Bajeti: Serikali yajaribu kitanzi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 June 2009

Printer-friendly version

WABUNGE wana siku ya leo na sehemu ya kesho kujadili na hatimaye kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2009/10 ambayo tayari wameita “Bajeti ya fitina.”

HADI sasa, Bajeti ya Mustafa Mkullo ina majeraha na imepata kilema. Wabunge wengi wameonyesha kutokubaliana na sheria hii ya matumizi kwa mwaka 2009/10.

Lakini Mkullo bado anashikilia kuwa serikali imelenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuinua uchumi wa nchi.

Baadhi ya wabunge, taasisi za kidini na wananchi kwa jumla, wana maoni kuwa bajeti imekwenda kinyume na “Maisha bora kwa kila Mtanzania,” ambayo Rais Jakaya Kikwete aliahidi.

Wabunge wengi nilioongea nao wanasema hakuna mahali ambapo mwananchi wa kawaida anaweza kujivunia bajeti hii; wala anakoweza kushika na kusema bajeti itamnufaisha.

Kwa mfano, serikali imesema itatoa fedha ili kusaidia wafanyabiashara na mabenki yaliyokopesha wafanyabiashara hao, ili kukabiliana na kile alichoita, “mtikisiko wa kiuchumi.”

Lakini serikali imeshindwa kutenga hata kiasi kidogo cha fedha kusaidia wakulima wadogo walioathirika na mtikisiko huo wa uchumi duniani na ambao mazao yao yataozea vibandani na ghalani.

Wananchi wanashangaa ni vipi uchumi wa nchi utainuka bila kuweka kipaumbele kwa wakulima wa mazao mbalimbali wakati wanaopewa fedha ni wafanyabiashara wasiolima.

Katika hili serikali haiwezi hata kuthibitisha kuwa fedha zote zilizokopwa na wafanyabiashara kutoka kwenye mabenki zilitumika kwa ajili ya kununulia mazao ya wakulima.

Utakuta baadhi ya walengwa wengi katika mpango huu wametumia fedha zao kutafutia vyeo vya kisiasa.

Tayari kuna maoni kuwa kwa njia hii ya “kusaidia” wafanyabiashara waliokopa benki, serikali imelenga kuhifadhi huko, fedha za kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Ingawa ni mapema, siyo rahisi kupuuzia maoni haya baada ya ukwapuaji wa mabilioni kutoka Benki Kuu (BoT) uliofanywa na makampuni ambayo yanadaiwa kuichangia CCM mwaka 2005.

Aidha, inaonekana bajeti iliandikwa kwa haraka na bila kufanya utafiti wa kutosha na kufikiria mambo muhimu kwa kina.

Lakini kilichozua zogo kubwa ni uamuzi wa serikali wa kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini. Kwamba sasa vifaa vyote vinavyotumiwa na taasisi za kidini, isipokuwa Kurani, Tasbihi, Biblia na Rozali, vitatozwa kodi.

Haikutarajiwa serikali ichukue hatua hiyo. Bali ni vema kuwa Mkullo amesahihisha hili na kueleza hali itarejea kama ilivyokuwa kabla ya kusoma bajeti.

Serikali inajua kwamba karibu asilimia 30 ya elimu ya shuleni inayotolewa hivi sasa, inatolewa na asasi za madhehebu ya dini.

Vilevile wataalamu wa afya wanaeleza  kuwa taasisi za madhehebu mbalimbali ya dini zinatoa huduma kwa karibu robo ya wananchi.

Kwa mfano, madhehebu ya dini hasa yale ya Kikristo yana utitili wa shule za sekondari, vyuo, zahanati na hospitali, na kote huko hakuna ubaguzi wa aina yoyote.

Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo mkoani Iringa, ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Lutherani kinachukua hata watu wasio wa madhehebu maalum.

Hivi sasa, Tumaini kimefungua matawi Makumila (Arusha), TUDACO (Dar es Salaam), Chuo Kikuu cha Askofu Stepano Moshi na KCMC Medical School (Kilimanjaro).

Vyuo vingine vya asasi za madhehebu ya Kikristo ni Chuo Kikuu cha Sebastian Kolola, Chuo Kikuu cha Josiah Kibira (Bukoba), na Chuo Kikuu cha Nyanda za Juu Kusini cha Njombe (Iringa).

Madhehebu ya dini ndiyo yanayomiliki na kuendesha Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Chuo Kikuu cha kupika madakatari –  (Medical School University) Bugando, Chuo Kikuu cha Nyegezi (SAUTI) na Christian Medical Centre (DCMC) kilichopo Dodoma.

Orodha ni ndefu. Kuna Chuo Kikuu cha Askofu Kisanji kilichopo Mbeya, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (Dodoma) na Chuo Kikuu cha Mount Meru kilichopo mkoani Manyara.

Hapa ni nje ya hospitari za wilaya (DDH), zahanati, vituo vya afya na shule za awali na sekondari zilizotapakaa kila kona ya nchi.

Kuna taarifa kwamba kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT), pekee yake linakadiriwa kumiliki na kuendesha shule za sekondari zipatazo 215 nchini.

Pamoja na kwamba madhehebu ya Kiislamu yanamiliki chuo kikuu kimoja tu – Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro na kile cha Ualimu Chang’ombe, bado mchango wake hauwezi kudharauliwa.

Kwa hali hiyo, haikutarajiwa serikali kuanza kukamua taasisi za kidini na kukatisha tamaa wahisani wanaosaidia taasisi hizi, wakati serikali yenyewe haina uwezo wa kumiliki na kuendesha asasi nyingi kiasi hicho.

Kichekesho ni kwamba wakati serikali inakimbilia kukusanya kodi kutoka kwa asasi za kidini, imeshindwa kufuta misamaha ya kodi kwa makampuni ya madini yaliyoko nchini kwa mikataba ya kinyonyaji.

Waziri Mkullo amesema ni makampuni ya madini ambayo yataingia mikataba baada ya 1 Julai 2009, ambayo hayatapewa misamaha.

Hapa kila mtu anaishangaa serikali kwa hatua hii. Kufuta misamaha kwa makampuni ambayo hayajaja kutaka kuchimba madini, ni kiini macho.

Lakini pia uamuzi wa serikali ni wa upendeleo na utajenga matabaka. Ni uamuzi ambao unafukuza moja kwa moja wawekezaji wapya.

Hata hatua ya serikali kukopa fedha kutoka taasisi za fedha za kimataifa na kisha fedha hizo kuikopesha kampuni ya kigeni ya Artumas kwa ajili ya kufua umeme iliyoko Mtwara, ni kushindwa kusimamia fedha za mkopo.

Ingeeleweka iwapo serikali ingekopa na kutumia fedha hizo kununua hisa katika kampuni hiyo kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Hayo yanafanyika wakati bajeti za wizara mbalimbali zimeshuka ikilinganishwa na zile za mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, kwa mfano, Wizara ya Nishati na Madini, iliyopata fedha kidogo, haitarajiwi kuwa na mipango ya uhakika ya kuhakikisha taifa linaondokana na miradi ya umeme ya kuungaunga – huu megawati 20, ule 10 na ule 2.

Lakini hata hizo fedha kidogo ambazo wizara hii imepewa, hakuna mahali ambapo zinaelekezwa kwenye “mipango ya kuleta miradi mikubwa ya umeme.”

Hata katika kilimo hali ni ileile. Wakati serikali inaimba, “Kilimo Kwanza,” fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kununulia zana za kilimo ni Sh. 700,000 milioni.

Kama hivyo ndivyo, basi kiasi hicho kinatosha kununua si zaidi ya trekta 20. Ni wakulima wangapi watafikiwa na huduma hii au kuna walengwa wachache wateule wa serikali? Hii ni bajeti ya mgogoro. Ni bajeti iliyolenga kugombanisha wabunge na wananchi.

0
No votes yet