Bodi ya Mikopo ni Mradi wa CCM?


Josephat Isango's picture

Na Josephat Isango - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version

UKISOMA kwa haraka tamko la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), unaweza kuwasifu. 

Lakini ukiliangalia kwa makini, utaweza kugundua kuwa tamko lile lililenga kusafisha baadhi ya watu ndani ya chama na serikali na kukandamiza wengine.

Kwa nini nasema hivyo? Pengine utaniuliza. Kwanza, wengi wa walioshiriki katika kutoa tamko, ama kikao kilichofikia utoaji wa kauli zile, ni walewale wanaonufaika na genge la watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.

Baadhi yao wanafahamika hata wale wanaowafadhili katika shughuli zao za kila siku. Miongoni mwa wanaofahamika kufadhiliwa na watuhumiwa wakuu wa ufisadi, ni James Ole Milya anayetaka mjadala wa Richmond urejeshwe bungeni.
Milya ni mwandani wa waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashifa ya sakata la mkataba tata wa Richmond, Edward Lowassa.

Ukimsikiliza kwa makini Milya, haraka utagundua kwamba alikuwa anafanya kazi moja tu: Kumsafisha Lowassa ili kumuandalia mazingira mazuri ya kisiasa katika siku zijazo.

Unafiki wa viongozi hawa unaanza pale wanapokiri kuwa Richmond ilikuwa kampuni hewa, lakini hawakutaja vigogo walioingiza nchini kampuni feki.

Badala yake, vijana hawa walioajiriwa kufanya kazi maalum, waliishia kutoa dibaji tu: Walimtuhumu aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Viongozi wa UV-CCM walimtuhumu Sitta na Dk. Mwakyembe kwa sababu mbili. Kwanza, kusimamia Bunge kuchunguza tuhuma dhidi ya Richmond na Dowans na pili, kile walichoita, “kushindwa kuwajibika kwa pamoja.

Lakini UV-CCM hawakuzungumzia lolote kuhusu uamuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuhalalisha malipo ya Dowans wakati ambapo hata kikao cha baraza la mawaziri kilikuwa hakijafanyika.

Jingine ambalo UV-CCM walilizungumzia katika mkutano wao na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, ni suala zima la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Msemaji wake katika eneo hili, Zainab Kawawa, alisitiza “ni lazima bodi ya mikopo ipinduliwe.”

Hakueleweka. Je, alitaka safu ibadilishwe, kwa yule wa chini kuwa juu, au uongozi mzima uondolewe madarakani kwa mabavu.

Kimsingi UVCCM katika eneo hili, wamesahau mengi. Mathalani, sheria ya bodi ya mikopo inasema wanafunzi wote watakaodahiliwa na kuwa na sifa zinazostahili hawatakosa ufadhili wa bodi.

Lakini barua ya bodi ya 6 Julai 2009 yenye Kumb. Na. AB.48/55/01/34 ilikuja na mwongozo tofauti.

Ilisema wanachuo wanaosoma masomo ya sayansi watasomeshwa kwa mkopo wa asilimia 100. Hii ina maana kwamba, kile kinachoitwa, “Sera ya uchangiaji” kimefutwa rasmi.

Lakini papohapo, serikali inasema wale watakaodahiliwa katika idara ya elimu, wataendelea kuchangia. Kigezo kitakachotumika ni kilekile, kutumia taarifa zitakazopatikana kutoka kwa viongozi wa vijiji.

Kupitia mfumo huu, bodi ya mikopo inaweza kuamua kufanya itakavyo, bila kujali idadi ya wanafunzi ambao chuo husika kimedahili. Yapo hata malalamiko ya kushamiri kwa upendeleo katika vyuo vya umma.

Kutokana na mfumo huu wa kikatili, hakuna mwanafunzi atakayekuwa huru kuchagua chuo atakachopenda kusomea, ispokuwa bodi ndiyo itakayoamua.

Je, UV-CCM wanalijua hili? Je, wanafahamu kuwa kwa mfumo huo, bodi ya elimu itakuwa haindelezi elimu, bali itakuwa inaididimiza na kulifanya taifa kukosa wataalamu?.

Je, UV-CCM haifahamu kuwa pamoja na mapungufu yake, maamuzi mengi ya hovyo yanayofanywa na bodi ya mikopo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali yenyewe?

Jingine ambalo linasababisha bodi ya mikopo kushindwa kutekeleza majukumu yake ni uhaba wa fedha.

Mara kadhaa watendaji wa bodi hii, wamekuwa wakilalamika serikali kushindwa kuwapa fedha kwa wakati au kuwanyima kabisa.

Uzoefu unaonyesha kuwa kila mwaka bajeti inayosomwa bungeni, inatofautiana kwa kiasi kikubwa na fedha zinazotolewa.

Ni kwa sababu, serikali imekuwa ikichukulia suala hili kisiasa zaidi. Fedha hazifiki kwa wakati. Mfano hai ni hatua ya serikali kughairisha kufungua vyuo vikuu Septemba mwaka jana kwa kuhofia uchaguzi mkuu, na ikasema inaandaa pesa ili vyuo vifunguliwe Novemba.

Hadi Januari hii, bado kuna lundo la wanafunzi wanaoteseka. UV-CCM wanalijua hili. Wanajua kuwa taizo ni ombwe la uongozi lililopo serikalini na katika chama chao, lakini kwa kuwa walitumwa na kikundi fulani cha watu, hawawezi  kulisema hili kwa mapana yake.

UV-CCM wanafika mbali zaidi. Wanasema, “UV-CCM haiko tayari kuendelea kuvumilia kuona vijana wenzetu wakiwa wanateseka kwa ubinafsi na ukiritimba unaosababishwa na watendaji wachache wa bodi ya mikopo,” anasema Zainabu kwa sauti ya ukali.

Anasema, “UV-CCM inakitaka Chama Cha Mapinduzi kuipindua rasmi bodi ya mikopo ili vijana wenzetu wasome kwa utulivu na hatimaye waje kushiriki katika kulijenga taifa.

Hapa haraka unapata swali moja kubwa la kujiuliza. Je, bodi ya mikopo ni mali ya CCM? Kama siyo, inawezekana vipi vijana hawa wakatamka kuwa “tunakitaka chama chetu kuipindua rasmi bodi ya mikopo?”

Je, wamepata wapi uwezo huo? Nani amewahakikishia usalama wao? Nani atakayelinda mapinduzi yao?

UV-CCM imebaini kuwa kuna urasimu unaofanywa na watendaji, na kwamba haiingii akilini wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa wagome kwa kutolipwa fedha zao.

Viongozi wa umoja huu, wanaona tatizo la migomo liko Mkwawa tu? Mbona hawazungumzii lolote kuhusu wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki? Hawazungumzii migomo ya wafanyakazi, madai ya walimu, Shirika la Reli la taifa (TRC), mabenki, viwanda na mashamba?

Ni bahati mbaya kwamba hata msemaji mwenyewe – Zainabu Kawawa – si mwathirika wa maisha ya watoto maskini. Zainabu yupo katika tabaka la waliobarikiwa. Anaweza hata kuamua kwa niaba yetu, kupanga kwa niaba yetu na kusema kwa niaba yetu.

Mwandishi wa makala hii, Josephat Isango amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI, mwalimu na mwanaharakati. Anapatikana kwa simu Na. 0786-426414/ 0712 - 303906
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: