Bomu la Mwakyembe lalipuka


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version
Ni katika Sakata la Richmond
Mke wa waziri alipigia magoti Kamati
Mke wa Edward Lowassa akiwa na majonzi Bungeni

MKE wa mmoja wa mawaziri watatu waliojiuzulu kutokana na sakata la Richmond, alipigia magoti baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge akiomba wamlinde mume wake, imefahamika.

Hili ni moja ya mambo ambayo hayamo ndani ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge na ambayo yalipaswa kuwekwa wazi.

Timu ya waandishi wa habari za uchunguzi ya MwanaHALISI imegundua kuwa mke wa kigogo huyo (jina tunalo), alikwenda mbele ya wajumbe wa Kamati kwa lengo la kushawishi Kamati 'imlinde' mumewe.

Hata hivyo, mwanamke huyo aliambiwa kuwa asubiri ripoti itoke kwa kuwa wao walitumwa kuchunguza na siyo kuhukumu.

Gazeti hili pia limegundua kuwa mmoja wa mawaziri wa sasa 'aliwafuma' vigogo wawili (majina tunayo) katika ofisi ya serikali, usiku wa manane wakiwa katika harakati za kubadilisha mkataba huo kutoka Richmond Development Company (LLC) kwenda kwa dada yake Dowans.

Haikufahamika haraka kama hili ni moja ya mambo ambayo mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe alisema kamati yake haikuyataja kwa shabaha ya 'kulinda serikali.'

Akichangia mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri mkuu, wiki mbili zilizopita, Dk.Mwakyembe alisema kama kuna mtu anadhani hakujitetetea vya kutosha, basi mjadala uanze upya kuliko kutenda kinyume na Kanuni za Bunge.

Alituhumu baadhi ya wabunge akisema wamevunja Kanuni za 54 na 55 za Bunge zinazozuia jambo ambalo lilikwishajadiliwa bungeni kurejewa kujadiliwa.

'Kama watuhumiwa wana mambo hawakuyasema, turudishe mjadala huu upya. Waseme wanaoyajua na sisi tupo tayari kueleza hata yale ambayo tuliacha kueleza kwa kulinda heshima ya serikali,' alisema.

Kauli ya Dk. Mwakyembe ilitokana na kile kinachoelezwa kuwa jitihada za baadhi ya wabunge na vyombo vya habari kutaka 'kuwasafisha' watuhumiwa.

Inaelezwa kwamba mke wa kigogo aliyepigia magoti baadhi ya wajumbe wa Kamati, alirekodiwa na kanda yake imetolewa nakala na kuhifadhiwa na baadhi ya wajumbe.

MwanaHALISI haikuweza kuthibitisha kama kanda hizo zilimfikia Spika wa Bunge Samwel Sitta ambaye alipoulizwa kuhusu suala hili alisema ana taarifa na alichopewa peke yake.

Waandishi watatu wa gazeti hili walisikiliza kanda hiyo na hawakuwa na utata katika kutambua mara moja sauti ya mke huyo wa kigogo aliyekuwa akitafuta huruma kwa mume wake.

Naye Mwakyembe alipoulizwa kuhusu taarifa za mke wa kigogo na kanda zake, alijibu haraka, 'Kazi yetu iliisha zamani. Hakuna mjadala mpya.'

Imebainika kuwa Richmond, kampuni ya kufua umeme, ilipewa zabuni kwa upendeleo. Aidha, imedhihirika kuwa kampuni hiyo iligawa mkataba wake kwa kampuni ya Dowans kinyume cha taratibu.

Kutokana na hali hiyo, wiki iliyopita, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilitangaza kuvunja mkataba wa Dowans na kuitaka kampuni hiyo kuodoa mitambo yake nchini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: