Benki ya Barclays sasa vululuvululu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

KASHFA ya udanganyifu wa riba iliyoigubika benki ya Barclyas kwa siku kadhaa, ilichukua sura mpya juzi baada ya mwenyekiti wa Bodi, Marcus Agius (pichani) kuamua kujiuzulu.

Wakati akiachia nafasi hiyo, Agius alisema "mzigo wa lawama unabaki kwangu" baada ya kashfa hiyo kubwa kuathiri hadhi ya benki hiyo.

Agius, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Barclays kwa miaka mitano na nusu, ni kiongozi wa kwanza kukumbwa na kashfa ambayo inaonekana kuzikumba benki nyingi na mamlaka za usimamizi wa fedha, lakini kujiuzulu kwake hakujapunguza joto kwa mtendaji wake mkuu, Bob Diamond, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kuondoka pia.

"Mzigo wa lawama utamkumba Bob Diamond, naye lazimika awajibishwe," alisema John Mann, mwanasiasa wa chama cha Labor ambaye ni mmoja wa wabunge watakaomhoji Diamond leo Jumatano na Agius kesho Alhamisi.

"Yeye (Diamond) lazima ajiuzulu. Anatakiwa kuondoka pia. Hakuna nafasi kwa watu kama yeye kama kweli ya Barclays inataka kuaminiwa tena nchini katika juhudi za kurejesha heshima ya benki hiyo iliyochafuliwa duniani kwani ni jambo la muhimu kwa uchumi wetu," Mann aliiambia Sky News.

Diamond na Agius wamekuwa wakitakiwa na baadhi ya wadau nchini humo kujiuzulu kutokana na kitendo cha benki ya Barclays kutozwa faini ya kiasi cha dola milioni 453 wiki iliyopita kutoka mamlaka za udhibiti za Uingireza na Marekani kwa kuwasilisha kiasi kisichostahili cha kiwango cha riba.

"Kwa hili, bado nafikiri kuwa itakuwa vigumu kwa Bob Diamond kundelea kubaki na kazi yake,” alisema mmoja wa viongozi 25 wa benki ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo, Diamond na Agius watahojiwa na kamati ya bunge  kutaka kujua Benki Kuu ya England (BoE) ilikuwa inajua nini kuhusu kashfa hiyo.

Taarifa zinasema nyaraka zilizotolewa wiki iliyopita zinaweza kuiumbua BoE, baada ya vyanzo vya kuaminika kuonyesha yalifanyika mazungumzo Oktoba 2008 na waliotajwa katika nyaraka hizo ni Diamond na gavana msaidizi wa BoE, Paul Tucker.

Si Barclays tu, bali zaidi ya benki 12 zinafuatiliwa katika mchakato wa uchunguzi duniani ukifanywa na mamlaka husika katika nchi za Amerika ya Kusini, Ulaya, na Japan ukihusisha benki za  Citigroup, HSBC, UBS na Royal Bank ya nchini Scotland.

Uongozi wa Barclays umekiri kwamba uliwasilisha viwango vya chini vya riba vya mikopo katika kipindi cha Novemba 2007 na Oktoba  2008 kutokana na kile walichoamini hata wengine walikuwa wanafanya vivyo hivyo na kwamba ikiwa wangeongeza wangejikuta kwenye matatizo.

0
No votes yet