Bilal, Khatib, Nahodha huenda wakatoswa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Dk. Mohammed Gharib Bilal

VIONGOZI wanaotaka kuwania urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huenda wakaenguliwa wote na hata kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Taarifa ambazo MwanaHALISI limepata kutoka kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kilichomalizika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, zinasema viongozi hao ndio wanapinga mpango wa kura ya maoni Visiwani.

Kwa zaidi ya miezi miwili sasa kumekuwa na taarifa za chinichini Visiwani na Bara kwamba baadhi ya viongozi wanajiandaa “kukwamisha zoezi la kura ya maoni Zanzibar” baadaye mwaka huu.

Wanaopinga kura ya maoni wanadai kuwa kinachopangwa sasa siyo kilichokubaliwa katika NEC ya Butiama ya Aprili mwaka jana.

Baadhi ya wanasiasa wanaodaiwa kuwa na mpango wa kuvuruga suala hilo, ni pamoja na wasaidizi wakuu wa Rais Karume.

Tayari Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) imemnukuu Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha akisisitiza kuwa kura ya maoni haijapigwa na kwamba si lazima wananchi waikubali.

Viongozi wengine wanaotajwa kuwa na kiu ya kugombea urais na kuhusishwa na kutopenda kura ya maoni ni Dk. Mohamed Gharib Bilal na Muhammed Seif Khatib.

Dk. Bilal ni waziri kiongozi mstaafu chini ya utawala wa Rais Salmin Amour (1995-2000) na Khatib ni waziri wa nchi masuala ya Muungano katika serikali ya Rais Kikwete.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Yussuf Mohamed, naye anadaiwa kupita katika baadhi ya majimbo ya Zanzibar kushawishi wanachama wa chama chake kupiga kura ya kukataa serikali ya umoja wa kitaifa.

Mtoa taarifa ameeleza, “Wapinzani wa kura ya maoni ndani ya CCM wanasema pale Butiama tulikubaliana wananchi waulizwe, lakini azimio lililopo mbele yetu linaagiza viongozi kuhamasisha wananchi kukubaliana na hoja.”

Lakini Bilal na Khatib walipoulizwa iwapo wanapinga maagizo ya NEC, walikana kufanya hivyo.

Bilal ameiambia MwanaHALISI kwa njia ya simu, “Mimi sijasema lolote sheikh. Nimesema wapi? Mimi naona watu wanataka kunisingizia katika hili. Sijui lolote na mimi sijasema lolote kuhusu hayo.”

Kwa upande wake, Khatib ameliambia gazeti hili, “Umepata wapi habari hizi – Zanzibar au Bara? Mimi sijapinga; kama kupinga nimepinga wapi, lini na kuna ushahidi gani?”

Khatib amesema maamuzi ni ya “Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa na mimi sina nguvu mbele ya vyombo hivyo.”

Naye kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) amekaririwa akitoa kauli ileile.

“Mimi nakwambia, hakuna serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar. Haya ni mambo ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Abeid Karume, basi,” kiongozi huyo ameliambia gazeti hili kwa sharti la kutoandika jina lake.

Mjadala wa kura ya maoni uliibuka katika ajenda maalum iliyoitwa, “Uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar” katika kikao cha NEC kilichomalizika mwishoni mwa wiki.

Kilicholeta zogo ni hoja iliyowasilishwa katika kikao hicho ikitaka wajumbe kuhamasisha wananchi kukubali hoja ya kura ya maoni katika hatua ya kumaliza migogoro Zanzibar.

Taarifa za wapinzani zinasema iwapo kura ya maoni itafanyika, basi “asilimia 74 ya wananchi wataonyesha kuwa wamekataa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Visiwani.”

Ndani ya NEC baadhi ya wajumbe walisimama kidete kukwamisha hoja ya kushawishi wananchi kuunga mkono kura ya maoni, ameeleza mtoa taarifa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mjumbe mmoja wa NEC kutoka Zanzibar alinukuliwa akimueleza mwenyekiti Kikwete, “Sisi msimamo wetu uko wazi. Tunasimamia maamuzi ya Butiama.”

Katika kikao cha Butiama, NEC iliagiza serikali ya Zanzibar kuandaa utaratibu wa kuitisha kura ya maoni inayolenga kuuliza wananchi, iwapo wanataka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi ujao.

“Pale Butiama tulikubaliana kuuliza wananchi. Hapa mmekuja na hoja ya kutaka tushawishi wananchi. Kuuliza na kushawishi ni mambo mawili tofauti,” alisema mjumbe huyo.

Ni baada ya kauli ya mjumbe huyo, ndipo mjumbe kutoka Zanzibar, Catherine Peter Nao, alipoibuka na kusema, “Tumekuelewa mheshimiwa Kikwete, subiri matokeo.” Nao hakufafanua kauli yake.

Ilionekana wazi katika kikao cha NEC kwamba Rais Kikwete, akiwa mwenyekiti, alikuwa akielekeza msimamo wa chama kwamba ni kuipigia kampeni kura ya maoni Zanzibar.

Naye mjube wa NEC kutoka Bara, Kate Kamba alitaka chama kieleze hatua zitakazochukuliwa dhidi ya viongozi watakaopinga zoezi la kura ya maoni.

Rais Kikwete amenukuliwa akimjibu Kamba kwa kusema, “Tutaamua papohapo watakapojitokeza.”

Mchakato wa kura ya maoni ya haraka na kundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, vilitokana na mikutano ya siri yaa mwaka jana kati ya Rais Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad.

Tayari Baraza la Wawakilishi (BWZ) limeridhia kuitishwa kwa kura ya maoni kwa shabaha hiyohiyo.

Akihutubia bunge jipya mjini Dodoma, baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2005, Rais Kikwete aliahidi “kushughulikia mpasuko” wa kisiasa Zanzibar.

Haijaeleweka vizuri iwapo Rais Kikwete amekuwa nyuma ya mazungumzo ya siri kati ya Rais Karume na Seif Shariff Hamad.

0
No votes yet