Bila kubebwa Kikwete hawezi kushinda urais


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Rais Jakaya Kikwete

NAWEZA kusema kitu ambacho watu wengi tayari wanakijua au kukikubali bila haja ya kufanya jitihada kubwa ya kuwashawishi.

Kwamba, bila ya kubebwa na vyombo vya dola na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete asingekuwa na nafasi ya kusimama tena kama mgombea na kwa hakika asingeweza kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Sasa hili linaweza lisikubalike na baadhi ya watu, lakini mtu yeyote ambaye ataliangalia kwa ukaribu kwa ushahidi mdogo tu nitakouweka hapa utaona kuwa jitihada kubwa imefanyika ya kuhakikisha kuwa Rais Kikwete haanguki, ndani ya CCM na kwenye uchaguzi mkuu.

Kufanya jitihada kuwa Kikwete asidondoke ni jukumu la shabiki wake yeyote yule na ni sehemu ya fani ya siasa. Kumpigia kampeni Kikwete siyo kosa hata chembe na watu (wawe wana CCM au vinginevyo) kujitokeza kumuunga mkono si jambo baya kwa kipimo chochote kile. Tatizo pekee ambalo ninaliona ni pale haya yote yanapofanyika kwa gharama ya kufuta demokrasia ndani ya CCM na ndani ya Taifa.

Ninachokiona sasa hivi (na nimekuwa mfuatiliaji wa siasa za Tanzania kwa muda mrefu tangu 1995) ni kuwa kuna jaribio la hatari la kumbeba Kikwete “kwa gharama yoyote ile”.

Inapofikia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano anapigiwa kampeni na mtoto wake ambaye tayari ameshagubikwa na wingu la kusababisha mvurugano kwenye Jumuiya ya Vijana basi ni lazima mtu mwenye kufikiri ajiulize ni nini kinachoendelea.

Kwa sisi wachunguzi tunaweza kuangalia kwa ukaribu na kuona dalili mbaya huko mbeleni. Niwe wa kwanza kusema kuwa sitashangaa kama Ridhiwani Kikwete atakuwa mgombea Ubunge mwaka huu na hata kupewa unaibu waziri! Mnafikiri haiwezekani? Fumbueni macho mtashuhudia!

Lakini kubebwa kunakofanyika naamini kuna hatari zaidi kwa CCM kuliko kitu kingine. Wakati kwenye Ubunge na Urais wa Zanzibar wana CCM wanaruhusiwa kugombea jimbo lolote bila kujali kama kuna mbunge wa zamani au la kwa sababu ni “demokrasia” na pale ambapo kuna wabunge wamedai kuna njama za kuwahujumu kwenye “majimbo yao” wamekuwa wakipuuziwa na likija suala la Urais mtazamo ni tofauti.

Wakati wabunge wanakebehiwa kuwa “hakuna mtu mwenye hodhi ya jimbo” kwa Urais inaonekana Rais Kikwete ndiye mmiliki “halali wa Urais”.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana na labda mapema zaidi viongozi kadhaa wa CCM wamekuwa wakituimbisha wimbo wa “Kikwete awe mgombea pekee” wimbo ambao hivi majuzi watoto wetu huko Dodoma (wenye kuitwa “wasomi”) wameurudia pasipo kufikiria wimbo huu wa Kikwete awe mgombea pekee.

Mwenyekiti wa CCM mwenyewe hajamkemea mtu yeyote ambaye amekuwa akirudia wimbo huu mambo ambayo yamekuwa yakifanywa hata mbele yake (kama ilivyotokea kule Tanga). Uongozi wa CCM hauoni tatizo kuimba wimbo huu usio wa kidemokrasia wa kumtaka Kikwete awe mgombea pekee.

Sababu ya wao kufanya hivyo ni rahisi kufahamika. Kikwete angepewa ushindani huru ndani ya CCM asingeweza kushinda.

Maneno kuwa Kikwete ni “mtaji” hayana ukweli wowote kwa sababu ni mtaji kwa kadiri ya kwamba ni “mtaji pekee”. Kama Kikwete angekuwa anakubalika ama kwa wananchi au ndani ya CCM angekuwa wa kwanza kutetea haki ya kushindanishwa akiamini kuwa rekodi yake inamtosha kumshinda mgombea mwingine yeyote.

Kama Kikwete angeweza kuchujwa kama wanavyochujwa marais wa Marekani nina uhakika wa asilimia 100 Kikwete angedondoshwa kiurahisi tu au kupata changamoto kubwa ambayo ingemfanya anoleke vizuri.

Lakini kwa sasa, CCM haiwezi kuweka mtindo kama huo kwa sababu wanaogopa asije akaumbuka.

Hii haina maana kuwa Kikwete siyo mtu mzuri, na wala haina maana kwamba Kikwete hajafanya “lolote”. Maana yake ni kwamba kiungozi Kikwete ni dhaifu kuliko marais wengine wote waliowahi kuwepo na kama angepata mshindani katika mazingira huru kabisa Kikwete asingepita.

Na yeye mwenyewe amesema kweli hivi karibuni alipodai kuwa kama angeboronga CCM wangemtosa. Tatizo ni kuwa hawawezi kumtosa wakati yeye ndiye Mwenyekiti wa CCM na Rais ambaye amezungukwa na kila aina ya ujiko utishao.

Matokeo yake Kikwete anasemwa pembeni, anakebehiwa pembeni, anadharauliwa pembeni na wakati mwingine na baadhi ya watu wa karibu yake kabia au ambao wanaonekana wako karibu yake. Laiti mambo ambayo yanasemwa juu yake na watendaji walio chini yake yangepata kuandikwa, nina uhakika kuna kundi la watu wangetimuliwa bila hata ya kusikilizwa kama Obama alivyomtimua Jenerali McChrystal wiki iliyopita.

Lakini kubebwa anabebwa. Hii ndiyo siri ya kupinga wagombea binafsi! Kikwete asingekuwa na nafasi kama haki ya Watanzania kugombea nafasi yoyote bila kufungwa minyororo ya kitumwa ya vyama vya siasa isingefutwa na Mahakama ya Rufani.

Kikwete angeweza kutumia mbinu kukihujumu chama cha upinzani au kukiwekea mizengwe, kwa mgombea binafsi angefanya nini? Ndio maana hata mara moja hajawahi kutetea haki hii ya msingi ya wananchi kwa sababu ingeweza kumgeuka.

Nina uhakika kabisa kuwa tunapoelekea uchaguzi mkuu na baada ya wagombea wengine wa Urais kujulikana, Kikwete hatofanya mdahalo nao. Kikwete hawezi kujadiliana na kujenga hoja huku anabanwa katika jukwaa huru kujieleza kwa sababu rekodi yake ni tata.

Si kwa sababu siyo mtu mzuri, si kwamba si mcheshi au hana mvuto, la hasha. Kwa kila kipimo cha umaarufu na uzuri yawezekana Kikwete anaongoza katika vingi.

Lakini katika uongozi wa siasa mvuto wake ni wa kulazimisha. Pasipo kubebwa na kutengenezewa mazingira ya kuwa mshindi pekee Kikwete asingeweza kushinda. Sijui kama anastahili ngwe nyingine au la, sijui kama angeweza kushinda ndani ya CCM au la, lakini historia itakuja kutoa hukumu kali ya jaribio baya kabisa la kuminya demokrasia ndani ya CCM.

Sitoshangaa hawa hawa wenye kuimba wimbo wa “awe mgombea pekee” na yeye mwenyewe kubariki (kwa ukimya wao) ndio watakaosimama mwaka 2014 wakianza kuimba wimbo wa “aongezewe muda” na hivyo kuweza kubadilisha Katiba yetu na kuondoa ukomo wa urais. Nina uhakika watakuwepo na hawataogopa.

Hawataogopa kwa sababu Mahakama Yetu ya Rufaa imekubali kuwa CCM inaweza kubadili Katiba na kuweka kipengele chochote hata chenye kufuta haki za wananchi kwa sababu tu wamefuata “utaratibu” unaokubalika.

Watabadili Katiba na kuondoa ukomo wa urais kwa sababu wanaweza na watoto wetu hawa hawa wa vyuo vikuu watakuwa wa kwanza wakiongozwa na “mtoto wa kwanza” kuanza kupita na kukusanya maoni ya kuunga mkono.

Demokrasia imevunjwa ndani ya CCM, na kwa sababu hiyo ni kanuni kubwa imevunjwa, basi kanuni hiyo itatafuta namna ya kutuvunja. Nyerere alionya juu ya kuvunja kanuni.

Wameivunja kanuni
Hawaulizwi kwanini
Wameficha kama mbuni
Vichwa vyao mchangani
Atawazindua nani
Demokrasia kutetea?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: