Bila katiba mpya tutagalagazwa milele


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version

HAKUNA ubishi, kwamba Tanzania ni moja ya nchi zenye katiba zinazotokana na watawala badala ya watawaliwa.

Ni katiba inayotoa mwanya kwa ufisadi, uzembe, utovu wa nidhamu kwa watawala na udhalilishaji wananchi, huku ikiwabebesha kila aina ya mzigo.

Hii ni katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyoandikwa na wateule wachache wa utawala wa chama kimoja wakati ule.

Kwa mfano, ni katiba hii inayoelekeza kuwa mtu akiishatangazwa kuwa mshindi wa urais, hata kama kuna ushahidi wa Mungu na sheria kuwa ameshinda kwa kuchakachua, hakutakuwepo mahakama, wala mwenye mamlaka ya kupinga au kuhoji matokeo hayo.

Maana ya ibara inayoruhusu “usultani” huu katika katiba ya Tanzania ni kwamba, rais yuko juu ya sheria. Je, aliyeko juu ya sheria anaweza kuwajibika kwa wananchi?

Katiba inayozuia mtu kuhoji matokeo ya urais, ni ileile inayotumika kulinda rais, hata aliyestaafu, dhidi ya matendo yake akiwa ofisini.

Ni katiba inayotoa ulinzi na kinga kwa rais aliyeko madarakani, aliyestaafu na hata marafiki na washirika wake.

Kwa ufupi, hii ni katiba inayompa fursa rais aliyeko madarakani, kutafuta kwa nguvu zote, mtu atakayefuata kuwa rais ili awe yule tu ambaye hatashughulikia makosa yake pindi aking’oka ikulu.

Wataalamu wa katiba wanasema: Lazima katiba itoke kwa wananchi na ikubaliwe nao kwa ajili yao. Iandikwe na mkutano wa katiba, ukijumuisha wadau wote nchini.

Hiki ni kigezo muhimu kwa katiba yoyote kuitwa endelevu na ya umma. Bahati mbaya, katiba yetu ilitokana na tume ya rais.

Katiba hii imekuwa kikwazo kwa mageuzi ya kisiasa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Inampa rais hata nafasi ya kuhonga na kulipa fadhila kwa kugawa madaraka.

Kwa mfano, nani anajua kwanini wakuu wengi wa wilaya na mikoa ni wanajeshi? Ni mbinu za kuwapa mahali pa kupumzikia baada ya miaka mingi kambini?

Ni kuwapa pole na kuwazawadia kwa kazi walizofanya? Ni kudharau kazi ya utawala ngazi ya wilaya na mkoa kuwa inaweza kufanywa na mtu yeyote?

Kipengele kinachompa rais mamlaka ya kuteua, hata mahali ambako uwezo kitaaluma ungekuwa kigezo, kinanyima taifa fursa ya kutumia wajuzi na wenye taaluma katika utawala.

0
No votes yet