Bodi ya Mikopo haijali mustakabali wa taifa


Godbless Charles's picture

Na Godbless Charles - Imechapwa 12 May 2009

Printer-friendly version

MAONI ya waliosoma makala yangu katika gazeti hili la Apili 8-14, yenye kichwa cha habari, “Bodi ya Mikopo inapuyanga,” yamenisukuma kuandika makala hii, ambayo nitaitumia pia kujibu baadhi ya hoja za watendaji wa bodi hiyo.

Baadhi yao walisema wangependa kufahamu jinsi Bodi hii inavyotekeleza sera yake ya ukopeshaji. Bodi ya mikopo ni taasisi ya serikali inayotoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kulingana na sheria Na 9 ya mwaka 2004, ambayo utekelezaji wake ulianza Julai 2005.

Sheria hiyo inataka Bodi kusimamia utoaji mikopo kwa wanafunzi wa stashada za juu na shahada katika taasisi za elimu zilizosajiliwa kwa mujibu wa sheria, ndani na nje ya Tanzania. Inaipa bodi mamlaka ya kukusanya pesa kwa wanafunzi wote waliosomeshwa na serikali tangu mwaka 1994.

Ukisoma kwa makini sheria iliyoanzisha bodi hiyo, utangundua kuwa bodi ilanzishwa kutekeleza sera ya ukopeshaji kwa wanafunzi wa elimu ya juu, wala si sera ya uchangiaji kama ambavyo inahubiriwa na serikali na watendaji wa bodi husika.

Kuwapo kwa bodi hiyo hakujasaidia wanafunzi wetu vyuoni. Ndiyo maana tumekuwa tunashuhudia migomo na migogoro isiyokwisha kwenye taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi kwa wale wanakopeshwa na bodi hii.

Katika mwaka wa masomo 2007/2008, bodi hiyo ilitengewa Sh 122 bilioni  kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 56,071. Badala yake, bodi ilitumia Sh 62.2 bilioni tu. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 52.2 tu ya fedha zilizotengwa na serikali kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu.

Ukiachana na mabilioni haya ya fedha ambayo mpaka sasa matumizi yake yanatiliwa mashaka, mkurugenzi wa Bodi amekiri kuwa serikali inatoa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Bodi.

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo, George Nyatega anajaribu kujitetea kwamba eti gharama za kuendesha Bodi ni ndogo. Anasema hadi kufikia mwaka jana (yaani 2007/2008) ilikuwa Sh 62.2 bilioni kwa wanafunzi 56,071.

Anasema, “Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma nchini ni 23, 061, na wanaoendelea na masomo ni 32,012; wanaosoma nje ya nchi ni 998. Kwa maana hiyo basi, kama Bajeti ya Bodi ya Mikopo kwa Mwaka 2007/2008 ilikuwa takribani 122 bilioni, kiasi cha Sh 62.2 bilioni pekee ndicho kilichotumika kutoa mikopo kwa wanafunzi. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 52.2.”

Kwa maana hiyo basi, kiasi kilichobaki cha Sh  54.8 bilioni kilitumika katika kuendesha Bodi ya Mikopo. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 47. Kwa hivyo basi matumizi ya Bodi ya mikopo ambao idadi ya wafanyakazi hawazidi hata mia moja wanatumia sawa na idadi ya wanafunzi 56,071. Kiasi hiki cha fedha za kuendesha Bodi ni mbali na Sh 1,392,133,375 zilichokusanywa kutoka kwa wakopaji hadi kufikia Desemba 31 2008.

Pia kiasi hicho ni mbali Sh.10,000 fedha ambazo Bodi ya Mikopo inawatoza wanafunzi wanaojaza fomu za kuomba mikopo, pesa ambayo hukusanywa kwa wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita nchini  wanaooomba, kwa sasa bila kujali kama wamefaulu ama la kwa hoja kwamba eti zoezi la kuchambua fomu linachukua muda mrefu.

Lakini pia inaonekana kwamba Bodi ya Mikopo haitoi taarifa za kweli za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Nyaraka mbalimbali zimethibitisha hilo. 

Kwa mfano mkurugenzi Nyatega anasema katika barua yake kwa Viongozi wa Serikali za Wanafunzi yenye Kumb. Na. CB 83/92/049 ya 5 Januari 2009 kwamba “Menejimenti ya Bodi ya Mikopo na Viongozi wa Serikali za wanafunzi katika kikao kilichofanyika tarehe 29 Novemba 2008, ilikubalika kuwa uandaliwe utaratibu wa kupata taarifa za uhakika kutoka kwa Serikali za Wanafunzi kuhusu wanafunzi ambao inaonekana wamepewa viwango vya juu vya mikopo wakati hali zao halisi za kiuchumi ni nzuri.

Ushahidi mwingine unaotuthibitishia kuwa Bodi ya Mikopo inatumia taarifa za uongo kutoa mikopo ni ripoti ya Kamati Maalumu ya kushughulikia matatizo ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji elimu ya juu ambayo ilitumia mamilioni ya fedha za walipa kodi, chini ya uenyekiti wa Profesa Anselm Luoga iliyowasilishwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 20 Januari 2009.

Kamati hiyo iliundwa baada ya migomo iliyovikumba vyuo vya umma kupinga sera hiyo. Iliwahoji wadau mbalimbali ili kupata maoni kuhusu uboreshaji wa sera hiyo, ikiwamo Menejimenti ya Bodi ya Mikopo. Katika ripoti hiyo, wajumbe wa Bodi wanakiri kuwa wanafunzi walitoa taarifa za uwongo.

Hivyo basi, hoja ya Mkurugenzi Nyatega kuwa Bodi haitumii taarifa za uwongo kutoa mikopo si sahihi. Bodi haina uwezo wa kubaini ipi ni taarifa sahihi na ipi si sahihi.

Vilevile, Nyatega anasema baadhi ya wanafunzi ambao wametoa taarifa za uwongo wamechukuliwa hatua. Lakini hajasema ni wanafunzi wangapi wamechukuliwa hatua mpaka sasa. Walikuwa wanasomea vyuo gani, na kama bodi imewachukulia hatua za kisheria, ni kesi ngapi zipo mahakamani?

Nilisema kuwa wajumbe wanalipana posho nono za vikao, tena kwa kikao kisichozidi hata saa tatu. Nilisema na nitaendelea kusema kuwa posho ya Sh 300,000 mpaka 500,000 kwa kikao kimoja haiendani na hali ya uchumi wa nchi yetu.

Mkurugenzi hajakanusha wala kukubali taarifa za malipo hayo manono. Kwa gharama hizi na nyingine, kila mwanye akili timamu hawezi kusema Bodi inajiendesha kwa gharama ndogo.

Gharama hizi ndogo za uendeshaji wa Bodi zinalinganishwa na za Bodi gani hapa nchini? Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludorvich Utoh imebaini hilo.

Posho ya Sh 500,000 kwa kikao kwa saa mbili kwa kila mjumbe ni sawa na fedha za kujikimu za mwanafunzi wa chuo kikuu kwa siku 100. Ni sawa na mshahara wa mwezi wa walimu watano wa shule ya msingi na sekondari.

Mkurugenzi wa Bodi ameonyesha uwezo mdogo mno katika suala analosimamia. Naishauri serikali na wadau wote wa elimu kutafakari udhaifu huu wa Bodi, ambao mimi nauita unyonyaji dhidi ya wananchi. Menejementi ya Bodi haijaonyesha kwamba inajali mustakabali wa taifa katika suala zima la elimu.

Mwandishi wa makala hii, Godbless Charles ni Mkurugenzi wa Habari kwa Umma na Masuala ya Kimataifa, wa Tanzania Students Networking Programme ( TSNP). Anapatikana kwa barua pepe: god4zungu@gmail.com Simu: 0717 682 586

0
No votes yet