Baraza la Wawakilishi laingia doa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Spika Pandu Ameir Kificho

BARAZA la Wawakilishi, chombo cha kutunga sheria Zanzibar linapita katika kipindi kigumu, pengine zaidi kuliko wakati wowote ule tangu lilipoanzishwa mwaka 1980.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Baraza la Wawakilishi lina majukumu mazito ya uwakilishi, kutunga sheria na kusimamia serikali.

Lakini matukio matatu yanatosha kuthibitisha mchoko wa baraza na doa lililopata. Kwanza, ni pale Baraza lilipotumwa kuchunguza kashfa nzito ya biashara ya magendo ya karafuu.

Pili, pale ulipokuja mjadala wa mchele mbovu ulioingizwa nchini. Tatu, pale ulipokuja mjadala wa iwapo Zanzibar ni nchi au vinginevyo.

Baraza lilikuja na ripoti nzuri iliyofichua uovu wa biashara ya magendo inayofanywa katika karafuu; zao ambalo bado lina nguvu kubwa katika mchango wake kwa pato la taifa.

Ali Juma Shamhuna, mwakilishi wa Donge, aliongoza Kamati Teule ya Baraza kuchunguza kashfa hiyo na kuja na taarifa nyeti.

Kamati iligundua kuhusika kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika biashara hiyo.

Kitu cha kusikitisha ni kwamba hakuna hatua za wazi ambazo leo serikali inaweza kujinasibu kuwa ilizichukua dhidi ya viongozi walioguswa.

Kibaya zaidi, baadhi ya waliotuhumiwa na  kuthibitika kuhusika, walibadilishwa tu vyeo na kupangiwa kazi nyingine, tena wengine kwenye taasisi nyeti.

Ndio kusema ufisadi uliofanywa na viongozi hao haukuwarudia wenyewe. Hakuna mashitaka waliyofunguliwa wala hakuna fidia yoyote waliyolipishwa ili iwe fidia kwa serikali kwa vile ilikosa mapato makubwa yaliyoingia mifukoni mwa viongozi binafsi.

Ukweli ni kwamba karafuu waliyouza viongozi hawa ilikuwa iuzwe na serikali na mapato yake yangeingia katika mfuko wa serikali. Haikuwa hivyo na hakuna manufaa ambayo serikali ilipata.

Sasa tuangalie upande wa pili. Wajumbe  walipojadili tukio la kuingizwa mchele mbovu nchini na mfanyabiashara mwenyeji, walifanya kazi nzuri na ya kupigiwa mfano.

Lakini kilichofuatis ilikuwa, na bado ni, aibu tupu. Serikali ilipitisha mikono yake mpaka kuhakikisha hakuna kamati ya baraza itakayochunguza suala hilo.

Na kweli, haikuundwa kama wakubwa walivyotaka. Badala yake walitishia wajumbe wachache wa CCM walioungana na Kambi ya Upinzani kulalamikia mchele huo na kutaka iundwe kamati kuchunguza.

Serikali iliitisha kikao cha dharura cha wajumbe wote wanaotoka CCM na kutoa matamshi makali dhidi yao . Tunakumbuka kikao hiki kilifanyika Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui, kikiongozwa na Rais Amani Abeid Karume.

Wana CCM waliambiwa kwamba waache kuungana na upinzani kuishambulia au kuiadhiri serikali ya chama chao. Ati waliambiwa wanakokwenda ni kuonyesha wanavyosaliti chama chao.

Hapa tunaona namna maslahi binafsi yalivyo muhimu kwao. Hakuna aliyeshtuka kwa yale yaliyoamuliwa na serikali baada ya kujibebesha dhamana ya kujichunguza.

Kosa lilifanywa na maofisa wa serikali, watuhumiwa ni pamoja na viongozi serikalini na maswahiba wao nje ya serikali; bado serikali ikajipiga kifua na kulazimisha kujichunguza.

Hii ni kama kesi ya Msomali; jaji kuwa Msomali, mwendesha mashtaka Msomali na wazee wa Baraza la Mahakama pia Wasomali. Ni hukumu gani itatoka? Je, staili hii ya utendaji wa SMZ itachukuliwa na serikali kwamba imestawisha utawala bora?

Mjadala wa “Zanzibar nchi au la” ulikuwa mzuri katika mtazamo wa kutatua tatizo sugu katika Jamhuri ya Muungano. Wananchi waliacha itikadi zao na kuanza kufuatilia michango ya wawakilishi kupitia vyombo vya habari vya serikali – Televisheni (TvZ), Redio (STZ) na gazeti ( Zanzibar Leo).

Kwa muda mrefu sasa Wazanzibari hawajawahi kupata fursa ya kusahao itikadi zao za kisiasa na kusikiliza majadiliano ya Baraza la Wawakilishi kupitia vyombo vya habari. Hii ni kwa kuwa vyombo hivi huonekana kupendelea serikali na CCM.

Na ilipofika hatua muhimu ya kutoa uamuzi, kila kitu kiliharibika. Zile nguvu zilizotiwa katika kujadili na kushauri hatua za kuchukuliwa, ziliyeyuka. Kama vile serikali iliogopa matokeo yake; ilijitahidi na ikafanikiwa kuteka nyara maamuzi ya wajumbe na kupenyeza yake.

Hili lilitendeka kupitia Spika, Pandu Ameir Kificho. Alipofika kwenye kiti chake, wakati akitarajiwa kueleza maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya Baraza – inayojumuisha wajumbe wa CCM na wa upinzani – alitoa mawazo yake.

Ilionyesha kabisa aliingia na maelekezo mengine kutoka kwa anaowajua. Nguvu za Baraza la Wawakilishi ziliuawa; mamlaka ya chombo hiki yalibezwa; matumaini ya wananchi yalikandamizwa; maendeleo ya watu na nchi yao yalidharauliwa.

Unapojadili kwa upana halafu ukaja na uamuzi finyu, unaonyesha ulivyochoka. Ndivyo ilivyotokea. Akili za watu muhimu zilichoka ghafla. Sasa baraza linaonyesha halina meno; halina ukali na ujasiri tena.

Baraza limeonyesha si taasisi ya kutegemea wala kutegemewa. Kumbe maamuzi na mawazo yake ni fadhila si mahitaji ya kweli ya kikatiba yanayopaswa kuaminika na kuheshimiwa.

Oktoba hii hapa. Serikali iliahidi kutoa maelezo juu ya Zanzibar kuwa nchi au la. Lakini inaonekana kuna wale ambao tayari wamesahau kuwa Rais Jakaya Kikwete keshalifunga hili.

Nani tena baada ya Kikwete kusema anaweza kurudisha hoja mezani? Tutambue likiletwa, itabidi kuwe na mjadala. Upi sasa wakati Rais keshasema? Hiyo ndiyo hofu yangu na wengine wanaotazama mambo kwa mapana yake.

0
No votes yet