Benjamin Mkapa presha juu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

BAKILI Muluzi, rais wa zamani wa Malawi anakabiliwa na mashitaka 80 ya rushwa na kujipatia mali ya umma visivyo.

Frederick Chiluba, rais wa zamani wa Zambia naye ana wakati mgumu. Anatuhumiwa kuiba mali ya umma huku mkewe, Regina, akiwa ameanza kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kuthibitika amejipatia fedha kwa njia haramu.

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, anaendelea kushika kiti hata baada ya kushindwa uchaguzi. Hofu yake ni kushitakiwa kwa makosa mbalimbali aliyofanya akiwa madarakani.

Achilia mbali tatizo la kuvuruga uchumi, mkewe, Grace, anatuhuma nyingi za matumizi mabaya ya fedha za umma ikiwemo kununua jumba la kifahari ughaibuni.

Pia Grace amekuwa akiishi maisha ya juu kwa kujipamba vito vya bei mbaya. Inadaiwa pia amejengewa jumba la ajabu lenye thamani ya Sh. bilioni tatu.

Fedha zote hizo ni za wananchi na walipakodi. Nchini Zimbabwe kumehanikiza kipindupindu, chanzo kikitajwa kuwa ukosefu wa dawa ya kuulia wadudu waliomo kwenye maji ya kunywa. Uchumi umeanguka kiasi cha kuwepo kiwango cha mfumko wa bei kisichofikirika.

Chiluba kama walivyo marais wengi wa Afrika, aliingia madarakani kama shujaa. Lakini baada ya miaka 10 ya utawala wake, akaamini bado anapendwa na kutaka kubadili katiba ili agombee kipindi cha tatu. Akakwama.

Mwenzake, Muluzi, akiwa ameingia madarakani kama mfanyabiashara aliyetumainiwa kujenga nchi kiuchumi na kijamii, naye akafanya mbinu hizohizo za kutaka kubaki kupitia mabadiliko ya katiba. Akakwama.

Wote walikuwa na kitu walichokuwa wakitafuta: Kuficha madhambi yao katika hali ya kujikinga na uwezekano wa kushitakiwa kwa maovu waliyoyatenda wakati wakiwa Ikulu.

Mugabe kwa bahati nzuri hana kikwazo cha katiba cha kugombea kadri atakavyo. Amekuwa madarakani tangu mwaka 1980 Zimbabwe ilipopata uhuru kwa Waingereza. Lakini kwa namna alivyoendesha nchi, salama yake ni kifo tu.

Amejitahidi kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kubaki madarakani. Uthibitisho ni kauli za wakuu wa vyombo hivyo. Walithubutu kusema hawataruhusu mpinzani kushika madaraka hata wakishinda.

Sasa, wakati haya yakitokezea marais wastaafu wa Afrika, huku walioko madarakani kama Mugabe na hata jirani Yoweri Museveni wa Uganda wakiogopa kustaafu, marais wastaafu Tanzania wanahali gani?

Wapo waandishi mahiri waliosema wazi wanamuomba radhi rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi. Kisa? Alizuliwa mengi; alikejeliwa hata na watu wasiostahili kwa kuwa tu aliruhusu watu kusema, alifungua minyororo ya uchumi na alifungua milango ya siasa za ushindani.

Mzee Mwinyi aligeuzwa gunia, mfano wa lile linalojazwa mchanga kwa ajili ya wanamasumbwi. Hata mkewe hakusalimika na tuhuma mbalimbali zilizokosa mashiko.

Watu walibaini tabia, staha na uvumilivu wa Mzee Mwinyi baada ya kuonja utawala wa mrithi wake, Rais mbabe mwenye ubavu wa kufokea na hata kutukana waliompigia kura.

Huyu ni Benjamin William Mkapa, mwanasiasa aliyeokwa ili umma uamini yu mtu safi, muadilifu na mbeba dhamana ya uongozi kwa moyo wake wote. Ni kiongozi aliyejitoa katika muonekano wa ngozi ya kondoo, kumbe, baada ya kuongoza kwa miaka michache, alianza kuonyesha rangi zake halisi.

Sasa, baada ya kuona haya yaliyompata mke wa Chiluba, Regina kwa kufungwa jela, hisia zimenijia juu ya mwisho wa Rais mstaafu Mkapa na mkewe, Anna.

Mkapa, rafiki mkubwa wa Muluzi, hivi sasa atakuwa anatafakari yamekuaje kwa mwenzake. Wanafanana mno, isipokuwa kwa namna moja kubwa. Yeye hakujaribu wala kuwaza kubadili katiba ili apate kugombea tena baada ya muhula wake kwisha.

Mkapa pia hakufinyanga mrithi wake. Ndiyo! Hata kama mwisho wa siku alikubaliana na Rais Jakaya Kikwete kuwa mrithi wake, haitakuwa kwa kupenda yeye ila alilazimika kimazingira.

Alihofu nguvu za mtandao; alihofia CCM kumeguka kama asingekubali yaliyoandaliwa kutendeka kama ilivyodhihirika pale alipokengeuka utaratibu uliozoeleka wa kutafuta mgombea mmoja kutoka watatu.

Angefanya ukichwa ngumu na kuendelea kupanga mtu wake, gharama ingekuwa kubwa. Naye alishaapa hawezi kuwa mwenyekiti wa mwisho wa chama kikongwe alichoachiwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Mkapa alitoa sifa za ziada za Kikwete kwenye Mkutano Mkuu Dodoma, ilhali akijua kuwa hiyo ilikuwa ni rafu maana wakati huo walikuwepo washindani wenzake, Profesa Mark Mwandosya na Dk. Salim Ahmed Salim.

Leo kelele zinapigwa kuhusu mwenendo wake alipokuwa rais. Yanatajwa kwa nguvu aliyoyatenda mkewe na pengine hata na mwenyewe huku akishuhudia wenzake, Chiluba na Muluzi, wakibanwa mbavu.

Hapa ndipo ninapopata hisia kwamba Mkapa analala na hofu. Kila akifikiria nyuma anatamani ardhi ipasuke ajitie maana hakuna tena muda wa kujisahihisha.

Kuna habari za kuthibitika namna walivyojilimbikia mali maana alipoingia Ikulu na kutaja mali anazomiliki, ni tofauti na alivyotoka.

Labda Muluzi na Chiluba hawakuwaza kwamba wangeweza kufika walipo sasa, lakini hata Mugabe hakuwahi kuwaza kuwa ipo siku atagawana madarakana na Morgan Tsvangirai. Hakuna lisilowezekana!

Ndiyo maana namuuliza Mkapa pamoja na kutamka kuwa yote yanayosemwa dhidi yake ni uongo na kutaka magazeti yanayomchafua yachanwechanwe; ana hakika ya kuvuka salama?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: