Baraza la Wawakilishi laandika historia


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

BARAZA la Wawakilishi la Zanzibar (BWZ), chombo mahsusi cha kutunga sheria, limefanya maamuzi yanayoandika historia mpya.

Tofauti na lilivyofanya pale ulipoibuka mjadala wa nafasi ya Zanzibar katika Muungano, safari hii Baraza limekuja na maamuzi yanayolenga kupatikana ufumbuzi wa moja ya kero kubwa za Muungano.

Baraza limeekeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuchukua hatua tatu baada ya kuwa limejadili Taarifa ya Serikali kuhusu mapendekezo ya uendeshaji kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.

Muungano wa Tanzania, unafikia umri wa miaka 45 hapo 26 Aprili mwaka huu, ulipatikana baada ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuunganishwa 26 Aprili 1964 na Mkataba wa Makubaliano ya Muungano wenyewe, ulihusisha mambo 11 tu. 

Kwanza, serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa kazi ya usimamizi, udhibiti na uendeshaji shughuli zote zinazohusu utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia inakuwa ya Zanzibar pekee.

Pili, Baraza limetaka serikali ianzishe chombo cha kusimamia shughuli zote za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na mambo mengine yanayoambatana nayo. Chombo hiki ni mfano wa Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) lakini kitakuwa na mamlaka yake kwa shughuli hizo zinapofanywa ndani ya ardhi ya Zanzibar.

Tatu, serikali imetakiwa kuhakikisha eneo lote la Bahari Kuu inayohusisha maeneo ya Zanzibar, linashughulikiwa na SMZ, ambayo ndiyo itakayonufaika na mapato yatokanayo na shughuli zitakazoendeshwa katika maeneo hayo.

Wakati maamuzi ya Baraza kuhusu mambo mawili ya kwanza yaliridhia mapendekezo ya serikali, maamuzi ya suala la tatu yalikuja baada ya Baraza kukataa pendekezo la serikali la kutaka uchangiaji gharama za uendeshaji shughuli za kiuchumi – na mgawano wa mapato yatokanayo – kwenye maeneo ya maji ya ndani ya Zanzibar uwe wa ushirikiano kati ya SMZ na Serikali ya Muungano.

Hatua hii imekuja baada ya mjadala mzito uliotokea kuhusu mapendekezo yaliyowasilishwa na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid, tarehe 3 Aprili 2009.

Mapendekezo hayo ni muendelezo wa uchambuaji mapendekezo ya Mshauri Mwelekezi aliyepewa kazi ya kutafiti na hatimaye kushauri serikali mbili katika Jamhuri ya Muungano, juu ya namna bora ya kugawana mapato yatokanayo na raslimali ya mafuta na gesi asilia itakayopatikana Zanzibar.

 Wataalamu waliopewa kazi hiyo ni kampuni ya AUPEC ya Uingereza. Mkataba wa kuwezesha kufanyika kwa kazi hiyo ulifikiwa mapema mwaka 2007 na kazi rasmi ilianza 20 Juni 2007.

Hatua ya kutuma kampuni ya ushauri ililazimu baada ya kutokea mtafaruku pale Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipozuia kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ndani ya maji ya Zanzibar mwaka 1997.

Hatua hiyo ilifuatia kitendo cha Serikali ya Muungano, kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kusaini mkataba na kampuni ya ANTRIM Resources ya Canada kufanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi asilia upande wa Zanzibar 29 Januari 1997.

Tangu hapo, kumekuwa na majadiliano kati ya serikali mbili kuhusu jambo hilo na ndipo ilipokubaliwa kwamba suala hilo liingizwe katika orodha ya mambo yanayojadiliwa katika kile kinachoitwa “Kero za Muungano.”

Uteuzi wa wataalamu washauri ni hatua iliyoridhiwa na pande zote mbili. Na kinachofanyika ni muendelezo wa majadiliano ya ripoti ya awali ya wataalamu hao, baada ya kila upande kujadili ripoti tangulizi.

Mjadala wa kama Zanzibar ni nchi au si nchi ulioibuka mwaka jana, ulileta joto kali kisiasa. Uligusa hisia za Watanzania, lakini zaidi Wazanzibari ambao waliumizwa na kauli aliyoitoa bungeni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba “Zanzibar si nchi bali sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Wazanzibari walijenga nguvu na sauti moja. Na kwa sababu suala hilo lilikuja wakati Baraza la Wawakilishi nalo likiwa kwenye mkutano wake, mjadala wake ulikuwa mzito na ulisukuma wajumbe wote, bila ya kujali vyama wanavyowakilisha barazani.

Kila mjumbe na kila upande walionyesha wazi kutoridhishwa na alichokisema Pinda, ingawa ndivyo isemavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Serikali ilitakiwa tu kueleza msimamo wake kuhusu kauli ya Pinda; haikuwa kama ilivyochukuliwa kwenye suala hili la utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asilia kwani serikali yenyewe ndiyo iliyowasilisha taarifa ambayo baada ya kujadiliwa kumekuja azimio la Baraza linalopaswa kufanyiwa kazi nayo.

Lakini kuonyesha unafiki wa kisiasa, uongozi wa juu wa Serikali ulilivaa suala hilo na kushinikiza maamuzi tofauti na msimamo wa Baraza, kwa maana ya vile wajumbe walivyoazimia.

Alikuwa Spika, Pandu Ameir Kificho aliyeshtua wajumbe aliposema uamuzi wa baraza ni suala hilo kuachiwa wanasheria wa serikali mbili kujadili na kutoa uamuzi unaojali maslahi ya taifa.

 

Hadi leo hakuna uamuzi uliotangazwa baada ya wanasheria wawili kukutana – na kwa hakika inasemekana hakuna kikao walichokaa kwa ajili hiyo – isipokuwa suala hilo lilizimwa na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa bungeni.

Kikwete alisema kwamba hakuna asiyefahamu kuwa “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.” 

Sasa Baraza limetoa maelekezo kwa serikali ambayo utekelezaji wake inasubiriwa. Inatakiwa ifikapo Juni mwaka huu, serikali iwe imeandaa muswada wa sheria ya kuanzisha shirika la maendeleo ya mafuta la Zanzibar; labda ZPDC.

Azimio la Baraza la Wawakilishi linafungua ukurasa mpya wa kutoa malalamiko ya Zanzibar kuhusu mfumo mbaya wa uendeshaji Muungano ambao siyo tu unaongeza mgogoro, bali pia unaumiza maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar, ambayo kulingana na Katiba, ni jukumu la Zanzibar yenyewe. 

Zanzibar imekuwa ikilalamika kutonufaika na mapato yatokanayo na maliasili zake wakati Tanzania Bara ina madini mengi inayonufaika nayo peke yake.

Ni msimamo wake kwamba japokuwa utafutaji na uchimbaji mafuta ni miongoni mwa mambo ya Muungano yaliyoongezwa baada ya orodha ya kwanza, utekelezaji wa shughuli hizo hauwezi kufanyika bila ya kuguswa sheria za ardhi ambazo si suala la Muungano.

Lakini pia SMZ inasema TPDC lililoanzishwa kwa sheria ya Bunge, haliwakilishi maslahi ya Zanzibar na haina uwakilishi wenye uwiano kwani ni ofisa mmoja tu kutoka Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi ya SMZ anayeshiriki vikao vya maamuzi.

Zanzibar inaamini muungano umeziba fursa zake nyingi za kuendelea kiuchumi kutokana na mfumo mbaya wa muungano ambao kwa upande mwingine, umechochea uchumi imara Tanzania Bara.

Mfano wa serikali ya Muungano kusimamia shughuli za utafiti na uchimbaji mafuta na gesi asilia, bila ya kuishirikisha SMZ – huku ikinufika na mapato kutokana na usajili wa meli na kodi tozwa – unathibitisha malalamiko hayo.

0
No votes yet