BAKWATA itakufa CCM ikiondoka madarakani


Dk. Hassan Nassir's picture

Na Dk. Hassan Nassir - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Kiongozi mkuu wa BAKWATA,  Mufti Simba Shabani Bin Simba

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limepotea njia. Baraza hilo lililoanzishwa mwaka 1968 kwa nia ya kutetea maslahi ya waislam, limeacha kazi yake ya asili iliyokusudiwa, badala yake sasa linafanya kazi ya kutetea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake.

Kiongozi mkuu wa BAKWATA, Mufti Simba Shabani Bin Simba, amekuwa akisikika akituhumu viongozi wa vyama vya upinzani kuwa wanataka kuleta vurugu, huku akiacha jukumu lake la msingi la kutetea waislam.

Wala hakuna shaka kuwa BAKWATA, chombo chenye mamlaka ya kusimamia waislam, kilichowahi kuwa na mahusiano mazuri na wafadhili wa ndani na nje, imekuwa taasisi ya mwisho kimaendeleo kutokana na viongozi wake kuingiza siasa ndani ya chombo hiki.

Matumaini yaliyobaki ya waislam kwa BAKWATA, ni ya kiimani zaidi kama kupata taarifa za kuandama mwezi mtukufu wa Ramadhan na kusherehekea sikukuu za kiislam. Basi!

Wakati baadhi ya taasisi za kidini zinashindana na serikali katika uanzishwaji wa vyuo vikuu, hospitali za rufaa kama Bugando na KCMC, BAKWATA imeishia kumiliki zahanati, vituo vya afya na shule za sekondari zinazoongoza kwa matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne na sita.

BAKWATA haina hata chuo kikuu kimoja inachokimiliki, wala ardhi iliyotengwa kwa ajili hiyo. Pengine inasubiri kupewa jengo na serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro hakimilikiwi na BAKWATA, wala majengo yake yaliyotolewa na serikali wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa.

Wakati Mtume Muhammad (SAW) alipanga mikakati madhubuti kusaidia waislam kwa kuanzisha benki ya waislam (Baitl-Mal) na kuwachagua viongozi makini na wenye uchungu wa maendeleo kuwa wasiadizi wake, uaminifu wake katika kutunza mali za waislam na wasiokuwa waislam uliwavutia hata waliokuwa wakimpinga.

Inaelezwa kwamba msimamo huo wa mtume, ndiyo chanzo cha ndoa yake na Bi. Khadija ambaye historia inaonyesha kabla ya kumuoa alikuwa mfanyakazi wake katika masuala ya biashara. Mtume alitunza kwa uaminifu mkubwa na hatimaye Bi. Khadija alivutiwa na kufunga naye ndoa na mtume.

Baada ya kufariki masahaba walichukua jukumu la kuwatumikia waislam, waliogopa kula mali ya waislam. Waliwasikiliza na kuyatatua matatizo yao, walitoa chao kuwapa wenye shida siyo kuchukua cha wenye shida kutia matumboni.

Yote haya walifanya kwa kuamini uongozi ni dhamana, na kubwa zaidi wakiamini ipo siku watasimama mbele ya Mwenyezi Mungu na kujibu jinsi walivyotumikia waliowaongoza.

Ni tofauti na viongozi wa sasa wa BAKWATA ambao husoma tu historia za masahaba na makhalifa waliowahi kutumia jamii ya kiislam kama vile umar bin Abdul Azeez (R.A).

Swali linakuja, kama hivi ndivyo, mbona tuhuma dhidi ya kutafuna hata mali za yatima na wale wasiojiweza zinazidi kuongezeka katika chombo hiki?

Baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, Desemba 2005 alikuwa mgeni rasmi katika baraza la Iddi mjini Arusha. Katika hotuba yake, aliilaumu BAKWATA kwa kushindwa kuwatumikia waislam kwa dhati.

Alisema waislam wameichoka BAKWATA na kwamba chombo hicho kimekuwa kama kikundi cha watu wachache chenye manufaa binafsi.

Waliokuwapo na waliosikiliza kupitia vyombo vya habari waliona jinsi waislam walivyozizima kwa furaha kutokana na kauli ya rais. Waliokuwapo ukumbuni walipiga takbir kwa kishindo kuashiria wameguswa na kauli ya rais.

Hili lilitokea mbele ya wafuasi wa BAKWATA na viongozi wake. Ulikuwa ujumbe kwa Mufti Simba na waislam kwa ujumla, hasa wale wanaotaka mabadiliko katika utendaji wa chombo chao.

Vyombo vya habari viliripoti kauli ya rais, na kwamba wengi waliamini kuwa kauli ya mkuu wa nchi ingesaidia kuwatoa BAKWATA katika usingizi wa pono. Wapi!

Nyingi ya shule zinazomilikiwa na BAKWATA zinatoa matokeo mabovu katika mitihani ya kidato cha nne na sita; huku zahanati zake nyingi zikilaumiwa kwa kutoa huduma duni.

Wengi walitarajia kuwa chombo hiki kingetumia raslimali zake kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabenki, hospitali, vyuo vya elimu ya juu na kuanzisha mifuko ya pensheni kwa wafanyakazi wa taasisi zake. Wangetumia misaada inayotolewa kwa faida ya waislam na jamii kwa ujumla.

Hoja kwamba waislam hawapendi kusoma haiwezi kuingia akilini mwa wengi. Mamia kwa makumi ya waislam wanasoma katika vyuo vikuu mbalimbali dunuani kama vile Khartoum, Tehran, Misri, Algeria, Senegal. Wengi wao wamejikita katika masomo ya uhandisi, udaktari, kilimo, teknolojia, uhusiano wa kimataifa na hata sheria za kimataifa.

Je, nani asiyetambua jinsi Zanzibar ilivyotikisa nyanja ya habari duniani? Kwa mfano, Zeyana Seif, mwanamke wa kwanza Afrika ametangaza idhaa ya Kiswahili ya Uingereza (BBC).

BAKWATA wanafahamu kuwa waislam walikuwa wa kwanza kuandaa mpango wa kujenga chuo kikuu cha kimataifa huku viongozi wa jumuiya za kiislam wakitafuta misaada ndani na nje.

Baadhi ya waislam licha ya umasikini waliokuwa nao walijitolea kuchangia kabla jumuiya hiyo kukumbwa na mgogoro na hatimaye kuvurugika na majukumu ya jumuiya hiyo kukabidhiwa BAKWATA. Maafa ya waislam kimaendeleo yalianza hapo.

Katiba ya BAKWATA imelalamikiwa mahakamani na baadhi ya waislam kuwa ina mapungufu. Lakini hadi leo BAKWATA haijatatua tatizo hilo kwa faida ya jamii ya kiislam.

Aidha, BAKWATA badala ya kujiingiza katika siasa, ingejikita katika kusimamia mali za waislam zilizouzwa na zinazouzwa na baadhi ya viongozi wake kinyume cha taratibu.

Tarehe 17 Aprili 1991, rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi aliwataka  waislam kukaa pamoja na kutafuta suluhu juu ya mgogoro wa chombo chao, lakini BAKWATA imegoma kutii agizo la kiongozi huyo kwa kudhani kuwa inalindwa na CCM. Wapo wanaosema, siku CCM ikiondoka madarakani, BAKWATA nayo itakufa kifo cha mende.

Wanaosema CCM ikishindwa uchaguzi BAKWATA itakufa wanasema pia kuwa kifo cha BAKWATA utakuwa mwanzo mpya wa kimaendeleo kwa jamii ya kiislam na waislam kwa ujumla.

Waislam wanalalamika kunyimwa fursa za maendeleo na watawala wanaolalamikia hali hiyo, siyo Mufti wala viongozi wakuu wa BAKWATA.

Kuna taarifa mara baada ya wakiristo kufunga mkataba na serikali (MoU) baadhi ya taasisi za kiislam zilikaa na kutunga rasimu ya mkataba kama huo na kuupeleka serikalini kwa manufaa ya waislam, lakini walipata vizingiti huku serikali ikitaka BAKWATA iandae.

BAKWATA imekaa kimya. Haitaki kutenda yale ambayo waislam wanataka. Wanadhani kwao hilo si tatizo, bali tatizo ni CHADEMA.

Je, katiba ya BAKWATA si inasema kila kiongozi wa BAKWATA lazima awe muislam mwaminifu mwenye kufuata quran na sunna, wapi wanapoteleza viongozi hawa kuwatumikia waislam?

Mwandishi wa makala hii, anaishi nchini Ufaransa amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI kupitia mtandao. Anapatikana kwa imeil:hushuni@hotmail.com
0
Your rating: None Average: 3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: