Bila fedha hupati urais Kenya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

KADRI msimu wa kampeni za uchaguzi mkuu wa rais nchini Kenya unavyokaribia – miezi michache ijayo – kuna neno moja tu linalowafanya wagombea wote wa urais wawe macho nalo: Fedha.

Katika mahojiano na wagombea urais na wasimamizi wa kampeni kutoka ndani ya vyama vitakavyokuwa na wagombea, inaelekea kwamba matumizi ya fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu yanaweza kuwa maradufu ya miaka mitano iliyopita.

Kampeni hizo zinatarajiwa kuwa kubwa zaidi, zenye ushindani zaidi na msisismo zaidi huenda kuliko miaka mitano iliyopita.

Kinachosababisha hayo yote ni katiba mpya inayotoa fursa mpya kwamba mwananchi atamchagua rais, mbunge, seneta, gavana na wawakilishi katika serikali za mitaa.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Coalition for Accountable Political Financing (CAPF), yenye makao yake makuu jijini Nairobi inakadiri kuwa Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga walitumia dola za Kimarekani 75 milioni (kiasi kilichoweza kufuatiliwa) kwa ajili ya kampeni za urais mwaka 2007.

Wachunguzi wa ndani wa masuala ya kampeni walisema hivi karibuni kuwa kampeni za urais, zikilenga kupata siyo tu urais, bali pia maseneta wa kutosha na wabunge kutoka miongoni mwa wagombea wa vyama ili waweze kuendesha bila matatizo, zinaweza kumgharimu mgombea urais kati ya dola 100 milioni na dola 50 milioni.

Wachunguzi hao wanakadiria kwamba wagombea wa nafasi ya urais kama vile Uhuru Kenyatta, William Ruto, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, George Saitoti, Peter Kenneth, Raphael Tuju na Martha Karua, kila mmoja anaweza kutumia kiasi hicho katika kampeni hizo.

Hata hivyo matarajio ya Kenyatta na Ruto yamepigwa kumbo baada ya kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake The Hague, Uholanzi kwa makosa waliyofanya katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Upande mwingine matumizi ya fedha kwa wagombea urais yanatarajiwa kuingiza zaidi ya dola 500 milioni katika uchumi wa Kenya, kichocheo cha fedha kinachoweza kuongeza mfumo wa uchumi katika nchi ambayo inakabiliwa na maisha magumu (Mfumo wa bei Januari ulikuwa asilimia 18).

Hata hivyo, fedha hizo zinatarajiwa kuishia kwenye mifuko ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa na washauri katika vyombo vya habari na siasa kwa vile wagombea watatoa fedha hizo kwa ajili ya matangazo, biashara, safari na kulipa waratibu wa kampeni.

0
No votes yet