Baraza jipya ni mzigo mpya


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

WALIOTEULIWA kuwa mawaziri wameapishwa. Ni vigumu kukiri kuwa hili ni baraza jipya. Kuongezwa wapya wanne au watano katika kundi la wakuukuu 50 hakuwezi kuwafanya wale wakuukuu kuwa wapya.

Wanabaki na ukuukuu wao. Upya katika hilo uko wapi? Jipya ni ukubwa wake. Rais Jakaya Kikwete alipounda kwa mara ya kwanza mwaka 2006 lilikuwa na mawaziri 61. Alipopigiwa kelele mwaka 2008 baada ya serikali yake kuvunjika bungeni, alipunguza hadi 51.

Mwaka 2010 Rais Kikwete aliunda Baraza la Mawaziri 51, lakini aliposhinikizwa, wiki iliyopita ameongeza hadi 55. Huu ndio upya uliopo.

Rais Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa shinikizo. Haikuwa hiari yake. Walishinikiza aunde upya baraza lake. Kwa kuwakomoa akatengeneza baraza kubwa kuliko la mwanzo. Uzito wa mzigo huu utaongezeka juu ya vichwa vya wananchi walipakodi.

Kuomba ridhaa ya kamati kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilikuwa njia ya kujitoa katika lawama kwa watakaoathirika na mabadiliko hayo. Huu ni ushahidi wa ‘wenzangu’.

Ndiyo maana haikushangaza kuona watu waliokutwa na masanduku yaliyojazwa mali isiyojulikana wakiyalinda kwa silaha za kivita hawajashughuliwa hadi leo! Hivi kwa nini tunawalazimisha wananchi watufikirie kuwa tu sehemu ya uchafu huo? Huko kwenye mazao, mbolea itapona kweli? Mchezo wa uporaji ukiendelezwa kilimo si kitakufa! Ukishawaua wakulima nchi inabaki vipi?

Haya ndiyo mambo yaliyowafanya wengine wasiwe na hamu hata ya kumsikiliza Rais Kikwete akitaja majina ya mawaziri wake. Hawakutegemea kitu kipya.

Baada ya kulisikia baraza tulipata wasaa wa kucheka kicheko kile cha marehemu mama yangu. Waliokuwa wanatusikia bila kutuangalia usoni walidhani tunacheka kweli. Tulikuwa tunajutia!

Mvua iliyonyesha tarehe 11 Aprili 2012 ilikuwa kubwa na mafuriko yake yaliacha madhara makubwa kwa wananchi wengi waishio maeneo ya Mbagala. Ukuta wa nyumba yangu ambao ulikuwa unashikana na bafu na choo ulianguka. Fikiria familia yako haina choo utakuwa na muda wa kumfikiria mtu atangaze mawaziri wake?

Ndugu yangu mmoja kwa kunihurumia akanishauri nikajiandikishe kwenye serikali ya mtaa. Nilicheka tena, kwa uchungu. Watu wamelipuliwa na mabomu ya Jeshi la Serikali 29 Aprili 2009 na 16 Februari 2011 mpaka leo bado wanaishi kwenye mahema, serikali haiwajali.

Kama hao walioathiriwa na mabomu ya serikali, mpaka leo wanapata shida, itatujali sisi ambao tumeathiriwa na mvua ambayo siyo ya serikali? Kuthibitisha hayo nenda kashuhudie tabu wanayopata waliohamishiwa eneo la Mabwepande. Wametelekezwa.

Kabla ya kuvunja baraza la mawaziri kutokana na kashfa ya Richmond, Lucas Siyame alikuwa naibu waziri wa maafa katika ofisi ya Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Upareni yalitokea maporomoko ya ardhi usiku wa manane, watu walifukiwa hai kwenye nyumba zao wakafa kwa makumi. Na sehemu zote ambako watu walikumbwa na maafa Lowassa alimtuma Siyame kwenda kushughulikia waathirika, kuwafariji. Wote wawili sasa hawako tena serikalini, msaada wetu utatoka wapi?

Hivi karibuni nilisoma mahali kuwa Sh. 4.6 milioni zimepelekwa wilaya ya Temeke kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya Mbagala. Nilipomuuliza mwenyekiti wa mtaa wangu akasema hajui lolote pamoja na kwamba alishatuorodhesha majina wote tulioathirika.

Chuki ilinijaa nilipopewa hati ya serikali iliyonitaka nilipe kodi ya jengo hilohilo lililoanguka. Bado watu walitaka nikae nisikilize majina ya watu wanaokuwa mawaziri, wanisaidie kipi?

Wabunge wanaopayuka bungeni wakionyesha uchungu katika luninga na kumbe moyoni hawana wajue wananchi wamewashtukia. Asiyeamini asome ujumbe huu:

“Mwalimu wangu! Hapa Geita hali si njema kwa mbunge, alikuwa mzomeaji bungeni, sasa hivi wananchi ndiyo tunamzomea kama si kumkimbiza kama nyau!”

“Shalomu. Imeandikwa ‘usimnyang’anye maskini kwa kuwa ni maskini; wala usimdhulumu mtu mnyonge; kwa sababu BWANA atawatetea’. Nimekuwa nikifuatilia mwenendo wa Bunge la sasa, wabunge wetu (CCM) wanaonekana kucharuka na kuwatetea wananchi kwa sasa, wanafiki wakubwa! Walikuwa wapi siku zote? Au baada ya kuona wanakaribia kunyang’anywa tonge mdomoni ndiyo wanakumbuka shuka wakati kumekucha! Maana wamedhulumu haki ya Watanzania wanyonge kitambo sasa.”

Wote wameuliza ni wangapi walioonekana katika luninga wakipiga kelele? Je, walitia saini zao kwenye karatasi ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu?

Wanasema wabunge wa CCM waliotia saini zao, wabarikiwe sana. Waliokaa kimya Mwenyezi Mungu awanyamazishe kwa amani, lakini waliokemea kwa midomo yao halafu wasitie saini zao wamewekwa kwenye kapu moja na wanafiki.

Dawa ya watu wanafiki ikichemshwa kila mtu atanywea jimboni kwake! Namwomba Mungu atuepushe na mvua za mawe tunazoziita kwa unafiki wetu!

Wanaotaka niseme lolote juu ya baraza hili warejee makala iliyotangulia. Niseme, niseme nini! Ambao hawakuisoma makala ya wiki iliyopita kuna sehemu niliandika hivi:

“Tatizo hapa siyo mawaziri wezi. Wezi wapo kila mahali hata katika hao wapya watakaoteuliwa wezi watakuwapo. Tatizo ni nchi kukosa kiongozi wa kusimamia mawaziri wezi ili wasiibe.”

Kama tatizo ni kukosekana kiongozi wa kuwadhibiti mawaziri wasio waadilifu dawa yake si kuvunja baraza la mawaziri na kuunda jingine! Dawa ni kumpata kiongozi atakayeweza kuwadhibiti mawaziri wasio waadilifu.

Dawa ni kumpata kiongozi mwenye ujasiri na uwezo wa kuwafikisha katika vyombo vya sheria viongozi wote wanaotuhumiwa.

Kiongozi mwenye dhamana akishindwa kufanya hivyo anaonyesha udhaifu au ushirika wake katika kadhia hiyo.

Kwa baraza hili la mawaziri  Watanzania wanapaswa watambue ukubwa wa dhambi waliyoitenda wale waliowaficha ukweli mwingine. Tuna miaka mitatu ya kwenda na hawa watu, kama kasi ya ubadhilifu ni kubwa kiasi hiki, hii nchi itabakiwa na kitu gani kufikia mwaka 2015?

Na kwa sababu hiyo, walioua Azimio la Arusha, wakafuta maadili na kuitupa miiko ya uongozi, wana dhambi kubwa zaidi! Ole wao watu hao! Wanapaswa kuelewa kuwa siku hazigandi!

Watanzania, huu si wakati tena wa kulalamika. Lazima mjikomboe wenyewe! Wadaini viongozi wenu Azimio la Arusha kama mlivyowadai katiba mpya. wote Wanaokuja kwenu wakidai wanataka kuwakomboa waambieni waje na ahadi ya Azimio la Arusha.

Nguvu ya Umma ikidai Azimio la Arusha, wa kukataa nani? Wanaokuja kwenu kwa jina la waheshimiwa hawawafai, kaeni mbali nao! Wakati wa kupeana maneno matupu umepita. “Saa ya ukombozi ni sasa,” alisema Mtikila.

0713 334239
0
No votes yet