Bukoba hawana madaktari


Felician Byakugira's picture

Na Felician Byakugira - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

MTOTO analia. Ni Justin Maro. Yuko mikononi mwa mama yake, Averina Nyangoma. Wanatoka kijiji cha Katoma, karibu kilometa sita nje ya mji wa Bukoba.

Wako kwenye foleni ya watu wapatao 25. Wanaandikisha vipande ili waende kuwaona madaktari. Mtoto analia bila kukoma. Mama yake anabembeleza, kubembeleza na kubembeleza. Justin hakomi kulia.

Kwenye foleni kuna mama mwenye watoto wawili – mapacha. Wanalia. Wanalia na kulia. Akina mama wengine wana watoto. Wanalia pia.

Kila mwenye mtoto anatamani afike dirishani. Apate kipande. Aende kukutana na daktari. Kulingana na vilio vya watoto, foleni inaonekana kutosogea lakini wamo tu.

Hatimaye Averina, mama yake Justin anafika dirishani na kupata kipande. Anakwenda moja kwa moja kwenye foleni nyingine ambako anakaa kwa dakika zipatazo 20.

Hapa anaambiwa siyo mahali pake. Aende kwenye foleni ya daktari wa watoto. Anakwenda. Anajiunga na foleni ya wanaokwenda kwa daktari wa watoto.

Daktari wa watoto hayumo ofisini. Wanasubiri. Daktari hafiki. Wanasubiri. Baada ya saa nzima, daktari anakuja. Anaingia ofisini. Baada ya dakika kama tano anafungua amlango na kutoka nje. Analo la kusema.

Daktari anawaambia wenye watoto kwamba kila anayetaka huduma sharti awe na chati kinachoonesha kuwa “amepima ukimwi” – mama na mtoto wake.

Akina mama wanaangaliana. Sura zao zinajipinda mithili ya tarakimu 8. Wanaguna lakini mguno haubadili kauli ya daktari.

Mama Justin anabeba kitoto chake. Anakwenda eneo la “kupimia ukimwi” –mahali pa kupimia afya kuona iwapo mtu ana virusi vya ukimwi (VVU).

Hapa inakuwa foleni nyingine. Justin anaendelea kulia na sasa sauti inaanza kubana. Ni karaha tupu.

Baada ya kusubiri kwa muda, Averina na akina mama wengine wanaambiwa vifaa vya kupima iwapo mtu ana virusi vya ukimwi vimeisha.

Ni safari fupifupi ndani ya hospitali lakini za mzunguko. Mama Justin na wenzake wanarudi kwa daktari wa watoto kueleza walichoambiwa. Wanakuta daktari wa watoto ametoka.

Ni karaha. Misonyo. Mvimbo wa nyuso na mashavu. Vilio vya watoto. Akina mama wanarudi kwa daktari wa watu wazima. Daktari hayumo. Wagonjwa wanaosubiri wanawaeleza, “daktari ametoka sasa hivi.”

Hapo ilikuwa saa 5.30 asubuhi. Tangu saa mbili na nusu Justin na mama yake wanatafuta daktari. Mtoto amelia na kukaukiwa sauti, huku akikohoa, kuhema na wakati mwingine kupitisha kinyeshi chembamba.

Hatimaye ninapigiwa simu. “Yule mtoto uliyesaidia kupeleka hospitali hajapata tiba. Mama yake hajaonana na daktari.”

Ninapewa maelezo marefu. Machungu. Ya kutisha. Ninawauliza wenzangu iwapo mjini Bukoba kuna hospitali binafsi ambako mtoto mdogo – miezi tisa – anaweza kupewa tiba. Ninaambiwa ni hospitali ya Hindu.

Ndipo nikawaelekeza Mama Justin na aliyefuatana naye kwenda Hindu. Walikwenda. Walikutana na daktari. Wakanambia anaitwa Dk. Kemibala.

Daktari alitaka kupima choo. Ajabu. Hakikupatikana. Wakapima damu. Justin akakutwa na malaria. Akachunguza kifua. Akasema ni kikohozi cha kawaida.

Mama Justin akaandikiwa dawa za kununua. Ni za Sh. 6,000. Ukiweka gharama ya kipande dirishani Sh. 2,000, inakuwa jumla Sh. 8,000. Lakini mtoto kapata huduma.

Wangapi wana uwezo wa kwenda praiveti? Wangapi wana bahati ya kupata msaada kama aliopata Justin?

Hata kama kusingekuwa na dawa, kupatikana kwa daktari ofisini kwake kwaweza kuwa sehemu ya tiba; kwani aweza kutoa ushauri. Lakini kama daktari hayupo, tufanyeje?

0
No votes yet