Banda ashusha thamani ya kwacha


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

BENKI Kuu ya Malawi imekubali kushisha thamani ya fedha za nchi hiyo kwa asilimia 50 ili kuimarisha uhusiano na wahisani.

Kwa muda mrefu Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa likiitaka Malawi kupunguza thamani ya fedha yake iitwayo Kwacha, kwa madai kwamba hatua hii ingeongeza maozo ya bidhaa nje na kupunguza mahitaji ya bidhaa zinazoingizwa hapa nchini.

Lakini, Rais aliyepita, marehemu Bingu wa Mutharika aliyefariki mwezi uliopita alikataa masharti hayo, akisema kupunguza thamani ya shilingi kungeongeza mfumuko wa bei.

Rais mpya wa Malawi, Joyce Banda yuko katika harakati za kutaka kurejesha imani ya wafadhili ili kuvutia tena misaada.

Dola moja ya Marekani hivi sasa imefikia kwacha 250 kutoka 168.

“Hatua za kupunguza thamani ya kwacha na kuliacha soko la fedha liwe huru, zitaendelea kuchukuliwa na serikali katika juhudi zake za kutaka kuafikiana na IMF,” amesema Gavana wa Malawi, Charles Chuka.

Ameongeza kuwa hatua hii bila shaka itafungua milango kwa wafadhili kuendelea kuisaidia Malawi katika miezi michache ijayo.

Hata hivyo, watalaam wa uchumi wamesema hawatarajii kama hatua hiyo itaathiri bei za bidhaa mara moja, kwa kuwa wafanyabiashara wengi walikuwa wakitarajia hatua hiyo kuchukuliwa na tayari wengi wao walikwishaanza kutumia viwango hivyo.

Katika siku za karibuni, Malawi imekabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni baada ya wafadhili kupunguza misaada, na biashara ya tumbaku kuanguka. Tumbaku ndio zao kuu linalouzwa nje.

Hii imesababisha upungufu wa mafuta katika nchi hiyo.

Wiki iliyopita Rais Banda alitanganza kumzuia Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, kuhudhuria mkutano Umoja wa Afrika nchini humo kutokana na tuhuma za makosa ya kivita zinazomkabili kwa sababu za kiuchumi.

Hatua hiyo ilikuwa pia inapingana na msimamo wa mtangulizi wake, Marehemu Mutharika.

Rais huyo pia amemtimua mke wa Mutharika, Callista kwenye kazi yake ya uratibu wa Uzazi Salama, Shirika la Habari la AFP limeripoti.

Joyce Banda ambaye ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais Malawi na wa pili kuwa rais Afrika, anafahamika kwa kupigania haki za wanawake.

Alishika madaraka ya nchi hiyo mwezi uliopita baada ya kifo cha Rais Mutharika (78) aliyefariki akiwa ofisini baada ya kuongoza nchi hiyo tangu mwaka 2004.

Uamuzi wa Mutharika kumteua kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi wa mwaka 2009, ulishtua wananchi wengi wa Malawi, hasa wahafidhina, waliotawaliwa na mfumo dume – ambao hakuwahi kuwa makamu wa rais mwanamke.

Vile vile, mshangao mkubwa zaidi ulikuwa pale Banda alipomkatalia Rais Mutharika wake katika mipango yake ya kutaka kaka yake, Peter Mutharika ndiye awe rais wa Malawi baada ya yeye kumaliza kipindi chake.

Kutokana na hatua hiyo, Banda alitimuliwa kwenye chama tawala, Democratic Progressive Party, na hivyo kujiweka katika wakati mgumu wa kushambuliwa na kukejeliwa katika mikutano ya hadhara na vyombo vya habari vya umma kila siku.

Kigogo mmoja wa chama tawala cha Malawi, aliwahi kusema kuwa nchi hiyo haikuwa tayari kuongozwa na mwanamke.

Naye mke wa rais Muthalika, alisema Banda alikuwa anajidanganya kwamba ni mwanasiasa makini, bali alikuwa tu mchuuzi wa maandazi.

“Inawezekanaje muuza maandazi awe rais,” alihoji mke wa Marehemu Mutharika.

Hata hivyo, Banda alijikuta anakuwa rais kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, baada ya mtangulizi wake kufariki dunia, na hivyo kupata nafasi ya kufanya mageuzi kwa mambo mengi aliyokataa.

0
No votes yet