Bajeti ya serikali ni kitanzi kipya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Waziri wa Fedha na  Uchumi, Mustafa Mkullo

KESHO, Alhamisi, serikali itasoma bajeti ya nne tangu Rais Jakaya Kikwete ashike madaraka, akiwa na kauli tamu na ahadi kedekede zikiwamo, "maisha bora kwa kila Mtanzania."

Bajeti itawasilishwa huku tarayi kuna malalamiko, miongoni mwa wabunge, kuwa bajeti imeonyesha upendeleo na kwamba haijibu ahadi alizotoa Kikwete wakati akitafuta urais na baadaye.

Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo anatarajiwa kuwa na kibarua kigumu wakati wa mjadala wa bajeti; na tayari imeonekana kutakuwa na vipengele vingi vya kubadilisha ili kukidhi matakwa ya wabunge wengi.

Wiki iliyopita, Mkullo aliwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha, mwelekeo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2009/10.

Katika kile alichoita, “Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali,” Mkullo ameweka mwelekeo wa bajeti katika sehemu kuu tano zifuatazo.

Kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua asilimia 18.5 ya pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 16.7 mwaka 2007/08.

Kuzingatia kwa makini vipaumbele vilivyoanishwa kupitia mchakato wa MKUKUTA, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2005 na Malengo ya Milenia.

Kugharamia matumizi ya kawaida ya serikali kwa kutumia mapato ya ndani kwa asilimia 100.

Kuongeza nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali.

Kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa kutoa umuhimu wa kwanza katika kulipa madeni ya mikataba ya ujenzi na kukamilisha miradi inayoendelea, hususani ya miundombinu na maji.

Kama huu ndio mwelekeo wa bajeti ya serikali, wananchi wasitarajie miujuza. Bajeti ya Mkullo haina kipya. Ni bajeti iliyoandaliwa kisiasa, iliyojaa mipango isiyotekelezeka na inayojikanganya kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kwa mfano, wakati Mkullo anasema serikali imepanga kukusanya dola 5,096,016 milioni (sawa na shilingi 5.1 trilioni), hapohapo anakiri kwamba katika bajeti iliyopita, serikali imeshindwa kufikisha lengo la mapato yake.

Katika bajeti iliyopita, serikali iliahidi kukusanya Sh 4.728 trilioni. Lakini hadi kufikia Machi 2009, serikali ilikusanya Sh. 3.2 trilioni tu, ambazo ni sawa na asilimia 91 ya lengo lake katika makusanyo.

Tayari serikali imeshindwa kukusanya Sh. 330,080 milioni katika kipindi cha miezi tisa ya bajeti. Hizi ni fedha nyingi sana na wala haijafahamika pengo hili la 2008/09 linaweza kuzibwa vipi.

Ni Mkullo huyohuyo aliyejitapa mbele ya Kamati, kwamba malengo na matumizi ya serikali yalikwenda kama yalivyopangwa.  Lakini papohapo akasema matumizi ya wizara, idara, taasisi za serikali, mikoa na halmashauri, “yalipungua kutokana na mapato kupungua.”

Sasa swali la kujiuliza ni kama mapato hayakufikiwa, serikali iliwezaje kutimiza malengo yake? Na kama fedha zote zilitumika kama zilivyopangwa, inakuwaje baadhi ya wizara zinalalamika kwamba fedha hazikutosha?

Lakini jingine, Mkullo anataka kuthibitishia Bunge na taifa kuwa haitarajiwi badhi ya wizara zikarudisha fedha serikalini.

Mkullo anajikinga suala la kurudisha fedha serikalini kwa vile katika mwaka wa fedha uliopita, jumla ya Sh. 99.1 bilioni zilirudishwa serikalini na kiasi cha Sh. 7.8 bilioni zikiwa sehemu ya fedha zilizotolewa na wafadhili, nazo zilirudishwa serikalini.

Kwa hiyo, pamoja na serikali kushindwa kukusanya kiasi ilichopanga, serikali hiyohiyo ilishindwa kutumia karibu Sh. 107 bilioni.

Bali, katika mwaka wa fedha ujao, Mkullo amepania kukamua “ng’ombe” – siyo tu maziwa, bali hata damu pale maziwa yatakapokuwa hayatoki.

Anasema serikali itapanua wigo wa mapato kwa kuhusisha vyanzo vipya, kuimarisha usimamizi na kuboresha mazingira ya  uwekezaji.

Hii maana yake ni moja. Wananchi watarajie ongezeko la kodi na kuanzishwa kwa kodi mpya. Ni kawaida ya serikali kuongeza kodi katika vinywaji – soda, bia na sigara. Hilo linatarajiwa kesho katika dhamira ya serikali ya kuongeza mapato.

Hata bei za mafuta – petroli, dizeli, mafuta ya taa na yale kupikia – hazitarajiwi kubaki salama katika mazingira haya ya kukukusanya na kukusanya kila uchwao.

Hatua hizi zinachukuliwa bila hata serikali kuangalia hali za wananchi wake. Hakuna ubishi kwamba hali za wananchi hivi sasa zimekuwa duni, ikilinganishwa na kabla ya Kikwete kuingia madarakani.

Mkullo hatarajiwi kuonyesha, katika bajeti yake ya kesho, jitihada za serikali kupitia upya bei ya minofu ya samaki ambayo tayari wataalamu wa uchumi wanasema, “taifa linaibiwa na wawekezaji.”

Bei ya kilo moja ya minofu ya samaki katika soko la dunia hivi sasa, inakadiriwa kuwa zaidi ya dola nane, wakati serikali inaambiwa bei ya kilo moja ni dola mbili.

Bajeti ya Mkullo haitarajiwi kuzungumzia pia hatua za kukabiliana na ucheleweshaji wa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam, unaosababishwa na uwezo mdogo wa kampuni ya Kupakia na Kupakua mizigo bandarini (TICTS).

Kutokana na mizigo kukaa kwa muda mrefu, mzunguko wa bidhaa unapungua na serikali inapoteza mapato kutokana na baadhi ya wateja kutumia bandari za nchi nyingine.

Serikali makini ilitarajiwa kukabiliana na hali hiyo kwanza, kabla ya kukurupuka na kuanzisha vyanzo vipya vya kodi. Ilitarajiwa wananchi wasikie mipango ya serikali ya kuimarisha kwa vitendo bandari za Tanga, Mtwara na Kigoma ili kuongeza mapato.

Hata katika kukabiliana na kile alichoita, “Mtikisiko wa kiuchumi,” Mkullo hasemi iwapo serikali itaondokana na matumizi holela ya fedha za umma.

Wala hajasema kama mawaziri, akiwamo yeye, wataachana na magari ya kifahari yanayonunuliwa na serikali kila kukicha kama vile Tanzania kuna kiwanda cha kutengeneza magari hayo.

Mkullo haijapiga marufuku safari za viongozi zisizokuwa na tija ndani na nje ya nchi. Badala yake, serikali imetengea kila wizara mabilioni ya shilingi kwa ajili ya safari hizo.

Serikali haijaonyesha kwa dhati jinsi inavyozingatia vipaumbele vilivyoanishwa katika MKUKUTA, ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2005 na malengo ya milenia. Hapa zimejaa kauli tupu za kisiasa.

Hivi hicho kinachoitwa ilani ya uchaguzi ni nini hasa, iwapo serikali imeshindwa kutatua tatizo dogo tu la mgawano wa mapato na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)?

Mkullo anasema serikali zote mbili zimekamilisha uchambuzi kuhusu vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano wa Tangayika na Zanzibar ili kufikia mwafaka.

Suala hili la Tume ya Pamoja ya Fedha lilianza kujadiliwa katika miaka ya 1996 ambapo mjadala ulizuka bungeni juu ya maslahi ya Zanzibar.

Sasa takribani miaka 14 imepita lakini hakuna kilichofikiwa. Badala yake, wananchi wanaendelea kusikia porojo kila kukicha kutoka kwa viongozi wao.

Katika hili moja la mgawanyo wa mapato, tayari tume mbalimbali zimeundwa, ikiwamo tume ya Shelukindo. Hakuna kilichofanyika ambacho wananchi wanaweza kuelezwa na kujivunia.

Sasa, iwapo katika suala hili ambalo limetajwa wazi katika Katiba ya Muungano, kwamba mgawanyo wa mapato uwe asilimia 4.5, linachukua miongo miwili, itatuchukua miaka mingapi kushughulikia mambo mengine?

Je, kwa nini serikali haitoi hicho kinachotajwa kwa Zanzibar, badala yake inaendelea kutumia fedha za wananchi kwa kisingizio cha kuunda kamati ya kutafuta mwafaka? Ni mwafaka gani unaoweza kwenda kinyume cha Katiba ya nchi?

Katika bajeti ya mwaka huu, serikali inasema itagharamia matumizi yake ya  kawaida kwa kutumia mapato ya ndani kwa asilimia 100.

Je, kama katika bajeti iliyopita, mapato hayakumalika, serikali ina uhakika gani wa kutimiza malengo yake kwa kutumia fedha za ndani.

Lakini ukiacha hilo, katika bajeti ya mwaka huu, serikali imesema itakusanya na kutumia Sh. 5,096,016 milioni (trilioni 5.1), lakini papo hapo inasema itatumia kiasi cha Sh. 6,688,254 trilioni kwa matumizi yake ya kawaida.

Kwa mujibu wa sura ya bajeti, mapato ya serikali yatakuwa Sh. 5,096,016 milioni; mikopo na misaada ya nje Sh.  3,181,948 milioni; mapato ya halmashauri Sh. 138,052 milioni; mapato kutokana na mauzo ya hisa Sh. 15,000 na mikopo ya ndani Sh. 1,082,669 milioni.

Kutokana na hali hiyo, serikali italazimika kutumia hata fedha za wafadhili kugharamia shughuli zake za kawaida.

Hata hicho kinachoitwa nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali, hakiwezi kupatikana iwapo serikali inashindwa kukabiliana na rushwa, ikiwamo rushwa katika mikataba.

Kwa mfano, serikali imeshindwa kuboresha matumizi ya gesi asilia ambayo ingetumika kuokoa mabilioni ya shilingi yanayolipwa kwa makampuni binafsi ya kufua umeme yaliyotapakaa nchini.

Baadhi ya makampuni hayo kama vile, kampuni ya Tan Power Resources ambayo inazalisha megawati 1 ya umeme, lakini tayari ikiwa serikali imeichotea mabilioni ya shilingi za wananchi kwa kile inachoita, “kuipa uwezo.”

Aidha, ukamilishaji miradi ya miundombinu na maji inayoendelea, ni mgumu kufanikiwa. Hii ni kutokana na kupanda holela kwa gharama za ujenzi, hasa katika miradi ya barabara.

Mifano ni mingi katika eneo hili. Gharama za ujenzi wa barabara nyingi zimepanda maradufu na serikali imeshindwa kuchukulia hatua wale wanaohusika.

Kwa ujumla, kama mwelekeo mzima wa bajeti ni huu ulioelezwa na waziri kwa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha,  basi bajeti mzima haileti matumaini kwa wananchi.

Bajeti haielezi uanzishaji wa viwanda vipya, au uendelezaji wa vilivyopo. Ni bajeti ileile ya kutegemea kila kitu kutoka nje.

Kitendo cha serikali kushindwa kuchukua hatua za kutafuta fedha kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika, na badala yake inategemea fedha zote za maendeleo kutoka kwa wahisani, kinaweza kuiumiza nchi iwapo wafadhili watashindwa kutoa fedha kutokana na msukosuko wa kiuchumi unaoendelea duniani.

Hata vipaumbele vilivyoainishwa ni vingi mno ikilinganishwa na kiasi cha fedha kilichopo. Serikali inaimba “Kilimo Kwanza,” lakini imeshindwa kutoa vipaumbele katika elimu na afya. 

Ni kutokana na kushindwa kuweka vipaumbele, kunakoweza kufanya tuwekeze katika kilimo na hatimaye kukuta tunarudi nyuma kwa kurudisha ujinga na maradhi.

Hoja kubwa hapa ni kuchagua tunachotaka, kupanga na katika kupanga ndiko kunakuwa na vipaumbele. Ukosefu wa hili umekuwa dondandugu kwa serikali.

Jingine ni kwamba hakuna mipango inayojulikana ya maendeleo. Katika mambo kumi yalioonyeshwa katika bajeti iliyopita, hakuna hata moja ambalo serikali inaweza kusema, “hapa tumefanikiwa.”

Tayari Mkullo, na Gavana wa Benki Kuu (BoT) Beno Ndullu, wamejichanganya na kuchanganya jamii. Waliishasema kwamba mtikisiko wa uchumi duniani hauwezi kuathiri Tanzania.

Sasa Mkullo anasema mtikisiko umeathiri mapato ya serikali na tayari imeundwa tume inayoongozwa na Gavana Ndullu kushughulikia suala hilo.

Ni gavana yuleyule aliyelihakikishia taifa na dunia, kwamba mtikisiko huo haujagusa uchumi wa nchi ambaye sasa ameteuliwa kuongoza tume ya kuangalia ni kwa kiasi gani mtikisiko umeathiri uchumi wa nchi.

Haitarajiwi kwamba uzembe uliotokea katika bajeti iliyopita, wa kushindwa kusimamia sera za fedha za nchi hadi kufikia wafadhili kusimamisha misaada, utakuwa umeondoka mwaka huu.

Ni uzembe huohuo wa dhahiri uliosababisha kushindwa hata kukusanya kile kidogo kilichokuwako. Bajeti haitoi mwelekeo wa kuondokana na hilo.

Haitarajiwi pia makosa ya mwaka jana ya vitabu kuwa na mpungufu, yakajirudia tena mwaka huu. Katika Bunge la mwaka jana, vitabu alivyowasilisha Mkullo vilionekana vimekosewa na kulazimika kuwasilisha vitabu vingine.

Lakini jingine ambalo ni kubwa zaidi ni kwamba Watanzania watarajie tena mfumuko wa bei, kutokana na hatua ya serikali kukopa katika mabenki ya ndani.

Haijulikani uamuzi huu wa kukopa ndani umerudishwa lini. Kinachotajwa ni kwamba serikali ilisitisha ukopaji katika mabenki ya ndani.

Hatua ya kukopa katika mabenki ya ndani, kwa serikali isiyokuwa na uwezo wa kusimamia uchumi wake na katika mazingira ya kutegemea fedha za wafadhili, ina matokeo mawili ya haraka:

Kwanza, kama utegemezi huo ni mkubwa, serikali itashindwa kujiamulia mambo yake yenyewe katika maendeleo ya nchi. Pili, kwa ukosefu wa usimamizi wa fedha, serikali inaweza kushindwa hata kurejesha fedha kule ilikokopa.

Siku 60 za bunge la bajeti ambalo lilianza jana, Jumanne 9 Juni 2009 mjini Dodoma, zaweza kuwa za minyukano ya aina yake kati ya wabunge na serikali.

Bali mwelekeo wa bajeti ya serikali unatoa sura ya jiwe kubwa, nene na zito lililofungwa shingoni mwa wananchi. Kwa kitanzi hiki, matumaini ya wananchi ya kuwa na “maisha bora” yanazidi kupotea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: