Bakhresa ambeba Ramadhan Nassib


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Michezo

AKISIMAMIA jambo, mara nyingi linafanikiwa. Katika masuala ya soka, hata kama akiamshwa usiku wa manane, hujibu swali lolote. Pengine ni kwa sababu ya weledi unaotokana na uzoefu katika masuala ya mchezo huo wenye mashabiki wengi duniani.

Ninamzungumzia Amin Bakhresa, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), ambaye pamoja na baadhi ya viongozi wenzake wa mikoa, wameungana kumuunga mkono Ramadhan Nassib kutetea kiti cha makamu wa pili wa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika 28 Februari mwaka huu, atachaguliwa pia mjumbe wa kamati ya utendaji kutoka kanda ya tano inayojumuisha mikoa ya Mbeya na Rukwa, kutajazwa nafasi ya Theophil Sikazwe aliyefariki dunia 28 Juni mwaka jana.

Nafasi ya makamu wa pili inatarajiwa kujazwa baada ya Villa Squad iliyomdhamini Ramadhan Nassib, kupoteza sifa kwa kushuka daraja msimu uliopita, hivyo kwa mujibu wa katiba, kiongozi huyo anapoteza sifa.

Gumzo limekuwa ni juu ya kujaza nafasi ya Nassib. Jumanne iliyopita nilikutana ghafla na Bakhressa, katikati ya jiji, ambaye pamoja na mambo mengine alijibu maswali yangu matano ya haraka. Bakhressa na wenzake, wamejitokeza kumchukulia fomu Nassib kabla ya kuirejesha kwa niaba yake wakitaka agombee tena.

Swali: Nassib amepoteza sifa za kuwa makamu rais TFF, imekuwaje nyie kujitokeza kumsapoti?

Bakhressa: Aah (kicheko), nataka nikufahamishe kwamba Nassib hajapoteza sifa. Iliyopoteza sifa ni klabu ya Villa Squad. Nassib alidhaminiwa na klabu hiyo ambayo kwa kweli, hali halisi ni kama unavyoona, ilipoteza sifa kwa kushuka daraja.

Swali: Watu wanasema, ingekuwa vema klabu zingemchukulia fomu badala ya ninyi viongozi wa vyama vya soka vya mikoa.

Bakhressa: Huu nao ni ufinyu wa mawazo. Watu wamesahau kuwa kabla ya Tenga (Leodgar) kuwa rais, wakati ule (2004) wa mchakato, wadau wa soka ndio waliojitokeza kumchukulia fomu. Hakuna aliyehoji.

Mwaka juzi (2008), kabla ya kutangaza nia, klabu ya JKT Ruvu ilimchukulia fomu Tenga. Je, JKT ni chama cha soka? Leo hii inakuwa dhambi kwetu sisi kumchukulia fomu Nassib ambaye tunaona anatufaa?

Swali: Mna sababu gani za kumsapoti katika kuwania tena nafasi hii?

Bakhressa: Nassib anahitajika. Huyu jamaa amefanya kazi. Sisi tunajua kwa sababu tuko kwenye mpira siku nyingi.

Utendaji wake, hasa katika kuratibu na kusimamia mashindano kama ligi na ulinzi wa mapato uwanjani, umekuwa wa mafanikio kwa kipindi cha mwaka mmoja aliokaa madarakani. Ni mtu anayejua wajibu wake. Sisi tumeona kuwa tusimwache. Si vizuri kumpoteza.

Kwa sababu hizo, tumeangalia katiba, tumeona kabisa hakuna sehemu inayoweza kumzuia kugombea tena. Tumemshawishi na kumchukulia fomu; tukamwambia jaza na tutairejesha TFF.

Kitu kingine watu lazima waelewe, sisi si kamati ya uchaguzi; tumefanya kitu ambacho tunadhani kuwa tuna haki: kumchukulia fomu, kumuomba kujaza na kuirejesha. Bado kuna usaili na uchaguzi. Wajumbe wataamua, lakini sisi pia tuna haki ya kupiga kura.

Swali: Pengine unifafanulie kwa undani malengo ya harakati zenu?

Bakhressa: Kwa hakika, sisi tunataka kuusukuma mpira uendelee mbele. Kwa kiasi kubwa Nassib amesaidia mapato kuongezeka katika viwanja vyetu. Halafu ni muungwana. Ligi ya mzunguko wa kwanza imechezeshwa fairly, hakuna mambo ya rufaa kama zamani wala ligi kuahirishwa. Haki inatolewa bila kujali timu, yaani kila kitu ni fair.

Swali: Nasikia eti mnataka arejee ili kuhakikisha timu moja ya Dar ambako wewe Bakhressa ni mwenyekiti wa mkoa, inapanda daraja, halafu na rafiki yako Said Soud wa Tanga, naye ameahidiwa Coastal Union kupanda daraja. Hili likoje?

Bakhressa: Watu wameishiwa hoja. Nimesema Nassib ni muungwana. Hivi angeamua kuibakiza Villa ili abaki TFF si angefanya hivyo pengine kwa kutumia nafsi yake ya makamu rais? Angekuwa si muungwana Villa Squad isingeshuka.

Lakini alisimamia haki, na kwa nafasi yake ni mwenyekiti wa mashindano; angeweza kujipendelea lakini kijana wa watu aliacha mpira uchezwe uwanjani kwa kufuata sheria 17 za soka na Villa ikashuka.

Kuna jambo la ajabu katika katiba. Kwanza haimzuii kugombea. Pili, katiba ya TFF ina sehemu inajichanganya ambayo inaonyesha makamu atabaki kwa miaka yote minne; na kuna sehemu inasema kuna ukomo kama huu wa Nassib.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: