Baraza jipya la Mawaziri hiloo


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version
Rais Kikwete akitangaza Ikulu

RAIS Jakaya Kikwete ana orodha mpya ya baraza lake la mawaziri kiganjani, MwanaHALISI limeelezwa.

“Anaweza kuwataja wakati wowote. Mara hii idadi ya wanawake itakuwa kubwa kuliko ilivyokuwa katika baraza lililopita,” ameeleza mtoa taarifa.

Kutangazwa kwa mawaziri wapya kunatarajiwa kutanguliwa na tendo la rais la kufukuza au kubariki kujiuzulu kwa mawaziri wanane wa sasa wanaotuhumiwa ufisadi.

Hatua ya rais kubariki kujiuzulu au kuwafukuza mwenyewe mawaziri wake, itamwondolea mzigo mzito wa kuteua waziri mkuu mpya.

Taarifa za awali zilieleza juzi Jumatatu kuwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatishia kuachia ngazi iwapo rais atabakiza hata waziri mmoja miongoni mwa wanaoshinikizwa kujiuzulu.

Mawaziri ambao Pinda anaungana na wabunge kutaka wajiuzulu ni Mustafa Mkulo (Fedha na Uchumi); Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Wengine ni, Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii); Omari Nundu (Uchukuzi); George Mkuchika (TAMISEMI); Prof. Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika); Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii).

“Hapa ndugu yangu, rais yuko njiapanda. Waziri mkuu ‘ameapa’ kuwa hatakubali kuendelea na wadhifa wake iwapo bwana mkubwa (Rais Kikwete) atabakiza hata waziri mmoja miongoni mwa wanane wanaoshinikizwa kujiuzulu,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili.

Amesema, “Hii ina maana kwamba rais atalazimika sasa kufanya mabadiliko makubwa ya baraza lake la mawaziri, kinyume na matakwa yake ya awali ya kutaka kufanya mabadiliko madogo.”

Anasema, “Iwapo ataendelea na msimamo wake wa kutaka baadhi ya mawaziri wabaki, itamlazimu sasa kutafuta waziri mkuu mpya kwa kuwa huyu aliyepo hatakubali kubaki kwenye nafasi yake.”

Pinda alipotafutwa na MwanaHALISI kuzungumzia taarifa hizi hakupatikana kwa kuwa simu yake ilikuwa imezimwa.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku tatu baada ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na taarifa inayodai kuwa chama hicho kimeridhia uamuzi wa rais kufanya “mabadiliko makubwa” kwa baraza la mawaziri.

Hata hivyo, taarifa ya chama hicho inatofautiana na kile kinachoelezwa kwa siri na baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya chama na serikali.

Imeelezwa kuwa rais hakutaka kufanya mabadiliko makubwa, isipokuwa sasa atalazimika kuyafanya kutokana na shinikizo la Pinda na baadhi ya makundi ndani ya chama chake.

“Hata mle ndani ya CC, rais alitamka wazi kuwa ‘si wote wenye makosa.’ Lakini inaonekana wenzake wameamua kumzunguka kwa kutoa taarifa tofauti… ya kushinikiza kuwapo mabadiliko makubwa ya baraza,” anaeleza mmoja wa viongozi wa juu serikalini.

Anasema, “Hili linamweka rais katika wakati mgumu zaidi, hasa ukitilia maanani tayari waziri wake mkuu ana mtazamo tofauti.”

Tuhuma kubwa zinazowakabili baadhi ya mawaziri ni kushirikiana na watendaji serikalini kufisidi taifa; matumizi mabaya ya madaraka na ukiukaji maadili ya uongozi wa umma kwa kujilimbikizia mali kwa njia zisizohalali.

MwanaHALISI limeelezwa iwapo rais atashindwa kutekeleza sharti la waziri mkuu, la mawaziri wanane kuachia ngazi, basi atalazimika kuteua waziri mkuu mpya, jambo ambalo limeelezwa kuwa gumu wakati huu.

“Unajua kuteua waziri mkuu mpya ni kuongeza gharama kwa serikali na wananchi. Maana huyu atahesabika kama mstaafu na atalipwa kama waziri mkuu mstaafu,” ameeleza mtoa taarifa.

Amesema katika hali hiyo, rais atalazimika kuitisha Bunge kwa dharura ili kuidhinisha mteule wake mpya.

Kwa mujibu wa Ibara 55(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, mawaziri watateuliwa na rais baada ya kushauriana na waziri mkuu.

Rais pia, kwa mujibu wa Ibara 55(2) anaweza, baada ya kushauriana na waziri mkuu, kuteua naibu mawaziri.

Mtoa taarifa anasema uamuzi wa kuvunja baraza zima la mawaziri na kuteua waziri mkuu mpya, unaweza kuleta kasheshe ya mteule wa rais kukataliwa na wabunge.

Mkutano wa Saba wa Bunge ulimalizika wiki iliyopita mjini Dodoma huku wabunge wakijiorodhesha kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu kwa madai kuwa ameshindwa kudhibiti mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Tangu harakati hizo za kumfukuza, Pinda amekuwa miongoni mwa washawishi wakuu wa kutaka mawaziri waachie ngazi.

Ndani ya kikao cha CC, taarifa zinasema Rais Kikwete hakutaka kabisa kuzungumzia kuyumba kwa serikali yake na minyukano iliyotokea bungeni.

Inaelezwa rais alikuwa na shauku ya kutaka kufahamu kilichotokea kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Arumeru, ambapo chama chake kilishindwa.

Lakini alikuwa waziri mkuu Pinda aliyeibua hoja ya kufukuzwa mawaziri ndani ya kikao kwa kuanza kuelezea kilichotokea bungeni.

Mtoa taarifa anasema Pinda, akiongea kwa ukakamavu, alitahadharisha wajumbe kuwa masuala yaliyotokea bungeni yanapaswa kushughulikiwa haraka kabla “mambo kuharibika.”

Pinda amenukuliwa akimwambia Rais Kikwete kuwa mambo aliyosikia yametokea bungeni, ni makubwa na hivyo ni muhimu kuchukua hatua, tena mara moja.

Kabla Pinda kuweka msisitizo huo, Rais Kikwete alinukuliwa akieleza kikao, “…hili nalo mnataka lijadiliwe? Haya, lakini kila mmoja kati ya wale ana mambo yake…kama mnataka tujadili, haya tujadili.”

Inasemekana katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Kikwete hakutaja kamwe hali tete ya mawaziri wake kama ilivyodhihirika ndani ya bunge.

Naye mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM amemwambia mwandishi wa gazeti hili, “…hakuna namna ya rais kukwepa kuwatema mawaziri wote waliotajwa kwa tuhuma mbalimbali ili kumpa nafasi ya kujenga upya serikali yake.”

Amesema, “Hapana shaka kuwa lile tamko la CC alilosoma katibu mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, limeakisi ukweli kwamba wapo mawaziri ambao mwenendo wao wa kazi hauridhishi na wanapaswa kuondolewa…”

Baadhi ya watoa taarifa wanasema kuwa mtazamo wa chama umekuwa tofauti kidogo na ule wa rais kutokana na suala la utendaji wa mawaziri kutokuwa kati ya vipaumbele vyake.

Kuhusu mgawanyiko ndani ya CCM, vyanzo vya taarifa vimesema msuguano uliojitokeza ndani ya kikao cha kamati ya wabunge wa CCM kilichoketi mjini Dodoma, chini ya waziri mkuu Pinda, ni uthibitisho kuwa wapo wenye mtizamo wa Kikwete.

Makala ya mwandishi Kondo Tutindaga katika toleo hili uk. 7, inafanya majumuisho kuwa mawaziri wameangusha uchumi, meli, reli, kilimo, nishati na huduma za afya, “na bado wanakataa kujiuzulu.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: