Bosi Dawasco ataka kuua MwanaHALISI


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version
OFISA Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala

OFISA Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala anadai MwanaHALISI dola za Marekani 500,000 (sawa na zaidi ya Sh. 800 milioni) kwa alichoita “kumkashifu.”

Gazeti hili toleo Na. 289, liliandika habari za uchunguzi juu ya dawa zinazotumika kusafisha maji katika mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Mtoni.

Gazeti lilitaja aina za dawa zinazotumika, ubora wake, jinsi dawa zinavyohifadhiwa – nyingine zikiwa hazina lakiri – na kwamba maji ya Dawasco hayakuwa salama.

Sasa Midala, kupitia kampuni ya mawakili – Didace & Co. Advocates ya Dar es Salaam, anasema amekashifiwa kwa taarifa hizo zilizochukua kurasa tatu, tena kwa kuhojiana na watendaji wa Dawasco na yeye mwenyewe.

Anadai mambo mawili. Kwanza, kuombwa radhi kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la MwanaHALISI na kusema kuwa taarifa lilizotoa zilikuwa za uongo.

Pili, kulipwa dola 500,000. Kwamba hayo yasipotekelezwa, atashitaki gazeti na wahariri wake mahakamani.

Huyu ndiye Midala ambaye wakati anachukua utawala wa Dawasco, gazeti la Mtanzania, Jumatano 21 Julai 2010 liliandika, “…hivi sasa anasoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara…”

Midala hakukana taarifa hiyo, ingawa tangazo la kutafuta CEO wa Dawasco lilikuwa linataka mtu ambaye tayari ana shahada ya uzamili.

MwanaHALISI linaendelea kuchunguza:

  • Mazingira ya mitambo ya maji Dawasco
  • Iwapo kweli Midala alikuwa na sifa za kuwa CEO (kwa mujibu wa taarifa ya Mtanzania iliyonukuliwa hapo juu)
  • Iwapo anasoma au alikuwa anasoma; anasoma wapi (chuo) na iwapo alimaliza masomo hayo kwa kufaulu.

 

Soma ‘Madudu ya DAWASCO na hasira za CEO’

0
No votes yet