Bundi sasa amnyemelea Rais Kikwete 


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

KATIKA kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi ya kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara. Aliahidi kununua meli tatu zitakazotoa huduma katika maeneo ya maziwa makuu – Ziwa Viktoria, Tanganyika na Nyasa.

Aliahidi pia ununuzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400 katika eneo la Ziwa Nyasa na kujenga upya bandari ya Mbamba Bay, mkoani Ruvuma.

Lakini katika bajeti ya waziri wa mawasiliano na uchukuzi, Omari Nundu serikali haijatenga fedha yoyote ya kununulia meli mpya au kujenga bandari ya Mbamba Bay. Sasa bundi ameanza uchuro.

Kama Rais Kikwete ameshindwa kutenga fedha katika bajeti hii ya kwanza, bila shaka hataweza kufanya hivyo katika bajeti inayofuata na labda zote zinazofuata.

Wala rais hawezi kusema hakufahamu kuwa Nundu hakutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa meli. Kabla ya bajeti kuwasilishwa bungeni, shatri ipitie kwenye baraza la mawaziri, ambako Kikwete ni mwenyekiti. Sharti bajeti iendane na ilani ya uchaguzi ya chama kilichopo ikulu na mpango wa maendeleo wa taifa.

Hata katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliozinduliwa mjini Dodoma na Kikwete mwenyewe, Juni mwaka huu, na kisha kujadiliwa katika mkutano wa bunge la bajeti unaoendelea, serikali haionyeshi mpango mahususi wa kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biasahara ya kimataifa. Bundi amemtolea macho.

Mpango wa miaka mitano wa serikali hauonyeshi kuwapo mkakati wowote wa kuliokoa Shirika la Reli la taifa (TRC). Naye Nundu katika bajeti yake ameshindwa kuonyesha mpango mkakati wa kulifufua shirika hilo.

Katika kipindi cha kampeni, Rais Kikwete aliahidi ujenzi wa reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria kupitia Nzega mkoani Tabora, hadi Kigoma.

Bajeti ya Nundu haijatenga hata shilingi kwa kazi hiyo; ndani ya bajeti iliyopitishwa bungeni, TRC iliyokuwa kimbilio la wanyonge huko nyuma imeachwa yatima.

Kinachoonekana katika bajeti, ni serikali kulipa anayejiita mwekezaji –kampuni ya Rites kutoka India – mabilioni ya shilingi, pamoja na kwamba mwekezaji huyo ameshindwa kuliendesha shirika kwa kufanya vitendo vinavyoashiria kuvunjwa kwa mkataba. Hiki nacho ni chanzo cha mlio wa bundi.

Rais Kikwete aliahidi ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Misenyi, mkoani Kagera na uwanja wa ndege mkubwa mkoni Kigoma. Ndani ya bajeti hii ya kwanza ya muhula wa pili wa Kikwete, serikali haijaonyesha uwezekano wa kutekelezwa miradi hiyo.

Ndani ya miezi 10 serikali imeshiriki katika kuandaa maandamano na migomo ya kujipinga na kujiibia yenyewe. Kwa mfano, baadhi ya makampuni ya mafuta yanamilikiwa na serikali, angalau kwa asilimia fulani, na mengine yanamilikiwa kwa ubia na watendaji wake ngazi ya juu serikalini na wengine kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kampuni ya BP Tanzania Ltd., ni kielelezo cha hili. Serikali kupitia msajili wa hazina inamiliki asilimia 50 ya hisa za kampuni ya BP. Hisa nyingine 50 zinamikikiwa na kampuni ya M/S Puma Energy Investment Ltd.

Hata hivyo, pamoja na BP kumilikiwa kwa ubia kati ya serikali na kampuni ya M/S Puma Energy Investment Ltd., mkurugenzi mtendaji wa chama cha waingizaji wakubwa wa mafuta (TOMAC), Salum Bisarara amesema mgomo huo umeungwa mkono na makampuni yote yanayouza mafuta nchini ikiwamo BP.

Kauli ya Bisarara imeungwa mkono na mwenyekiti wa chama cha makampuni yanayoagiza mafuta nchini, Selan Naidoo. Hapa bundi akilia, kwa ishara ya hatari inayokabili nchi, nani atashangaa?

Kuna madai mengi yanaibuka katika eneo hili. Kwamba wapo wanaosema, “dili hili” la mafuta limepikwa na watendaji wa serikali wanaomiliki biashara ya mafuta ili kujinufaisha binafsi.

Watendaji hao wa serikali wanaoshiriki katika maandalizi ya bajeti kuu ya taifa, ndio wanadaiwa kupenyeza hoja ya ongezeko la kodi kwenye mafuta kwa kuwa walijua “sharti serikali itasalimu amri” na mwisho wa siku wao ndiyo watakaonufaika.

Mwezi mmoja baada ya bajeti kuu kupitishwa na bunge, serikali imekubali kupunguza tozo inayotozwa na Mamlaka ya Bandari nchini (THA) ya kutoka Sh. 18.10 kwa lita hadi Sh.12.05; imepunguza tozo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka asilimia 0.6 ya bei ya kununulia mafuta katika soko la dunia kwa kila lita hadi asilimia 0.4.

Hakuna mashaka, kwamba hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha ambacho kitakosekana kwenye bajeti kuu ya serikali. Kwamba kitaingia mifukoni mwa baadhi ya viongozi wake, ndio uchunguzi unaofanywa na wanaopenda nchi hii.

Pamoja na serikali kupunguza kiwango hicho cha kodi, bado wamiliki wa mafuta wamegoma kuuza mafuta yao kwa bei elekezi iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Katika kikao kati ya “wafanyabiashara” wa mafuta na EWURA kilichojadili mvutano wa bei ya bidhaa hiyo Ijumaa iliyopita, wadau hao wawili walishindwa kuafikiana na baadaye kila upande uliibuka na tamko lake.

Wakati EWURA ikisema “atakayegoma kutoa huduma ya mafuta atafutiwa leseni na atakayeuza kwa bei ya juu atatozwa faini hadi Sh. 3 milioni,” wafanyabiashara walisisitiza, “tumekuja nchini kuvuna, siyo kupata hasara.”

 Je, hapa nani atamfunga paka kengele? Bila shaka ni serikali itakayoendelea kusalimu amri kwa kukubali kupugunza sehemu muhimu ya mapato yake ili kujinusuru na hasira ya wafanyabiashara wa mafuta.

Hatua yoyote ya kufuta leseni itaongeza ukubwa wa tatizo. Ni kwa sababu, tangu serikali ilipojiondoa kwenye biashara, imebinafsisha kila kitu. Shirika la mafuta la taifa (TIPER) tayari limekufa, huku shirika la taifa la maendeleo ya petroli (TPDC) linakufa polepole.

Kufuta leseni za wamiliki wa vito vya mafuta, kutavifanya vituo hivyo kufungwa kwa muda mrefu au milele kutokana na mgomo huu kuhusisha wamiliki wote wa vituo hivyo. Hatua hiyo itainyima serikali mapato, italeta usumbufu kwa wananchi wanaotumia nishati hiyo na italeta matatizo makubwa ya kiuchumi kwa taifa.

Hapa pia kuna tatizo sugu la uhaba wa umeme nchini. Rais Kikwete na serikali yake waliahidi wananchi ifikapo tarehe 1 Julai 2011, uhaba wa umeme utabaki kuwa historia. Serikali imeshindwa kutimiza ahadi hiyo.

Baadaye waziri mkuu, Mizengo Pinda akaliambia bunge, “tunaomba muda ili turudi hapa na mpango mkakati wa kumaliza tatizo hili la uhaba wa umeme nchini.” Bali, pamoja na ahadi hiyo ya Pinda bungeni, hakuna mwenye matarajio ya serikali kuja na suluhu ya kuondoa giza linalozidi kuongezeka kila uchao na bundi anaendelea kulia mtini.

Badala yake, wengi wanatarajia serikali itakwenda bungeni 13 Agosti 2011, ikiwa na mipango mingi, lakini isiyoweza kutekelezeka. Tayari kuna taarifa serikali imeomba Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuiwezesha kununua majenereta ya kuzalisha umeme wa dharula.

Hili likifanyika, tatizo la mgao wa umeme linaweza kupugua angalau kwa muda. Lakini sharti serikali ijiandae kwa mgogoro mwingine. Ule wa NSSF kushindwa kulipa wanachama wake. Wapo wanaosema kwa jinsi mfuko huu unavyowekeza katika miradi yenye mashaka, muda si mrefu utakufa, hata kama wenyewe wanajitapa kuwa na uhai wa miaka 50 ijayo.

Kwingine ambako Kikwete inaonekana bundi amemkalia dirishani ni kuuzwa, katika mazingira ya ufisadi, kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Ndani ya mradi huo, viongozi kadhaa wa chama chake na serikali wametumbukia katika tuhuma nzito za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Dk. Didas Masaburi, mbunge wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki na diwani wa kata ya Kuvukoni, jijini Dar es Salaam, amebeba tuhuma za kuingiza kinyemela mwekezaji – kampuni ya Simon Group Limited – huku kukiwa na agizo kutoka ofisi ya waziri mkuu likimkataza kufanya hivyo.

Hadi sasa, hakuna anayefahamu Masaburi kama amelipwa kupindisha agizo la waziri mkuu au ametenda hayo ili kutekeleza kile alichoita mwenyewe, “maslahi ya umma.” Bundi anakoromea dirishani kwa rais na Masaburi.

Dk. Masaburi aliyepitishwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM kilichokuwa chini ya Kikwete kugombea nafasi ya meya, aliwahi kutuhumiwa kufilisi mradi wa mabasi ya wanafunzi mkoani Dar es Salaam.

Je, Kikwete hakujua tuhuma hizi? Hakuletewa taarifa? Kama alijua na aliletewa taarifa, nini kilimsukuma kumpitisha? Kama hakujua na wasaidizi wake hawakumwarifu, sasa anachukua hatua gani kukiokoa chama chake kilichotumbukia katika kashfa hii?

Miezi 10 ya utawala wa Rais Kikwete wa awamu ya pili, imeghubikwa na milio ya bundi. Hakuna anaposhika pakashikika. Katika maeneo mengine, hata cha kushika hakionekani. Chukua mfano ufuatao.

Hatua ya wabunge wa chama chake kuungana na wabunge wa upinzani kukataa bajeti za baadhi ya wizara bungeni, ni ishara kuwa Kikwete anakabiliwa na kibarua kigumu katika kipindi hiki cha miaka minne iliyosalia.

Hatua ya kutumia wingi wa wabunge kupitisha bajeti, haisadii serikali wala chama chenyewe. Afadhali serikali kuondoa ilichowasilisha bungeni na kwenda kurekebisha, kuliko kutumia wingi wa wabunge kupitisha kile ambacho hakikidhi mahitaji ya wananchi wengi.

Hata baadhi ya wenzake ndani ya chama, wameanza kusema chinichini, “Kama Kikwete anakipenda chama chake, vema akaamua kuitisha uchaguzi sasa kupima hadhi na umaarufu; na labda na uhalali wake.”

Bundi aliaye mtini anaashiria mwendo mgumu kwa CCM na hata anguko kuu kabla Rais Kikwete kumaliza muhula wake wa mwisho.

Sheikh Yahya Hussein, mtabiri rafiki wa serikali na CCM, hayupo tena. Haijafahamika alimwachia nani majeshi yake yasiyoonekana aliyosema ameyaelekeza kumlinda Rais Kikwete na labda chama chake. Vyovyote iwavyo, mlio wa bundi hauwezi kupuuzwa.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)