Bodi ya Mikopo yakiuka sheria


Josephat Isango's picture

Na Josephat Isango - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version
Mtazamo

SERIKALI ya Jamhuri imekiuka Sheria Na. 9 inayounda Bodi ya Mikopo nchini. Wakati sheria inasema wanafunzi wote watakaodahiliwa na kuwa na sifa zinazostahili hawatakosa ufadhili wa Bodi, barua ya Bodi ya 6 Julai 2009 yenye Kumb. Na. AB.48/55/01/34 imetoa mwongozo tofauti.

Bodi inasema, “Wanachuo wanaosoma Sayansi watasomeshwa kwa mkopo wa asilimia 100. Hii ina maana kwamba kwao, kile kinachoitwa, “Sera ya uchangiaji” kimefutwa rasmi.

Lakini papohapo, serikali inasema wale watakaodahiliwa katika Idara ya Elimu, wataendelea kuchangia. Kibaya zaidi, kigezo kitakachotumika ni kilekile cha kutumia taarifa zitakazopatikana kutoka kwa viongozi wa vijiji.

Mfumo huu, unaifanya Bodi ya mikopo kuamua itakavyo, bila kujali idadi ya wanafunzi ambayo chuo husika kimedahili. Mfumo huu umevipa vyuo vya umma kipaumbele kwa ukopeshaji.

Kulingana na mfumo huu wa kikatili, hakuna mwanafunzi atakayekuwa huru kuchagua chuo atakachopenda kusomea, bali itaamuliwa kulingana na idadi iliyoamriwa na bodi.

Je, kwa mfumo huo, Bodi ya elimu inakuwa inaendeleza elimu au itakuwa inaididimiza na kutufanya taifa lisilo na wataalamu?

Bodi haikuzingatia mahitaji ya wananchi. Mfumo huu utavifanya vyuo vikuu kupata nafasi chache za kudahili. Hili ni tangazo jingine la kifo kwa vyuo vikuu vya binafsi hasa vile ambavyo vilikuwa na lengo la kusaidia wananchi.

Kuna vyuo vikuu vingi vya binafsi vinavyotoza ada ndogo kuliko hata vile vya umma. Inawezekana serikali haikufuta kwa nia njema azimio lake la kuondoa msamaha wa kodi kwa mashirika ya dini.

Kwa utaratibu huu ni wazi kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi watakaokopeshwa watatoka vyuo vya umma; vyuo vikuu vya binafsi vijiandae kuzikwa.

Kuna mambo mengi mchanganyiko katika suala hili. Kwanza, iwapo serikali inasema haina uwezo wa kulipia watoto wote wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu, kwa nini inajitwisha mzigo mwingine wa kulipia wanafunzi wa sayansi kwa asilimia 100 bila kujali kama wazazi wao wana uwezo au hawana?

Pili, kama serikali inasema haina fedha za kutosha, kwa nini fedha hizi zisitumike kuongeza idadi ya wanafunzi kuliko kuchukua fedha hizi kulipia watu wenye uwezo?

Tatu, kile kinachoitwa na serikali, “Sera ya uchangiaji” mbona hakifuatwi katika suala hili?

Nne, tarehe 2 Juni 2009 wakuu wa vyuo vikuu nchini walikutana katika ukumbi wa mikutano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo waliamua kuwa mfumo huu usipitishwe. Je, nini kimesukuma serikali kukaidi agizo hilo la makamu na manaibu wa vyuo vikuu?

Tano, serikali haioni kwamba kupanga idadi ya wanachuo wanaopaswa kufadhiliwa kupitia Bodi ya Mikopo, hata kama wamefaulu kutawafanya mamia ya vijana wetu kurudi nyumbani?

Sita, kama mfumo wa serikali ni kuchukua wanafunzi wachache kutoka wanafunzi waliomaliza masomo ya kidato cha sita, nani anahakikishia wanafunzi hawa kurudishiwa Sh. 30,000 walizozitoa kulipia fomu, hasa wale watakaokosa nafasi?

Bodi imekusanya pesa za Watanzania wangapi kwa njia hii haramu ambayo hakuna uhakika kuwa pesa hiyo itarudishiwa? Je, elimu ya juu kwa wanafunzi waliofaulu kidato cha sita ni fadhila au haki? Hakika, maswali ni mengi.

Kama ni haki kwanini Watanzania wasiipate. Ni wazi kwamba hapa kuna kila dalili kuwa serikali imedhamiria kuleta migomo vyuoni. Hakuna dalili kuwa serikali imejinfunza kutokana na makosa ya huko nyuma.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine cha Nyegezi (SAUTI), Mwanza. Anapatikana kwa simu Na. 0786-426414
0
No votes yet