Bukoba watilia shaka ahadi za Kikwete


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete amedondosha ahadi Bukoba mjini kwa maratajio ya kuchota kura. Anatafuta kuendelea kupanga ikulu.

Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Bukoba Jumatano ya wiki iliyopita, Kikwete alinukuliwa akisema serikali itanunua meli kubwa na mpya itakayofanya kazi katika ziwa Viktoria na kupunguza kero ya usafiri ziwani.

Hivi sasa, meli ya mv Viktoria ndiyo kubwa inayofanya safari ziwani humo, baada ya mv Bukoba kupinduka na kuua zaidi ya watu 1000 Mei 1996.

Kikwete ametonesha vidonda hai. Tangu mwaka 1996 serikali imekaa kimya. Benjamin William Mkapa alimrithisha Kikwete kimya hicho. Kikwete amekuwa kimya kwa miaka mitano. Bila shaka kuna sababu ya Kikwete kuahidi ununuzi wa meli. Tutaona.

Nakumbuka mama yangu alizimia muda mfupi baada ya kuambiwa kuwa meli imezama na kuua watu wengi. Siku ya tatu baadaye aliaga dunia.

Ilikuwa hivi: Kaka yangu alimwambia mama yetu kuwa meli imezama na kuua watu wengi. Alimwambia kuwa yeye alikuwa asafiri kwa meli hiyo, lakini alipoona imejaa, akaamua kubaki pale bandari ya Kemondo ili asafiri siku nyingine. Hiyo ndiyo ilikuwa safari ya mwisho ya mv Bukoba.

Ndani ya meli hiyo aliteketea mke wa kaka yangu na watoto wake wawili. Aliteketea mpwa wangu Evelyn, mtoto wake na binti mmoja ambaye alikuwa amemchukua kutoka kijijini kwetu Bushumba ili amsaidie shughuli za nyumbani.

Nasimulia. Ilikuwa hivi: Baada ya kaka kumwambia mama yetu kuwa meli imezama na kuua wengi, mama aliuliza, “…na Ndimara alikuwemo?” Kaka alijibu, “Hapana. Ndimara yuko nje ya nchi.” Mama alijibu, “…hivyo ndivyo wamezoea kunidanganya…” Alikaa kimya hadi alipoaga dunia, siku ya tatu.

Hakika nilikuwa nje ya nchi. Nilikuwa mji wa Kariba kwenye bwawa la Kariba lililoko mpakani mwa Zambia na Zimbabwe. Tulikuwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari tukijadili “Sheria, Demokrasi na Vyombo vya Habari.” Nilipata taarifa kwenye televisheni iliyoonesha meli ilivyozama.

Niliomba gari kutoka ubalozi wa Sweden nchini Zambia. Nilipewa. Ni kilometa 249 kutoka Kariba hadi Lusaka. Kesho yake niliunganisha na ndege, wakati huo Shirika la Ndege Tanzania (ATC) iliyokuwa inapitia Harare na kurudi Dar es Salaam.

Nilifika Dar es Salaam jioni ya saa 12. Niliondoka Dar es Salaam kwenda Bukoba kesho yake asubuhi. Nilifika kijijini Bushumba siku hiyohiyo saa 10.30 na kukuta wananawa mikono – wamemaliza kumzika mama.

Mjini Mwanza nilikuwa nimemwacha kaka yangu, Gration Tegambwage akichuruzika machozi yasiyoisha – amepoteza mke na watoto wawili. Nilimwachia andishi lililokuwa limeandikwa kwa njia ya shairi awe analisoma na kuona iwapo lingemsaidia kutuliza roho; lakini siyo kusahau.

Asingeweza kusahau haraka au polepole kwani kila baada ya muda, maiti zilizoopolewa ziliwekwa uwanjani Nyamagana na alilazimika kufunua kila maiti kuona iwapo atamwona mpenzi wake – mkewe au angalau mmoja wa watoto wake. Ni majuto. Ni machozi yasiyokauka. Hakuona yeyote.

Vilio hivi vimeendelea ndani ya mitima ya wengi. Serikali imekaa kimya. Miaka mitano imepita. Rais akaomba kura tena. Akapata. Akatulia ikulu. Akasahau. Miaka ikapita. Akaondoka. Akaja mwingine – Jakaya Mrisho Kikwete.

Naye Kikwete amekaa miaka mitano. Sasa anaomba kura ili aendelee kupanga ikulu kwa miaka mingine mitano. Ndipo anaahidi meli.

Kwa kumbukumbu zangu mv Viktoria iliingia ziwani Viktoria mwaka 1965. Tunaambiwa haikuwa mpya. Huenda ni kweli. Tangu hapo imekata maji usiku na mchana hadi ikazeeka.

Meli hii imezimika mara kadhaa ikiwa safarini. Imeshindwa kuendelea na safari na kuwekwa ghatini kwa vipindi vingi. Imekarabatiwa na kukarabatiwa. Baadhi ya wafanyakazi melini humo wamesikika wakisema, “...nalo hili limeoza.”

Hii ina maana gani? Kwamba abiria wanasafiri kwenye mgongo wa mauti. Kwamba lolote laweza kutokea. Lolote lipi? Bila kutabiri majanga, lakini linajulikana: kuzama, kupinduka na kuua abiria mithili ya mv Bukoba.

Kinachouma ni kwamba mgombea wa CCM alipotoa ahadi ya meli, wananchi wa Bukoba walishangilia. Wachache walitikisa vichwa kwa masikitiko. Wachache au hakuna waliojiuliza kwa nini mgombea atoe ahadi siku hiyo na siyo miaka kadhaa iliyopita.

Niliwahi kuhutubia mkutano wa hadhara mjini Bukoba, miaka mingi iliyopita nilipokuwa mwakilishi wa Muleba Kaskazini. Niliwaambia wananchi, pamoja na mambo mengine kuwa, “…nimushekelela olufu nk’omunyima.”

Omunyima ni mnyama ndogo mweusi ambaye, hata anapofukuzwa na kupigwa, kwa nia ya kumuua, bado anaendelea kutoa sauti kama anayecheka. Ndipo wenye lugha yao wakasema “unachekea mauti kama mnyima.”

Wakazi wa Magharibi mwa Ziwa Viktoria wamekuwa wakichekea mauti kama mnyima. Kuna majanga mengi yaliyowakumba na serikali ikakaa kimya; lakini wao waliendelea kuonyesha tabasamu. Ni mengi na yanajumuisha vita vya Uganda na hata ukimwi uliokingiwa magego hadi watu walipoanza kupukutika.

Nilitoka Bukoba siku ya Jumatano ambayo mgombea wa CCM alikuwa ahutubie mjini hapo. Nilikutana na wanaume wawili na mwanamke mmoja – wote wa makamo – kwenye hoteli ya Victorius Perch.

Ni mwanamke aliyekuwa wa kwanza kueleza kuwa kuna mkutano wa mgombea urais wa CCM siku hiyo. Maneno yake yalidakwa na mmoja wa wanaume, na kama kawaida katika lugha yao. “Nani? Ekikwanga okyanga” – anayekukataa nawe huna budi kumkataa!

Ni ujumbe mkataa. Inaonekana hao hawachekei mnyima tena. Wanajadili mengi ambayo serikali imefanya lakini imesahau au imedharau wasafiri kwenye ziwa Viktoria wanahitaji na hakika wanastahili chombo imara cha usafiri.

Mmoja anang’aka, “Naona wanafikiri kuwa sisi tuna uzoefu wa kufa.” Mwingine anaorodhesha yale ambayo serikali imefanya na kutaja uwanja mpya wa taifa jijini Dar es Salaam kuwa ndio watawala wameona ni muhimu kuliko meli.

Kikwete atakuwa amebanwa sana katika kampeni za sasa za kutafuta urais hadi kufikia hatua ya kuahidi meli ziwani Viktoria ambayo hajawahi kutamka katika mipango yake.

Ni kama alivyofanya kwa wakazi wa Misenyi mkoani Kagera ambao wamekuwa wakifukuzwa kutoka maeneo yao ya asili kwa madai kuwa ni eneo la ranchi iliyobinafsishwa. Sasa anasema wapimiwe viwanja ndani ya ranchi.

Mgombea urais wa CCM anajua kuwa nani walinunua na wanamiliki ranchi ya Misenyi. Tumeambiwa ni baadhi ya marafiki zake. Alikuwa wapi hadi juzi ndipo aseme hilo? Mbona hakusikia vilio vya wananchi pale mkuu wa mkoa alipokuwa akiwakomalia kuwa wataweza kuhamishwa “hata kwa mtutu wa bunduki?”

Ahadi za Kikwete zitakuwa nyingi mwaka huu. Anayejua sababu ni yeye mwenyewe na chama chake. Kinachoonekana ni kwamba katika maeneo mengi, kama Bukoba na Misenyi, anajichongea.
Huenda kura zisitimie.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: