Barwany: Tunataka maendeleo


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MBUNGE wa Lindi Mjini, Salum Barwany anasema wananchi wa mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara, hawana shida ya kubadilisha vyama.

“Watu wetu wametulia sasa, hawataki kubabaika kwa kuhama vyama. Kiu yao kubwa ni maendeleo ya kweli siyo siasa ya ahadi hewa,” ameliambia MwanaHALISI katika mahojiano maalum yaliyofanyika Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Barwany ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), anasema wananchi hao wametelekezwa kwa miaka mingi; serikali haijawatambua.

Anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali, kinaendeleza ahadi zisizotekelezwa kwa watu wa kusini, wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapeleka siasa za ubabaishaji.

Kauli hizi zimekuja baada ya viongozi wakuu wa CHADEMA kupita mikoa hiyo na mjini Lindi ambako lipo jimbo analoliwakilisha.

Viongozi hao, pamoja ya kupongeza wananchi kwa kuchagua ‘mbunge hodari’ mwaka 2010, waliwasihi safari ijayo wafikirie mara mbili kuchagua CUF.

Walisema CUF imeshikana na CCM hivyo wabunge wake hawana ubavu wa kuibana serikali kuharakisha maendeleo.

Isitoshe, wakamsihi ama ahamie CHADEMA au CCM ambako atatumikia vizuri wananchi.

Hoja hii imemtibua Barwany. Anasema wananchi wa Lindi walitafakari vya kutosha kabla ya kuchagua CUF. Wanataka maendeleo si ahadi.

Barwany, katika uchaguzi mkuu wa 2010, alimshinda kada Mohamed Abdulaziz wa CCM ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa.

Anasema wana Lindi hawataki tena siasa za propaganda; zile ambazo huishia uchaguzi unapofanyika na ukiisha waliotoa ahadi hawaonekani.

“CHADEMA walikuwa wapi siku zote. Wanatokea leo Lindi wakati wananchi wamekuwa katika shida nyingi kwa miaka yote ya serikali ya CCM.

Anakishutumu chama hicho kwa kuidharau mikoa ya kusini kimaendeleo. “Baada ya kuona wametosheka na maeneo miliki yao, leo ndio wanaona umuhimu wa kusini lile ambalo hawakulipatia hata mbunge mmoja wa viti maalum.

“Hawa CHADEMA katika uchaguzi uliopita, walishindwa kusimamisha angalau mgombea mmoja wa udiwani. Hii inatosha kuamini huku Lindi si maeneo yao, ni dharau kwa watu wa kusini,” anasema.

Bali Barwany anashangaa viongozi wa CHADEMA kubeza serikali ya umoja wa kitaifa wakati kwenye kampeni za uchaguzi walinadi kuja kuunda serikali ya pamoja.

Anasema chama hicho kingeangalia uwezekano wa kupata uwakilishi kwenye serikali Zanzibar badala ya kumshauri yeye kuhamia CHADEMA.

Hivi CHADEMA hawajui siasa za zama hizi zinahimiza serikali shirikishi zaidi, kuliko utengano, anahoji Barwany.

Akijibu hoja kwamba CCM na CUF wamefunga ndoa hivyo CUF sasa haiwezi kutumikia vizuri wananchi, Barwany anasema: Tunavyoamini sisi ni kwamba CHADEMA na CCM lao moja katika kuikandamiza CUF hasa Bara.

“Angalia tu CHADEMA inavyoshambulia CCM haishughulikiwi, kinyume na tulivyokuwa CUF wakati ule tukishika kambi ya upinzani.

“Kila siku viongozi wakiswekwa vituo vya polisi wakiwa wamevunjwa mikono. Hatujasahau alivyovunjwa mkono Profesa Lipumba pale Mbagala Zakhem,” anasema.

Anaigeukia serikali akiilaumu kwa kutoa ahadi hewa za maendeleo kwa wananchi wa kusini.

“Tunaahidiwa kama watoto wadogo. Serikali mara tutafanya hili, halifanywi; tutajenga hili, halijengwi. Ni siasa tupu. Sasa tunadanganywa kwa mji wetu wa Lindi kupandishwa kuwa manispaa kutoka halmashauri,” anasema.

Anasema hakuna wataalamu wa kutosha, bajeti haitoshi, mkoa hakuna viwanda vya kupunguza vijana wasio kazi.

Barwany anasema wakati halmashauri imeongezewa kata tano mpya (sasa zipo 18), katika kupandishwa kuwa manispaa, bajeti imebaki ileile Sh. 8 bilioni kwa mwaka.

Anasema wananchi wa Kusini wanapambana wenyewe kupata maendeleo baada ya kusahaulika; hata barabara ya Dar es Salaam hadi Kibiti kwa CCM imekuwa ajenda ya kisiasa kila unapofika uchaguzi.

Analaumu hali hiyo akisema inachangia kukimbiza vijana mikoa hiyo na kuhamia Dar es Salaam kwa matarajio ya maisha mazuri.

“Kitendo cha serikali kudai maisha magumu yapo kila mahali ni cha kupumbaza watu ambao wanajua nchi yao imejaaliwa raslimali nyingi.

“Lindi na Mtwara tuna gesi nyingi lakini kwa sababu ya ukiritimba wa serikali, tunaona bomba likitokea Songosongo hadi Dar es Salaam na sasa kutoka Mnazibay kuipeleka Mombasa, Kenya,” anasema.

Barwany anasema serikali ya CCM itaendelea na deni kwa wananchi wa Lindi na Mtwara, mikoa iliyochangia sana ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

“Raslimali iliyopo kwetu inatumika kujenga mikoa yao. Huu ni ubaguzi, lakini pia ni wizi wa raslimali yetu. Walewale walionufaika wakati wa harakati za ukombozi ndio wananufaika hadi leo,” anasema.

“Inatuhusu nini sisi wazalishaji wa korosho, ufuta, mahindi na muhogo kutwambia dunia nzima imekumbwa na mtikisiko wa uchumi. Je madini yetu na raslimali nyingine zinatumikaje kwa ajili ya maendeleo yetu,” anahoji na kusema:

“Sisi tuna madini, gesi, mafuta, mbao, chumvi, saruji, maua… huu si wakati wa siasa, tunataka raslimali zitumike kujenga mikoa yetu na kubadilisha maisha ya wananchi wetu.”

Anasema wananchi wamethibitisha kuwa CCM haiwezi tena kuongoza, ndio maana “wametuchagua CUF.”

Barwany anachukizwa pia na utamaduni unaoendekezwa na serikali – kugeuza mikoa ya Lindi na Mtwara kama mahali kusikokalika.

“Tunaletewa viongozi waliokataliwa huko, walioshindwa kuleta tija kwingine. Mtumishi anapangiwa kuja kwetu kama adhabu baada ya kuharibu mikoa mingine. Huko ni kufanya kusini jela ya watumishi waovu,” anasema.

Mfumo wa kununua mazao ya wakulima, hasa korosho na ufuta, yanayolimwa sana kusini, nao unatatiza, akisema umeendeleza dhulma kwa wakulima.

Serikali inauita “stakabadhi ghalani.” Ni vyama vya ushirika kununua mazao kwa mkopo na malipo kulipwa kwa awamu.

Anasema mfumo huo haufai kwa wakulima wanaotegemea kilimo cha kujikimu ambacho hakitoi mavuno mengi. Ukimkopa baada ya kuvuna, “atapataje fedha za kupata mahitaji ya kila siku.”

Barwany anasema Rais Jakaya Kikwete aliyeingia madarakani 2005, amesahau kusini licha ya ahadi yake ya kuipa kipaumbele mikoa iliyoachwa nyuma.

Barwany alizaliwa 30 Juni, 1959. Alisoma elimu ya msingi shule ya Mingoyo, Lindi mjini 1968/74 na sekondari ya Mkonge 1976/79.

Mfumo wa vyama vingi uliporudishwa nchini mwaka 1992, alijiunga na NCCR-Mageuzi na kuwa mwenyekiti wa wilaya ya Lindi, kuanzia 1993 hadi 1995.

Mwaka 1996 alihamia Tanzania Labour Party (TLP) na mwaka 1999 akaingia CUF ambako kwa sasa pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: