Barua ya wazi kwa Rais Jakaya Kikwete


Mbwana Muungwana's picture

Na Mbwana Muungwana - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version

Mheshimiwa Rais,

Kwa heshima kubwa napenda kukutarifu kuwa hali ya kampuni ya simu Tanzania (TTCL) ni mbaya. Hii ni kwa sababu waendeshaji wapya kampuni ya SAKATEL kutoka CANADA kwa makusudi wameamua kuihujumu kampuni yetu.

Historia ya kuifisidi TTCL ilianza mwaka 1999 baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu kuanza mchakato wa kuuza asilimia 35 ya hisa za TTCL kwa wawekezaji wa nje.

Hatimaye serikali iliuza hisa zake kwa  kampuni za MSI na DETACON kwa thamani ya dola za Kimarekani 120 milioni.

Awali ilidaiwa kuwa wawekezaji walionunua TTCL walikuwa wanatoka nchini Uholanzi. Kumbe haikuwa hivyo.

Waliojiita wawekezaji walikuwa ni wajanja wachache walioshirikiana na mfanyabiashara mmoja kutoka Sudan Mohammed Said Ibrahim. Hawa ndiyo waliofanya hila kuchukua kampuni yetu ya umma.

Baada ya kukamilisha ujanja huo, wawekezaji DETACON wakaondoka kinyemela na kuiacha TTCL mikononi mwa MSI feki.

Muda mfupi baadae, wakahujumu hesabu na kutoa taarifa za kupotosha kwamba TTLC ilikuwa inaendeshwa kwa hasara na hivyo MSI haiwezi kununua hisa za TTLC kwa bei ya awali waliokubaliana na seikali.

Mheshimiwa rais, kuanzia hapo TTCL ikawa inaliwa Sh. 600 million kila mwezi na MSI feki. Fedha hizo zimeliwa kwa miaka minne na hatimae ikaimarishwa kampuni ya simu za mkononi ya CELLTEL.

Baada ya kukamilika CELLTEL, Mohammed Ibrahim akauza kampuni yake kwa mfanyabiashara mwenzake kwa Kuwait na kubadilshwa jina na kuitwa Celtel International (sasa ZAIN).

Wakati utawala wakp ulipoingia madarakani, ulitafuta mwendeshaji mwingione wa kuongoza TTCL kutokana na makubaliano yaliokuwapo kati ya serikali na CELTEL International.

Katika mchakato huo ikapatikana kampuni ya SASKATEL kutoka Canada. Serikali ikadhani kwamba imetatua tatizo la TTCL, kumbe hata hao walioletwa walikuwa feki kama ilivyokuwa MSI.

Mheshimiwa Rais, kinachofanywa sasa na SAKATEL ni kuihujumu TTCL kwa lengo la kuijenga kampuni mpya ya HITS ambayo inasemekana kuwa inamilikiwa na baadhi ya vigogo.

Miongoni mwa hujuma za moja kwa moja zinazofanywa na SASKATEL ni kusimamisha matangazo yote ya biashara, kusitisha kutafuta wateja wapya (Marketing) na kusimamisha ununuzi wa vipuli vya mitambo ya TTCL.

Nyingine ni kuhamisha mkakati wa biashara (Business Plan ya TTCL) ya TTCL ambayo iliyotengenezwa na wazalendo kupelekwa HITS.

vilevile, kusitisha uwasilishaji wa michango ya wafanyakazi katika mifuko ya Hifadhi ya jamii NSSF na PPF na kusitisha kupeleka  michango ya wafanyakazi katika chama chao cha Kuweka na Kukopa.

Mheshimiwa Rais,  wanaoitwa waendeshaji wa TTCL wamekusanya madeni ya TTCL yanayofikia Sh. 15 bilioni lakini hazionekani katika Akaunti ya TTCL.

Vilevile wanaojiita wawekezaji wameleta wafanyakazi wa kigeni kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazalendo, huku wakilipwa mamilioni ya fedha kila mwezi.

Hali hii imetuchosha wafanyakazi, lakini tunasita kufanya mgomo kwa sababu tunahofu kwamba utaathiri taifa. Tunakuomba wewe rais uingilie kati.

Katika ujenzi wa taifa,
Mbwana Muungwana,
Kny: Wafanyakazi wa TTCL

0
No votes yet