Bashar Assad: Ole wao watakaoniingilia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Rais Bashar Assad

RAIS wa Syria, Bashar Assad ametoa onyo kali akisema eneo la Mashariki ya Kati linaweza kuwaka moto ikiwa nchi za Magharibi zitaingilia kumaliza machafuko yaliyodumu kwa miezi saba sasa.

Amesema mgogoro unaweza kupanuka na kuwa zaidi ya “Afghanistan 10.”

Kauli hiyo ya Assad iliyomo kwenye gazeti la Sunday Telegraph la Uingereza, ndiyo kali zaidi dhidi ya wazo la kutaka nchi za nje ziingilie machafuko hayo.

Alisema hao wote wanasingizia hali ya usalama wa ndani ili kujenga uwezekano wa kupeleka majeshi ya Magharibi baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya anga ya NATO yaliyosaidia kumwondoa madarakani Rais wa Libya, Muammar Gaddafi.

"Syria sasa ni kiungo katika eneo hili. Hali inatatiza na ukichezea ardhi yake utasababisha tetemeko la ardhi,” alisema Assad katika mahojiano. “Je, mnataka kuona Afghanistan moja au makumi ya Afghanistan?”

Marekani na washirika wake hawajaonesha shauku ya kuingilia mgogoro wa nchi nyingine ya Kiarabu na upinzani nchini Syria haujaomba msaada wa kijeshi kama ilivyokuwa Libya na wao wamekuwa wakipinga nchi za nje kuingilia kati mgogoro huo.

Siku moja baada ya kutoa kauli hiyo, Umoja wa Nchi za Kiarabu umewasilisha mpango wa kumaliza machafuko ya umwagaji damu. Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, ilisema serikali ilitarajiwa kutoa majibu juzi.

Hakukuwa na ufafanuzi juu ya kilichomo katika mpango huo, lakini tangazo hilo limekuja siku chache baada ya umoja huo wenye wanachama 22 kuongeza juhudi za kutatua machafuko yaliyojaa umwagaji damu kwa miezi saba sasa. Wapinzani wa Rais Assad wanataka aondoke.

“Jopo la wanadiplomasia wa umoja huo lilikutana katika kikao cha “wazi na ukweli” pamoja na ujumbe wa Syria nchini Qatar, Jumapili,” alisema Hamad bin Jassim, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar.

Mwanadiplomasia kutoka umoja huo aliyeko makao makuu Misri alisema umoja huo utaandaa kikao kingine leo kujadili mgogoro huo.

Mawaziri watapokea ripoti ya ujumbe uliotumwa Syria na “mpango kazi” alisema ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Machafuko dhidi ya utawala wa Assad yalianza katikati ya Machi lilipoibuka wimbi la upinzani katika nchi za Kiarabu ulioangusha tawala za Tunisia, Misri na Libya. Umoja wa Mataifa unasema majeshi ya serikali ya Assad yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.

0
No votes yet