Balozi Ndangiza: Rwanda tumebadilika leo


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

“LIPO tatizo la msingi kuhusu nchi yetu Rwanda. Unajua jumuiya ya kimataifa ilishindwa kuzuia mauaji ya kikatili. Wenyewe tukayasimamisha. Katika kipindi kifupi nchi yetu imejenga uwezo katika mambo mengi na tunaendelea vizuri. Watu wengine wanatushangaa tumefikaje hapa.

“Basi hawatupendi na wanajitahidi kutuvuruga, unaona wanajitahidi kutugombanisha na jirani zetu tunaoshirikiana nao vizuri hasa katika Afrika Mashariki. Watu wajue Rwanda ya leo ni Rwanda mpya siyo ile wanayoifahamu ya zamani.”

Ndivyo asemavyo Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Fatuma Ndangiza aliyefanya mahojiano maalum na MwanaHALISI, Jumanne ya 20 Julai 2010, ofisini kwake Upanga, jijini Dar es Salaam.

Balozi Ndangiza analalamika kwamba kuna watu wanaichukia Rwanda, wanaitaka isimame katika kupata maendeleo. Wanaitaka igombane na jirani zake ikiwemo Tanzania.

Anasema, “Wanataka kuona Rwanda inabaki nyuma. Wanaichukulia Rwanda ile ya zamani iliyokabiliwa na ukabila. Tumebadilika sana na tumefika hapa kwa nguvu nyingi sana. Hatuwezi kurudi nyuma.”

Malalamiko ya Balozi Ndangiza yanakuja sasa baada ya kuibuka madai kwamba ni Rwanda iliyohusika na mauaji ya Profesa mahiri wa sheria nchini Tanzania, Jwani Mwaikusa, aliyezikwa wiki mbili zilizopita nyumbani kwake Tegeta Salasala, nje ya jiji la Dar es Salaam.

Profesa Mwaikusa, aliyekuwa mmoja wa wahadhiri waandamizi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na wakili wa Mahakama Kuu, aliuawa usiku wa Julai 13, mwaka huu, kwa kupigwa risasi pamoja na watu wengine wawili wakati anawasili nyumbani kwake. Wauaji hao hawakuiba chochote walipoingia ndani.

Serikali ya Rwanda inatajwa kuhusika kutokana na mchango muhimu wa Profesa Mwaikusa katika utetezi wa watuhumiwa wa mauaji ya halaiki, yaliyofanywa nchini Rwanda mwaka 1994.

Profesa Mwaikusa alitoa hoja zilizosababisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda (ICTR) iliyoko jijini Arusha, Tanzania, ikatae maombi ya waendesha mashitaka kutaka mtuhumiwa anayemtetea, Mustafa Munyakazi (75), apelekwe nchini Rwanda kushitakiwa.

Lakini Balozi Ndangiza anakanusha madai. “Hatuna manufaa yoyote tutakayopata tukifanya hivyo. Serikali yetu inaheshimu haki za binadamu na inaheshimu mchango wa watu wote wanaosaidia katika kufanikisha haki kwa watuhumiwa waliopo ICTR.

“Sisi Rwanda tumeondoa adhabu ya kifo. Ni kielelezo cha kutambua kwetu haki na kuheshimu haki ya mtu kuishi. Rwanda ya leo ni Rwanda mpya.

“Tumeshatoka kule tulikokuweko. Hatuwezi kurudi nyuma eti kupanga au kuua mtuhumiwa au wakili anayemtetea. Itakuwa kinyume na dhamira yetu ya kujenga jamii inayofuata sheria na kupenda haki za watu.

“Sasa kila hatua tunayoichukua katika serikali inalenga kushawishi Wanyarwanda kupendana na kuacha utaratibu wa kulipiza visasi kwa mtu yeyote. Tunawajenga imani watu wetu wapende kusameheana.

“Tunaendeleza jamii yenye upendo na inayokubali maridhiano. Hivi mtu aliyeua wakati wa mauaji yale (1994) utamfanya nini? Watu tungependa watuelewe hivi. Hatuna tatizo hata kidogo na Watanzania,” anasema.

Akisisitizia kazi ya Mahakama inayoshughulikia watuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda, Balozi Ndangiza anasema serikali ya Rwanda imekuwa ikijadiliana na Umoja wa Mataifa juu ya uwezekano wa kuhamishia Rwanda kesi zote kwa kuwa ICTR inamaliza muda wake.

Katika hali kama hiyo, anasema, ndiyo maana serikali imekuwa ikiimarisha ujenzi wa uwezo wa mfumo wa kisheria ili kuja kusimamia kesi hizo kama inavyofanya kwa kesi zinazoshughulikiwa na mahakama za kijadi za Gacaca nchini Rwanda.

Serikali ya Rwanda ilianzisha mahakama hizo ili kushughulikia watuhumiwa waliohusishwa na mauaji ya 1994 waliopo nchini Rwanda. Ingawa zimepewa nguvu ya kisheria, zinalalamikiwa kwa ukiukaji wa haki.

Lakini hilo haliingii akilini mwa Balozi Ndangiza kwani anasema watu wanalaumu tu lakini “nani amefanya utafiti na kuja na ripoti inayozipinga kuwa hazifai?”

Balozi anasema serikali imeanza kupitia majalada ya kesi zilizoko ICTR Arusha ambazo zinaweza kwenda kushughulikiwa na mahakama za kisheria za Rwanda. “Unajua haiwezekani mahakama ya ICTR ikawepo tu bila ya kufika mwisho wa kazi zake maana hao watuhumiwa watakwisha. Mhimizo wa Rwanda haupo kwa kesi moja tu kama watu wanavyowaza.”

Wapo wanaoiona hali ya mambo nchini Rwanda wakati huu ikijiandaa na uchaguzi mkuu wa rais mwezi ujao, ni mbaya na wanailaumu serikali ya Rais Paul Kagame kuwa inakandamiza wapinzani wake.

Balozi Ndangiza yu tofauti. Anasema hali ya nchi ni shwari na watu wanafanya shughuli zao kwa amani. Nchi imepiga hatua kubwa ya maendeleo na kuna uhuru mpana.

Anasema ile tu kuwepo wanasiasa wanne wanaowania kiti cha urais dhidi ya Rais Kagame na kuanza vizuri kwa kampeni, ni dalili ya kuwepo uhuru na demokrasia.

“Tunatarajia uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Lakini najua watu wanashangaa kusikia nchi iliyokumbwa na mauaji ya kimbari juzi tu, leo inafanya uchaguzi na rais anapingwa na washindani wanne.

“Tumejenga mifumo madhubuti kila eneo. Sasa wapo wanasiasa wanaodhani Rwanda ni ile ya kabla ya 1994 iliyojaa ubaguzi na ukabila. Wanachezea sheria na hawataki kufuata katiba lakini hawataki kuulizwa.

“Haiwezekani, eti sababu tuna uchaguzi basi serikali ifumbe macho iache wanasiasa wasumbue amani yetu. Hii hapana. Lazima tulinde sheria na katiba yetu.

“Pamoja na kufanya uchaguzi, ni muhimu nchi ibaki na amani na watu wake washikamane vizuri vilevile. Serikali ina wajibu wa kikatiba kulinda mafanikio haya,” anasema.

Balozi Ndangiza anasema demokrasia inahitaji amani, umoja na mshikamano kwa watu wake. Tunataka hali hii iimarike ndani ya Rwanda lakini “ienee pia kwa wanachama wenzetu wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.”

Anasema Rwanda imepiga hatua kubwa katika demokrasia na kutaja mafanikio ya kuwapa wanawake nafasi katika vyombo vya maamuzi kama mfano halisi wa uimarishaji wa demokrasia.

Uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi nchini Rwanda umefikia asilimia 56 na bunge lake lina spika mwanamke.

Akigeukia vyombo vya habari na jukumu la kulinda uhuru, amani na umoja kwa watu, Balozi Ndangiza anasema hakika Watanzania na Wanyarwanda wanahitaji habari zinazonufaisha mustakbali wao.

“Ninyi watu wa vyombo vya habari mnatakiwa kuhakikisha mnatenda haki katika kazi yenu. Msimuonee mtu wala nchi zetu zilizoamua kushirikiana. Msifuate wale wanaodhani hatuna haki ya kuendelea kama wao. Andikeni mlichokitafiti vizuri huku mkitoa nafasi kwa mlalamikiwa kueleza upande wake,” anasema.

Balozi Ndangiza anaeleza waziwazi hofu aliyonayo juu ya jumuiya ya kimataifa kuichukulia Rwanda kirahisi.

Anasema kelele nyingi zinazopigwa kwa Rwanda zinajaribu tu kudhoofisha nchi. “Lazima ufahamu matukio ya uhalifu yameongezeka duniani na ni ishara ya kukua kwa uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu… jumuiya ya kimataifa imeshindwa kudhibiti hili kwani baadhi ya mataifa tajiri yanahusika na uovu huo,” anasema.

0
No votes yet