Bangi haifai, haifai!


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HAKUNA kitu kinachoweza kutosheleza hoja ya baadhi ya wabunge au mtu mwingine yeyote ndani ya nchi, kutaka serikali iruhusu kilimo cha bangi.

Kwamba sasa baadhi ya wabunge wanadhani ni bora serikali iruhusu wananchi wastawishe mashamba ya bangi, hatukufikiria hata mara moja kuwa itakuwa ni pendekezo linalotoka kwa watunga sheria.

Miaka ya nyuma, yalikuwepo maoni ya watu tofauti kutaka serikali ihalalishe utengenezaji na uuzaji wa gongo kwa kisingizio kuwa Watanzania wengi wamekua kwa fedha zilizotokana na biashara hiyo.

Hilo halijapata nguvu ndipo mpaka leo ni marufuku biashara hiyo.

Lakini, wabunge wawili, Abbas Mtemvu (Temeke, mkoani Dar es Salaam) na Mustafa Akunay (Mbulu, mkoani Manyara) wamependekeza sheria inayokataza kilimo cha bangi, irekebishwe ili kilimo na biashara ya bangi iwe halali.

Wanashauri serikali itoe vibali kwa wakulima kusafirisha bangi kwenye nchi ambazo biashara hiyo imehalalishwa kisheria, ingawa hawataji hata nchi moja ambako kilimo cha bangi na biashara yake ni ruhusa.

Sababu waliyoitoa ni kwamba kilimo hicho kikiruhusiwa – badala ya hali iliyopo sasa ya wanaoshiriki kusakamwa na vyombo vya dola – kitachochea kipato zaidi kwa wakulima.

Inafahamika wazi bangi ni zao lililopigwa marufuku dunia nzima kwa kuwa matumizi yake husababisha athari za kiafya kwa mwanadamu. Bangi ni ulevi hatari kama ulivyo ule wa madawa ya kulevya.

Hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa mtumiaji wa bangi anapata uwezo wa kufikiri zaidi, kutenda zaidi au kutambua zaidi majukumu yake. Kinyume chake watumiaji wamekuwa wakidhoofika na mwishowe baadhi yao huishia hospitali za wagonjwa wa akili.

Uzoefu unaonyesha namna gani watumiaji wa bangi wanavyochanganyikiwa baada ya kuzoea kama vile wanavyoathirika kiafya watumiaji wa madawa ya kulevya.

Tofauti na sigara, ambayo yenyewe ni hatari kwa matumizi ya muda mrefu, bangi inalewesha na mvutaji hupata mchemko wa ajabu akishatumia.

Si busara hata chembe kuruhusu bangi ilimwe na kuuzwa na tunahimiza vita dhidi ya ustawishaji zao hili viendelee kwa nguvu.

Laiti wale wabunge wanaowakilisha maeneo yaliyo maarufu kwa kilimo cha bangi, wangewajibika ipasavyo, tusingesikia hata siku moja baadhi ya wilaya nchini zinakabiliwa na njaa.

Tunatoa indhari kwamba wabunge wahimize kilimo cha mazao ya chakula ili kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa chakula na mazao ya biashara kwa ajili ya kuongeza tija kwa uchumi wa nchi.

0
No votes yet