” anasisitiza.

Amesema, “…vita dhidi ya ufisadi vinatakiwa kupiganwa katika ngazi zote, lakini inaonekana katika ngazi za serikali na halmashauri, rushwa imeota mizizi na wahusika wa kashfa hii ya UDA nao wapime uzito na wachukue maamuzi wenyewe kabla ya kuwajibishwa.”

Kuna taarifa kuwa jiji la Dar es Salaam limeuza hisa zake linazomiliki katika shirika hilo bila ya kuwasiliana na mwanahisa mwenzake (Hazina).

Pia katika mchakato huo Simon Group aliyesemekana kuwa amenunua hisa hizo aliweka Sh 400 milioni tu kwenye akaunti binafsi ya mwenyekiti wa bodi ya UDA.  Mtoa taarifa anasema, “Hapa serikali lazima itoe kauli kuhusiana na sakata hili.”

Mbali na wabunge hao kutaka kutolea macho suala la UDA, pia wabunge wanatarajiwa kuibana serikali kuimarisha usafiri wa reli ili kuondokana na tatizo hilo kwani mizigo mingi inayokwenda mikoani itakuwa ikisafirishwa kwa njia ya treni badala ya barabara.

“Jambo la kwanza ni  kuiboresha  reli ya sasa ili ifanye kazi kwa uwezo mkubwa kwa kusafirisha abiria na mizigo,” amesema mbunge mmoja.

“Ukiangalia bajeti iliyoombwa, mahitaji halisi kwa fedha za matumizi ya kawaida ni Sh. 63.68 bilioni na fedha iliyotengwa na serikali ni Sh 900 milioni, kiasi ambacho ni pungufu sana ya fedha iliyoobwa,” alisema huku akishangaa namna serikali inavyochukulia jambo hilo kiurahisi.

“Hivi kwa hali kama hii kuna jambo linaweza kufanyika?” anahoji.

Sababu za kushindwa kufanya kazi kwa reli ya kati zinaelezwa kuchangiwa zaidi na menejimenti ya Kampuni ya Rites ambayo inadaiwa kuwa tangu iingie kwenye menejimenti, tarehe 1 Oktoba 2007, imetia hasara ya Sh. 98.386 bilioni.

Kampuni hiyo kutoka India, ilikabidhiwa jumla ya injini 79, mabehewa ya mizigo 1,357 na mabehewa ya abiria 97 yaliyokuwa yakitumiwa na  TRC, lakini badala yake TRL kwa makusudi iliamua kukodisha injini za treni 25 na mabehewa ya abiria 23 kutoka India.

Hata hivyo, kutokana na kutofanyiwa matengenezo,  kati ya injini 79 zilizokabidhiwa TRL, ni injini 39 tu zinazofanya kazi hivi sasa; tena zikiwa chini ya kiwango cha ubora, huku injini  40 zikiwa zimekufa kutokana na kutokarabatiwa.

Kati ya mabehewa 1,357 ya mizigo ni 638 tu yanayotumika na kati ya mabehewa 97 ya abiria ni 45 tu yanayotumiwa; na kwamba yote hayo yako chini ya kiwango cha ubora.

Kwa upande wa mabehewa ya mizigo 1,357 yaliokabidhiwa TRL, hadi sasa mabehewa 719 hayatumiki na kwa upande wa mabehewa 97ya abiria, 52 hayatumiki kutokana na uharibifu.

Mbunge mwingine anasema kwamba hali hii ilisababisha, hadi kufikia Aprili 2010  tangu kubinafsishwa TRC, shirika hilo limepata hasara ya Sh. 98.4 bilioni kutokana na kushuka kwa usafirishaji wa mizigo kutoka tani 57 milioni zilizosafirishwa mwaka 2007 hadi kufikia tani 25 milioni mwaka 2010.

Taarifa zinasema kwamba treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza zilipungua kutoka nne kwa wiki hadi kufikia moja mwaka jana.

“Hii ni aibu kwa serikali inayotarajia kuadhimisha miaka 50 ya uhuru; badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma,” anasema mbunge mwingine.

Wabunge wanaona kuwa Rites ilihujumu na kwamba kilichoonyesha kukera ni kwa kampuni hiyo ya India kuendelea kudai fedha baada ya kubainika kuwako kwa hati za madai.

Miongoni mwa hati za madai (invoisi) ni Na. 055 ya mwezi Julai 2011, inayoonyesha kuwa serikali hadi sasa bado inailipa RITES  Management Service Fee ya dola  10,982 za Marekani kwa mwezi.

Pia kuna hati ya madai Na. 056 ya Julai ya dola 40,498.20 za Marekani.

Katika hati ambazo gazeti hili limeona nakala zake, fedha hizo zinapaswa kuingizwa kwenye akaunti Na. 0011407376 ya benki ya AXIS iliyoko Mumbai, India.

“Katika hili, tunataka ufafanuzi wa juu ya malipo haya huku mkataba ukiwa umevunjwa,” ameeleza.

Hoja nyingine ya wabunge ni gharama za matengenezo ya injini aina ya 88 class kiasi cha dola 1,538,000 hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2011 kutokana na barua ya tarehe 20 Julai 2011 iliyoandikwa na H. L. Chaudhary, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL.

“Hapa kuna mchezo wa kuigiza ambao serikali inawafanyia Watanzania. Kama mkataba umevunjwa ni kwa vipi Chaudhary bado ndiye Mkurugenzi Mtendaji na nyaraka zote zinazohusiana na shirika hilo anaendelea kuzimiliki yeye?” amehoji mbunge.

Wabunge wanataka wahusika wakuu wa mkataba wa Rites wawajibishwe kwa uzembe kwani inaonyeshwa serikali imeingia gharama kiasi cha Sh. 63.68 bilioni katika kufidia kuvunjwa kwa mkataba kati ya TRC na RITES.

Mbunge mmoja anasema, “Jambo hili likiachwa bila wahusika kuchukuliwa hatua, itaonekana kuwa sheria zinabagua (double standards) katika kushughulikia wale wote wanaoliingizia hasara taifa letu au wahujumu uchumi.”

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)