Bethidei ya Anna Mkapa na njozi zangu


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version
Mama Anna Mkapa

LEO 29 Aprili, Anna Mkapa anatimiza miaka 67. Ni yule mke wa rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyekuwa mpangaji wa ikulu kati ya 1995 na 2005.

Najisikia kumpongeza Mama Mkapa kwa kuwa ni watu wachache wanaofikia umri huo katika nchi zinazoendelea. Ninasema ni wachache kwa kuwa safari ya kufikisha misimu hiyo 67 ni ngumu na yenye vikwazo lukuki.

Katika umri huo, bila shaka Mama Mkapa ameona, amesikia na kuguswa na mengi. Hakuna shaka kuwa anayo simulizi ndefu ya kuwaambia wengi kuhusu alikotoka na alipo hivi sasa.

Lakini kwa mtazamo wangu, ninadhani sehemu kubwa ya simulizi hiyo ndefu itakuwa imejikita kwenye kipindi chake cha kuwa Ikulu. Hapo ndipo nadhani utamu wa simulizi unaweza kupatikana kutokana na mikikimikiki iliyopo katika Kitalu Na. 1.

Lakini Mama Mkapa hawezi kuongea mengi leo. Atasimama. Atatupa neno moja au mawili. Itabidi simulizi zake azifanye siku nyingine. Siku hii atamwachia mumewe aongee. Sasa natafakari mambo atakayokuwa nayo Benjamin Mkapa.

Natafakari hisia atakazokuwa nazo na pengine cheche ambazo anaweza kuzitoa wakati akimpongeza Anna kwa kufikisha umri wa miaka 67.

Ili mahali hapo pawe burudani nzuri, ni pale rais mstaafu atakapoamua kuvunja ukimya na kusema, enough is enough – “Imetosha – sasa naamua kuvunja ukimya juu ya tuhuma zote zinazoelekezwa kwangu, kwamba nilikitumia vibaya mno Kitalu Na. 1.

Njozi yangu inasema Mkapa atasema hivi: “Ninamshukuru Mungu aliyetuwezesha kuiona siku hii muhimu; na ninamshukuru zaidi kwa kumfikisha mwenzangu katika umri huu wa maisha yake. Hongera sana Anna na Mungu akujalie maisha marefu zaidi ili ikiwezekana uweze kuiona hata bethidei ya 100.”

Naona kama Mkapa atasema, “Bila shaka wengi wenu mliopo hapa mtakuwa mmewahi kusikia kuwa mimi, nikiwa na wadhifa wangu wa mkuu wa nchi, katika Kitalu Na. 1, mnamo 22 Juni 1999 nilibariki usajili wa kampuni yangu ya ANBEM.

“Kwamba mimi na Anna ndio tulioandikishwa kuwa wakurugenzi wake, tukiwa na makazi binafsi katika Barabara ya Mfaume, Upanga, Dar es Salaam. Kwamba Anna ndiye aliyekuwa mkurugenzi msimamizi kuanzia 21 Juni 1999.

Njozi yangu inamwona Mkapa akiendelea kuwa “ANBEM imekuwa na hisa katika Kampuni ya TanPower Resources Limited kwa ajili ya kuendeleza mgodi wa Kiwira ulioko mkoani Mbeya. Eti wanasema mgodi huo tuliununua kwa bei poa.

“Kwamba ANBEM imesababisha serikali kulazimika kulipa Sh. 17 bilioni ambazo iliweka dhamana katika mkopo waliopewa Kampuni ya TanPower Resources Limited kwa ajili ya kuendeleza mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira ulioko mkoani Mbeya.

“Kwamba fedha hizo hazikutumiwa kwa lengo lililokusudiwa ambalo lilikuwa ni pamoja na kukarabati mitambo ya mgodi.

“Kwamba TanPower Resources Limited ni kampuni yenye wanahisa watano – kila mmoja akiwa anamiliki hisa 200,000, ikiwamo ANBEM Limited ambayo wanadai inamilikiwa na sisi wawili.

“Kwamba makampuni mengine yenye hisa kama sisi ni Devconsult International Limited ya Dar es Salaam inayomilikiwa na Daniel Yona na Dan Yona; Universal Technologies Limited inayomilikiwa na Wilfred Malekia na Evans Mapundi; Choice Industries Limited inayomilikiwa na Joe Mbuna na Goodyear Francis na Fosnik Enterprises Limited inayomilikiwa na Nick Mkapa, Foster Mkapa na B. Mahembe.

Njozi zinanituma kumwona Mkapa akiendelea, “Kwamba, kwa pamoja tulipewa Sh. 17 bilioni kutoka serikalini kwa ajili ya kukarabati mitambo ya mgodi wa Kiwira iliyokuwa imechakaa na kuhitaji matengenezo makubwa, lakini hakuna kilichofanyika.

“Kwamba kwa pamoja, pamoja na kuwa na fedha zote hizo, tumeshindwa kukarabati mitambo yote na uzalishaji umeme umeshuka kutoka megawati sita zilizokuwa zikizalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa kabla ya mgodi kubinafsishwa, hadi megawati moja, isiyotosha hata kwa yale maeneo ya Kyela, Ileje na Rungwe yaliyolengwa awali.

“Kwamba, kwenye makaa ya mawe uzalishaji umeshuka mno kulinganisha na ilivyokuwa kutokana na uchakavu wa miundombinu uliochangiwa zaidi na kutokarabatiwa.

Wakati wageni waalikwa wakiwa kimya na kufuatilia kauli hizo, Mkapa ataendelea, “Nimekwisha eleza waziwazi kuwa watuache tupumzike tule pensheni yetu. Wanatulazimisha tupanue midomo yetu, tujibu mapigo. Aslani hatuwezi kufanya hivyo!

“Tunao utetezi wa kutosha kutoka kwa mrithi wetu, kwamba waachane na sisi, watuache tupumzike, lakini inaonekana hawasikii wala kuelewa somo.

“Pamoja na utumishi wetu wa miaka yote kumi, bado kuna watu wanashinikiza tuchukuliwe hatua za kisheria, eti kwa kuunda kampuni tukiwa bado madarakani. Ebo! Hawajui na sisi tulijiandikisha kwenye kampuni hiyo kama wajasiriamali? Watuache tupumzike kwa amani.

“Sasa nasema hivi: Pamoja na presha ya kunitaka niseme wasitarajie chochote kutoka kwenye kinywa changu. Isitoshe, tayari tumekingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa juu wa dini na baadhi ya wananchi wenye mapenzi mema.

“Kamwe sitafungua mdomo wangu, na wasitarajie nitaonekana hadharani kwa urahisi. Dar es Salaam kuna umbeya mwingi. Nitakaa nyumbani kwangu Lushoto au wakati mwingine Masasi ambako huwa napata uhuru wa kukutana na watu mbalimbali na kuzungumza.

“Tayari nimemwambia Anna kwamba msimamo wangu ni uleule. Waache waseme, waache waseme, mwisho wake watalala fofofo.

“Anna,” ataita huku akitabasamu, “Tumevumilia mengi. Tumevumilia makombora ya kila aina. Leo hii ninafurahi kuona kwamba unatimiza bethidei ya 67. Hongera sana na Mungu ashukuriwe kwa kutuwezesha kuiona siku hii tena. Hepi bethidei tuuyu!”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: