Bila kutambika mafanikio hayatapatikana serikalini


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

NILIKIOZALIWA mimi, kwa mila na desturi nyumba ni kitu kinachoheshimiwa sana. Ni mwiko kwa mtu yeyote yule mwanaume au mwanamke, bila kujali cheo chake, nafasi yake katika jamii au ukoo anaotoka, kucheza na nyumba ya mtu mwingine kwa njia yoyote ile.

Na ikitokea, kwa bahati mbaya mtu akaharibu, akachoma au akavunja nyumba ya mtu, basi hana budi mtu huyo mharibifu, kwa njia yoyote ile kutambika ili aweze kuepusha balaa na laana.

Balaa na laana zinazompata mtu akichezea, akichoma au akivunja nyumba ya mtu ni pamoja na kukosa baraka katika maisha. Baraka wanazoamini mtu anaweza kukosa ni pamoja na kukosa uzazi, pale watoto wanapopatikana kufa tena wakiwa bado wachanga.

Kwa sababu hiyo, kule kwetu Nyamongo, Bukira, Bunchari, Butimbaru, Busweta na Bukenye watu hawachezei au hawaharibu au hawavunji wala kuchoma nyumba za watu. Na hali ni hiyo hiyo kule Namanyere, Rukwa; Kanyigo, Kagera; Miono, Pwani; Magogoni na Chirombola, Morogoro; Naipingo, Lindi; Nangurue, Mtwara na hata Uchagani, Kilimanjaro.

Ajabu ni kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilicheza na nyumba za Watanzania katika kipindi kile ambacho uongozi wa awamu ya tatu ulikuwa mbioni kuondoka madarakani na kuupisha uongozi wa awamu ya nne ukiongowa na Jakaya Kikwete.

Kitendo kilichofanywa na serikali ya Rais Benjamin Mkapa mwaka 2004 akimtumia Waziri wa Ujenzi wa wakati huo, Dk. John Pombe Magufuli, ambaye bado anaendelea kuhudumu katika nafasi hiyo, hakikueleweka, hakieleweki na hakitaeleweka maishani.

Eti Mkapa na wafuasi wake wakaamua kugawana nyumba za serikali kwa kisingizio kwamba gharama ya kuzitunza ilikuwa kubwa mno!

Wengi waliopata nyumba hizo ni watu walioweza kuhonga na kurubuni wagawaji nyumba katika Wizara ya Ujenzi matokeo yake hata watu ambao hawakuwa wafanyakazi wa serikali nao walipata nyumba za serikali kwa bei sawa na bure.

Jambo kubwa lililojitokeza ni kwamba karibu wote waliopata nyumba hizo hawaishi katika nyumba hizo bali wamezikodisha kwa wageni na wanalipwa kwa pesa za kigeni. Maana ya ukweli huu ni kwamba waliogawana nyumba za wananchi hawakuwa wahitaji wa nyumba bali wabadhirifu wa nyumba.

Mbadhirifu ni yule ambaye anatumia zaidi kuliko anachohitaji na hapa mawaziri, makatibu, wakurugenzi na maofisa wa serikali na CCM ambao walikuwa na nyumba ndio waligawana nyumba hizi kama bakshish.

Wewe sikiliza yanayosemwa kuhusu ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa sana Dk. Harrison Mwakyembe. Eti serikali moja ya CCM inakuwa na ndimi tatu tofauti kuhusu ugonjwa wa Mwakyembe! Laana ya nyumba zetu hiyo.

Waziri wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Samuel Sitta, anasema Dk. Mwakyembe alipewa sumu lakini hamtaji ni nani huyo aliyempa sumu. Pia Waziri Sita hasemi huyo mtoaji sumu alimpa Mwakyembe hiyo sumu lini na wakiwa wapi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba anadai Mwakyembe hakupewa sumu na anamtaka Waziri Sitta athibitishe maneno yake. Na kuonyesha kuwa hataki utani amefungua faili dhidi ya mtu aliyesema (bila shaka ni Waziri Sitta) Dk. Mwakyembe na sasa tumeambiwa hati ya mashitaka ipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Eliezer Feleshi ikitazamwa vizuri kabla ya kuwapelekwa mahakamani.

Lakini pia ametokea Waziri wa Afya, yule bwana asiyetakiwa na madaktari wa Tanzania, Dk. Haji Mponda, kasema kuwa ugonjwa wa Dk. Mwakyembe ni siri ya mgonjwa mwenyewe. Naye Waziri wa Mambo ya Ndani kajitokeza kilingeni kudai eti yeye na polisi wake bado wanatafuta chanzo cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe!

Msicheze na nyumba za watu hamtaweza kufanikiwa wala kuendelea bila kutambika kuondoa mikosi inayowaandama. Watanzania milioni 40 wamenyang’anywa nyumba na kilio chao ni laana na balaa kubwa kwa waporaji nyumba. Katambikeni nyie CCM kama Watanzania wengine wanavyofanya.

Bungeni nako hawajui au hawaelewi kama posho za wabunge zilitoka, hazikutoka na kama zilitoka walipata wangapi maana wengi wanadai hawakuzipata posho hizo. Laana ya nyumba inawafanya viongozi wa serikali na Bunge wasijue cha kujibu kila wanapohojiwa kuhusu posho.

Spika wa Bunge Anne Makinda anasema posho ziliongezwa na zilianza kutolewa. Katibu wa Bunge hilo hilo, ambaye ndiye mtendaji mkuu, Thomas Kashilila anasema posho hazikuongezwa na hazikutolewa kwa sababu sheria inataka nyongeza yoyote ile iidhinishwe na Rais wa Jamhuri.

Akaja huyo anayeitwa mtoto wa Mkulima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akasema Rais Jakaya Kikwete kaidhinisha posho za wabunge zipande kutoka Sh.70,000 hadi Sh. 200,000 kwa maana maisha huko Dodoma yamepanda sana kuliko miji mingine ya Tanzania.

Kesho yake ofisi ya Rais, ikulu, kupitia kurugenzi ya mawasiliano, ikakanusha jambo hilo ikidai Rais hajaidhinisha nyongeza ya posho za wabunge. Haya sasa anayebisha kuwepo laana na balaa linalotokana na wizi wa nyumba, uporaji wa nyumba, uvunjaji wa nyumba na uchezaji na nyumba zetu atuambie laana hii inatokana na nini?

Ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni. Nenda Songea mkoani Ruvuma halafu uwaulize wakubwa mkoani humo swali moja tu rahisi sana. Je mmeua raia wangapi katika maandamano? Mkuu wa Mkoa kwanza atatisha kuwa anaendelea kuwasaka na kuwachukulia hatua waandamanaji na waliokufa ni wawili tu.

Kamanda wa Polisi Mkoa, Michael Kahmanda yeye anasema kafa mmoja tu na mwingine kagonga mti na pikipiki wakati akifanya vurugu lakini Mganga mkuu wa mkoa huohuo anasema yeye kapokea maiti wanne na majeruhi kibao!

Serikali moja, nchi moja na chama kimoja kinachotawala lakini majibu kibao tena yanatofautiana kulingana na wewe umemuuliza nani. Laana hiyo ya nyumba zetu. Ya Kamanda wa Operesheni na Mafunzo, Charles Chagonja anayedai Songea kuna wahuni na waandamanaji walitaka kuteka ikulu na ofisi ya Mkuu wa Mko, siyazungumzii hapa.

Nirejee tu kusema kwamba binadamu hapaswi kuchezea nyumba za watu, kuharibu nyumba za watu, kuvuruga nyumba za watu na hata kuvunja nyumba zetu. Ukifanya hivyo yatakukuta yanayoikuta serikali ya CCM leo, mpaka haielewi inafanya nini na wakubwa wake tena wasomi wanashindwa kujibu maswali rahisi. Dawa ni moja rudisheni nyumba zetu hilo ndilo tambiko pekee bila hivyo mambo hayatawanyookeni.

0
No votes yet