Batilda, Lema watafutana Arusha


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Batilda Burian, mgombea wa CCM jimbo la Arusha mjini

KINYANGANYIRO cha ubunge katika jimbo la Arusha Mjini, kimepamba moto. Wagombea watano kutoka vyama tofauti wanachuana kuwania nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Felex Mrema (CCM).

Mrema aliyeongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka minane, alishindwa kupenya kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliyemwangusha kigogo huyo wa siasa za Arusha, ni Batilda Burian, waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais (mazingira).

Kati ya wagombea hao watano, mchuano mkali upo kwa wagombea wawili, Godbless Lema – mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Batilda anayewania nafasi hiyo kupitia CCM.

Wagombea wengine watatu, Mc Milian Lyimo aliyejitosa katika kinyang’anyiro hicho kupitia Tanzania Lebour Party (TLP), Mohamed Balawi anayegombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na Joseph Mafatwa wa Demokrasia Makini, wanaonekana kama wasindikizaji.

Tayari msimamizi wa uchaguzi Arusha mjini Rafael Mbunda ameshamwandikia barua Lema kumwonya kwa kile alichodai, “kutumia lugha chafu dhidi ya Batilda.”

Mbunda anasema katika barua yake kuwa Lema alitoa maneno yaliyokatazwa na maadili ya uchaguzi. Hakutaja maneno hayo.

Hata hivyo, kujitosa kwa Lyimo katika kinyang’anyiro hiki kunaweza kumpa ahueni Baltida, ingawa kunaweza kumwangamiza pia.

Kwa mfano, watu ambao hawamtaki Lema wanaweza kumpa kura Batilda.

Lakini Batilda anakabiliwa na kibarua kigumu cha kujieleza mbele ya wananchi kuhusu uzawa wake na kile kinachoitwa, “mahusiano yake na mumewe.”

Wapinzani wa Batilda wanadai kuwa mwanasiasa huyo, si mzaliwa wa mkoa wa Arusha na wala haishi mkoani humo. Wanamwita wakuja.

Wanasema ameolewa Zanzibar na anaishi Zanzibar, na kwamba mumewe Othumani Masoud, ambaye ni mkurugenzi wa mashitaka Zanzibar (DPP), ni mwenyeji wa kisiwa cha Pemba.

Changamoto nyingine ni ule utamaduni wa watu wa Arusha kumweka mwanamke katika nafasi ya pili. Tangu jimbo la Arusha lianzishwe miaka zaidi ya 40 iliyopita, halijawahi kuongozwa na mwanamke.

Wapinzani wa Batilda wanafika mbali zaidi.

Wanasema mgombea huyo wa CCM ameletwa maalum na kundi la watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini ili kufanikisha mkakati wa kundi hilo “kushika dola mwaka 2015.”

Lakini mwenyewe amekana baadhi ya madai hayo. Kwanza, anasema yeye si wakuja kama ambavyo wapinzani wake wa nje na ndani ya chama wanavyosema.

Katika kukabiliana na madai hayo, Batilda ameamua kutembea na mama yake mzazi, Hawa Mairo ambaye inadaiwa kuwa aliwahi kuwania ubunge katika jimbo hilo huko nyuma. Hakufanikiwa kushinda.

Katika baadhi ya mikutano yake aliyoifanya amekuwa akikana kuwa yeye ni wakuja. Anasema amezaliwa mkoani Arusha na kupata elimu yake ya msingi na sekondari mkoani humo.

Pili, Batilda anakana madai kuwa anaishi Zanzibar, ingawa anakiri kwamba ameolewa huko. Anasema anaishi Arusha.

Tatu, Batilda anakiri kuwa mume wake ni Othumani Masoud, mwajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lakini anasema mume wake ndiye huwa anamfuata yeye.

Hata hivyo, utetezi huu mpya umezua mjadala mwingine. Kwamba haiwezekani Othumani kumfuata Batilda Arusha, wakati mume wake huyo ana mke mwingine Zanzibar.

Pamoja na kwamba katika maeneo mengine hoja kwamba Baltida kuolewa Zanzibar inaweza kuwa dhaifu, lakini kwa wenyeji wa mikoa hii ya Kaskazini, hili si jambo la kulipuuza hata kidogo.

Wengi wanaona kuwa hatua yake ya kuolewa Zanzibar, inamwondolea sifa ya kuwa sehemu ya kizazi cha Arusha; kutokana na kuwa na familia Zanzibar alipaswa kubaki Zanzibar na kufanya siasa zake visiwani.

Jingine ambalo wapinzani wake wanamtwisha ni kule kuzunguka katika wizara tano katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Wanasema, mzunguuko huo ni kielelezo cha kushindwa kazi hivyo anabebwa tu.

Hoja nyingine ambayo inaonekana kumtafuna, ni udini. Katika siku za karibuni wametokeza watu wasiofahamika wakipita na kusambaza ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) unaotaka waislamu kumchagua Batilda kwa kuwa ni muislamu mwenzao.

Hata hivyo, Batilda anaonekana kupata nguvu hasa baada ya ushindi wake mkubwa katika kura za maoni.

Tayari mgombea huyo amesimikwa cheo cha kabila la Kimasai anachopewa mwanamke (Leigwanaki), kama dalili za kukubalika na wazee wa kabila hilo. Cheo kama hiki amewahi kupewa waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

Naye Lema anayewania jimbo hilo kwa mara ya pili, baada ya kushindwa kwa mizengwe mwaka 2005, hayuko salama.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka 2005, Lema aligombea kupitia chama cha TLP; alitangazwa kupata kura 47,000 dhidi ya 51,000 za mpinzani wake, Felex Mrema.

Hadi sasa, wengi wanaamini kuwa Lema ndiye aliyeshinda uchaguzi huo, bali CCM walitumia hila kumtangaza Mrema.

Wanasema kabla ya matangazo ya jumla kutolewa, Lema alikuwa amemwacha Mrema mbali. Wanasema alikuwa mbele kwa zaidi ya asilimia 10.

Chanzo cha tuhuma dhidi ya Lema kinatokana na kushindwa kwa uongozi wa TLP kuendesha kesi iliyofunguliwa mahakamani.

Lema anasema kushindwa huko kumetokana na mahakama kutaka chama chake kuweka dhamana ya Sh. 5 milioni kama sheria inavyotaka na Sh. 27 milioni alizotaka kulipwa wakili.

“Tulishindwa kuendesha kesi hii baada ya chama kushindwa kumlipa mwanasheria na kuweka dhamana ya Sh. 5 milioni iliyotakiwa na mahakama,” anaeleza. Anasema wakili wao alitaka kulipwa nusu ya fedha hizo.

Anasema, “Tukaamua kuitisha mkutano wa hadhara ili kuomba fedha kutoka kwa wananchi, lakini mkutano uliohudhuriwa na watu zaidi ya 5,000 ulichanga Sh. 80,000 tu.

Hiyo ndiyo sura nzima ilivyokuwa,” anasema Lema kwa sauti ya masikitiko.

Pamoja na Lema kukana madai hayo, bado wapinzani wake wa kisiasa jimboni humo wanaendelea kumtuhumu kuwa aliuza jimbo.

Bahati mbaya, baadhi ya wanaotuhumu sasa, ni viongozi wa TLP ambao wanaonekana kufunga ndoa na CCM kuhakikisha kuwa Lema hashindi ubunge wa jimbo hilo.

Tuhuma nyingine ambazo wapinzani wake wamekuwa wakimtwisha wakati alipokuwa TLP ni kupigia debe mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Sombetini, Alfonce Mawazo.

Awali Mawazo alikuwa diwani wa TLP. Lakini aliondoka katika chama hicho kutokana na kutoelewana na baadhi ya viongozi wake wa mkoa.

Lema anajitetea kwamba alifanya hivyo si kwa maslahi binafsi, bali ni kutokana na uhusiano wake wa karibu na Mawazo.

Pamoja na hayo bado Lema anaweza kushinda. Katika baadhi ya mikutano yake ya kampeni, ameonyesha umahiri mkubwa wa kujenga hoja na kujibu tuhuma dhidi yake. Wengi wanamwona kuwa ndiye anayestahili kuwa mbunge wa jimbo hili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: