Bonde la Rufiji hazina tupu


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 16 June 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Chini ya RUBADA laweza kukomboa nchi

KAMA unadhani Tanzania haiwezi kulima chakula cha kutosheleza watu wake wote, badilika kimawazo.

Bonde la Mto Rufiji peke yake lina uwezo wa kutoa chakula kinachotosha mahitaji ya nchi na kitapatikana chakula cha kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye.

Lakini pia, Taifa litapata chakula cha ziada kwa ajili ya kuuza kwa nchi nyingine zitakazokabiliwa na tatizo la uhaba.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Aloyce Masanja anasema:

“Tukipewa uwezo na kuongezewa nguvu tunaweza serikali, uwezo upo wa Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa kutumia kilimo na hatutakuwa na haja ya kuomba msaada kutoka nje.”

Masanja, katika mahojiano maalum na MwanaHALISI yaliyofanyika wiki iliyopita kwenye ofisi za RUBADA, Ubungo mjini Dar es Salaam, analalamika kuwa serikali haijatilia mkazo mpango huo.

“Serikali ni kama imeisusa RUBADA kwa kutotupa kipaumbele huku wafanyakazi wakilipwa mishahara midogo tofauti na mamlaka nyingine za serikali,” anasema.

Mikakati ya kuwezesha RUBADA kutumika ili kuzalisha mpunga wa kutosha ipo tayari.

Bonde la Mto Rufiji lina eneo la kilomita 177,000 za mraba likijumuisha mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na sehemu za mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mbeya na Singida.

Ndani ya mikoa hiyo, kuna mabonde manne yenye rutba - Kilombero, Usangu, Ruwegu na Rufiji Chini – yaliyo chini ya usimamizi wa RUBADA na yanafaa kwa kilimo cha mpunga. Morogoro ndiko kwenye ghala kuu la chakula (FAMOGHATA) wanalolisimamia.

Mamlaka hiyo, anasema Masanja, imekuwa katika harakati za kutafuta wawekezaji wa kushiriki katika mpango wa kuzalisha mpunga katika bonde hilo.

Tayari RUBADA kwa kushirikiana na kampuni ya InfEnergy Limited ya Uingereza, imeanza kilimo cha umwagiliaji katika katika shamba la hekta 5,818 lilioko kijiji cha Mngeta ndani ya Bonde la Kilombero.

“Hawa wamelima hekta 2,765 na matarajio ni kuvuna tani 11,060 za mpunga katika msimu huu wa kwanza,” anasema Masanja.

Miongoni mwa teknolojia iliyotumika katika kilimo hicho, ni kushuhudia upandaji mbegu katika shamba hilo kufanywa kwa kutumia ndege.

Kazi inayofanywa na kampuni hiyo imeshirikisha wakazi 221 wa Mngeta walionufaika kupata ajira. Ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mpunga hadi tani 100,000 umeanza.

RUBADA pamoja na Waingereza hao wamenunua mashine ya kisasa ya kupukuchua mpunga yenye thamani ya Sh. 185 milioni. Uwezo wake ikishafungwa, itakuwa ni kupukuchua tani mbili za mpunga kwa saa moja, anasema Masanja.

“Mashine hii ni ya kwanza kununuliwa katika nchi za ukanda wa mashariki mwa Afrika,” anasema. Wanakijiji wa Mngeta wanaolima mpunga, watanufaika na mashine hiyo kwa kupeleka mpunga wao hapo.

Kampuni nyingine iliyoonyesha nia ya kushirikiana na RUBADA kuwekeza eneo la Bonde ya Mto Rufiji ni MIRO, inayojiandaa kutumia shamba la lililoko Ikwiriri katika bonde la Rufiji chini.

Bonde la Mto Rufiji ni muafaka pia kwa uzalishaji umeme wa kutumia maji. Masanja anasema utafiti umeshafanywa wa kubaini hazina iliopo kwa ajili ya uzalishaji wa nishati hiyo.

Kwa ujumla, mradi uliobuniwa kwa ushirikiano na Stiegler, una uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme. Hicho ni kiwango kikubwa cha umeme kuzalishwa nchini kwa kuwa hakijawezekana kupitia maporomoko ya Kihansi, mkoani Iringa.

Masanja anasema kwamba kuna miradi mwingine uliobuniwa baada ya utafiti; ambao ukitekelezwa ipasavyo, utawezesha uzalishaji umeme kufanyika. Hii ni miradi ya Ruhuji (megawati 685), Mnyera (megawati 485), Kilombero Kingengenanas na Shuguli Falls (megawati 464), Mpanga (megawati 165), Lukose (megawati 130) na Iringa (megawati 87).

“Miradi hii ikifanyiwa kazi vizuri itatuwezesha kupata nishati ya kutosha nchi nzima na ziada tutauza,” anasema.

“Sasa hazina tuliyonayo ni kubwa. Inataka mkazo wa serikali. Na iwapo mamlaka yetu itapata rasilimali za kutosha kwa maana ya fedha, hakuna kisichowezekana,” anasema.

Masanja anabainisha mvutano uliopo kati ya mamlaka hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambao anadhani hauna sababu za msingi kama maslahi ya taifa yanawekwa mbele ya maslahi binafsi.

Anasema kama mradi wa kuzalisha umeme kutokana na maporomoko ya Kihansi umefanikiwa chini ya usimamizi wa Tanesco badala ya Rubada walioubuni, hatashangaa kukuta hata huo wa Stiegler unaelekea njia hiyohiyo.

“Hawa Tenesco wametuonea. Miradi tunayoibuni hatimaye inageuka ya kwao. Walianza na Kihansi na inaonekana Stiegler unawaumiza,” anasema.

Masanja alianza kazi na RUBADA mwaka 1993 kama mchumi wa mamlaka. Mwaka 1995 alikwenda Japan kwa mafunzo maalum ya kilimo na maji.

Aliporejea nchini, aliendelea na kazi mpaka 1997 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Amsterdam, Uholanzi kwa masomo ya shahada ya pili.

Aliporejea alipandishwa cheo na kuwa Ofisa Mipango wa RUBADA. Mwaka 2004 aliteuliwa Mchumi wa Mamlaka hiyo. Baadaye aliteuliwa Mkurugenzi wa Uchumi na Mipango hadi mwaka jana alipopandishwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA.

0
No votes yet